The House of Favourite Newspapers

Kwa Walichopanga Monastir, Yanga Washindwe Wao Uwanja wa Mkapa Kesho

0

MSAFARA wa wachezaji, Benchi la Ufundi na Uongozi wa US Monastir ya nchini Tunisia umetua alfajiri ya jana Ijumaa huku wakitoa kauli ya kinyonge kuwa hawatatumia nguvu nyingi watakapovaana dhidi ya Yanga.

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana kesho Jumapili saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

US Monastir ambao tayari wamefuzu Robo Fanaili ya Kombe la Shirikisho Afrika katika Kundi D wakiwa na pointi 12 wakifuatia na Yanga 7, TP Mazembe 3 na Real Bamako 2.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kocha Mkuu wa US Monastir, Linos Gavriel alisema kuwa wataingia katika mchezo kwa ajili ya kukamilisha ratiba pekee na sio ushindi.

Gavriel alisema kuwa katika mchezo huo hawana cha kupoteza, kwani tayari wameshafuzu robo fainali hivyo hawatawatumia wachezaji wao muhimu na tegemeo kwa lengo la kupata majeraha wakati wana kibarua kigumu mbele ya safari.

“Hatukuja Tanzania kutafuta pointi tatu wala suluhu kwa sababu tumeshafuzu robo fainali, hivyo tutacheza mpira wa kawaida bila ya kutumia nguvu nyingi kama tulivyocheza nao Tunisia.

“Tunafahamu wapinzani wetu wanahitaji ushindi ili wafuzu hatua inayofuatia ya robo, hivyo tayari nimewaambia wachezaji wacheze kwa makini ili wamalize mchezo huo bila ya majeraha yoyote.

“Kwani tuna kibarua kigumu mbele ya safari ndefu katika michuano hii, malengo yetu ni kufika fainali hivyo sitaki kuona wakipatikana majeruhi katika mchezo huu,” alisema Gavriel.

Wakati akisema hayo, Kocha Mkuu wa Yanga Mtunisia, Nasreddine Nabi alisema: “Sitaki kuwaangalia wapinzani wangu nini wanachotaka kukifanya katika kuelekea mchezo huo.

“Ninaendelea kukiimarisha kikosi changu ili kipate matokeo mazuri ya ushindi na sio kitu kingine, nimepanga kutumia wachezaji wangu wote muhimu ili kuhakikisha tunapata ushindi wa hapa nyumbani utakaotupeleka robo fainali,” alisema Nabi.

Stori: Wilbert Molandi na Marco Mzumbe

Leave A Reply