The House of Favourite Newspapers

Kwaheri Shimon Peres Na Safari Ndefu Ya Kisiasa Israel

peres12Marehemu Shimon Peres enzi za uhai wake.

Septemba 13, 2016 vyombo vingi vya habari duniani kote vilitawaliwa na habari ya kuugua ghafla kwa mwanasiasa nguli wa nchini Israel, Shimon Peres.

Mzee huyu wakati akikimbizwa Hospitali ya Sheba Medical Center, alikuwa na miaka 93 na alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kiharusi yaliyopelekea kuvuja kwa damu kwenye ubongo.

peres…Akiwa kwenye moja ya makongamano ya kimataifa. 

Jopo la madaktari lililoongozwa na daktari bingwa, Dkt. Itzik Kreiss walijitahidi kuokoa maisha ya kiongozi huyu pasipo mafanikio, hatimaye usiku wa tarehe 27 Septemba, 2016 alifariki dunia baada ya mwili wake wote kupooza.

Historia yake

Shimon Peres, alizaliwa Agosti 2, 1923 huko Wiszniew, Poland. Kwenye familia yao walikuwa wawili, yeye na mdogo wake Gershon.

Baba yake Yitzhak alikuwa mfanyabishara na mama yake Sara alikuwa mfanyakazi wa maktaba.

Anahesabika kama mmoja wa wanasiasa wa muda wote kwenye taifa la Israel, wengi wanamuona kama baba wa pili wa taifa hilo baada ya David Ben Gurion, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa taifa hilo na ambaye anahesabika kama baba wao wa taifa.

Wakati wa uhai wake amewahi kutumikia nafasi mbalimbali nyeti serikalini.

Aliingia kwenye siasa rasmi mwaka 1959 baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Knesset, mwaka 1974 aliteuliwa na Waziri Mkuu wa wakati huo Yitzhak Shamir kuwa waziri wa usafirishaji nafasi aliyodumu nayo kwa muda wa miaka mingi.

Mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi chini ya Waziri Mkuu, Yitzhak Shamir.

Aliporejea madarakani Yitzhak Rabin, mwaka 1992 aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje hadi mwaka 1995 alipochaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Israel.

peresi…Akisisitiza jambo enzi za uhai wake.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alifanikisha mazungumzo ya amani kati ya Israel na mamlaka ya Palestina hali iliyopelekea kutangazwa kama mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1994.

Amewahi kuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili tofauti na baada ya kuachia nafasi hiyo alichaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo kutoka mwaka 2007 – 2014.

Ametumia miaka 55 akifanya kazi mbalimbali serikalini. Alikuwa mmoja wa viongozi wa juu wachache kuwahi kutumikia nafasi zote muhimu kwenye taifa hilo.

Ameacha watoto watatu Zvia, Yoni na Chemi, mkewe Sonya Gelman alifariki dunia mwaka 2011.

shimon…Akiwa kwenye moja ya dhifa za kitaifa kipindi akiwa Rais wa Israel.

Baadhi ya tuzo alizoshinda enzi za uhai wake.

1994- Tuzo ya amani ya Nobel.

2008- Alitunukiwa Udaktari wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha King’s College London.

2012- Tuzo ya Presidential Medal Of Freedom kutoka kwa Rais Barrack Obama wa Marekani.

Viongozi mbalimbali duniani wamehudhuria mazishi hayo, miongoni mwao ni Rais wa Marekani Barrack Obama; Katibu Mkuu UN Ban Ki-moon; Kansela wa Ujerumani Angela Merkel; Rais wa Ufaransa Francois Hollande; Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau; Waziri Mkuu wa Australia Malcolm Turnbull na Rais Wa Mexico Enrique Pena Nieto.

Marehemu Shimon Peres amezikwa leo Ijumaa kwa heshima zote. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. AMINA.

Na Leonard Msigwa/GPL.

 

Comments are closed.