The House of Favourite Newspapers

Kwa staili hii, tumeibiwa sana Katika Miradi ya Maendeleo

0

AWALI ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuwa katika hali nzuri na salama leo, kwani kuna wenzetu wengi wamejikuta wakishindwa kuamka kama tulivyofanya mimi na wewe. Hii ni zawadi kubwa ambayo hatuwezi kumlipa Mwenyezi Mungu zaidi ya kumuomba atuzidishie rehema zake za kila siku.

Baada ya utangulizi huo ninaomba sasa nije kwenye mada yangu ya leo, ambayo nia hasa ya kuileta kwenu ni kuitaka jamii kutambua namna gani viongozi wa serikali wamekuwa wakituibia kwa muda mrefu katika miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imefanywa katika nyakati tofauti. Kilichonifanya niwaze hivi ni baada ya uzinduzi wa majengo 20 ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliofanywa wiki iliyopita na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mradi ambao licha ya kuchukua muda mfupi (miezi nane tu) pia ulitumia kiasi cha shilingi bilioni 10 tu.

Rais Magufuli aliwahi kusema kuwa alipowapa wahandisi fulani ramani ya majengo hayo akitaka wamjengee akiwa na kiasi hicho cha fedha mkononi, aliambiwa kuwa ujenzi huo ungeweza kugharimu kiasi cha kati ya shilingi bilioni 150 hadi 170, fedha ambazo alisema hana, hivyo kumfanya kutafuta mtu mwingine wa kuifanya kazi hiyo. Rais Magufuli alisema alimfuata Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Injinia Elius Mwakalinga na kumpa ramani pamoja na kutaja kiasi chake cha fedha alichonacho na kwa mshangao wake, mtendaji huyo alimhakikishia kuwa fedha hizo zinatosha.

Shilingi bilioni kumi zimeweza kujenga majengo 20 ambayo yanaweza kuhifadhi wanafunzi zaidi ya 3000, hakika hili ni jambo jema sana na kwa kweli sina budi kumpongeza Rais Magufuli kwa weledi wake katika masuala ya ujenzi. Kwa kufikiria hesabu ya kutoka bilioni 150 hadi bilioni 10, najaribu kutafakari ni kwa kiasi gani taifa letu limekuwa likiibiwa na watu wasiona nia njema, kwani kwa mazoea ya miaka mingi tuliyonayo, hata kama tungeambiwa majengo yale yamegharimu kiasi kile cha fedha, hakuna mtu ambaye angeshangaa.

 

Sasa ninaangalia miradi mingine ya ujenzi iliyogharimiwa na serikali na taasisi zake, hivi kama zingetumia mahesabu kama majengo haya ya chuo kikuu, haiwezekani kwamba shule zote za sekondari za serikali zingekuwa na majengo ya kutosha kwa ajili ya vyumba vya madarasa, maabara pamoja na nyumba za walimu? Hii inaonyesha ni jinsi gani tuna tatizo kubwa na viongozi wetu, tunaowapa dhamana ya kuongoza taasisi zetu, kwani wanazitumia kujinufaisha wao binafsi na kuwaacha wananchi wakipata mateso ambayo yangeweza kuepukika.

Kama mradi mmoja tu wa majengo ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yameweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 140 zilizokuwa ‘tupigwe’ na wajanja, je fedha hizi zisingeweza kuelekezwa sehemu zingine na hivyo kutatua kero za wananchi? Ni imani yangu kwamba pamoja na umaskini tulionao, bado tungeweza kufanya vitu vingi, hasa vinavyohusika na jamii moja kwa moja, kama kuboresha hospitali, mashule, maji safi, miundombinu na mengine kadha wa kadha.

Nimuombe rais wangu Magufuli, afuatilie pia miradi mingine inayopata fedha kutoka serikalini, kwani bado kuna watu wenye roho mbaya, wanaojali zaidi masilahi yao binafsi badala ya kutanguliza nchi yetu mbele. Kadiri tunavyoweza kuokoa fedha kutoka mikononi mwa mafisadi hawa, ndivyo tutakavyoweza kuboresha huduma za jamii kwa kadiri fedha zinavyopatikana. Nimalizie kwa kutoa wito kwa Watanzania wenzangu, hasa wale wanaopata nafasi za kuongoza taasisi na miradi ya umma, waweke mbele uaminifu wao, kwa faida ya kizazi hiki na kijacho na kuacha kusifia vitu vizuri vya Wazungu ambavyo hata sisi tunao uwezo wa kuvifanya! Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli!

 

 

Leave A Reply