The House of Favourite Newspapers

Kwaheri The Undertaker

FLORIDA, MAREKANI|  CHAMPIONI| MAKALA ZA BURUDANI

JUMAPILI Iiliyopita kulifanyika tamasha kubwa la mieleka ambalo kwa mwaka huwa linafanyika mara moja, linajulikana kwa jina la WWE WrestleMania ambapo mwaka huu lilikuwa likifanyika kwa mara ya 33 tangu kuanzishwa kwake.

Kulikuwa na matukio mengi ya mastaa wa mchezo huo kutwangana lakini kilichogusa hisia za wengi ni tukio la mpiganaji mkongwe The Undertaker kupoteza pambano kisha kuamua kustaafu mchezo huo.

The Undertaker alitangaza kustaafu kwa ishara na siyo kwa kitamka, kwani alikuwa akipambana dhidi ya Roman Reigns mwenye umri wa miaka 31, alipoteza pambano hilo ikiwa ni mara yake ya pili kupoteza katika historia ya ushiriki wake katika WrestleMania.

Kumpiga The Undertaker hadi kukubali kuwa ameshindwa siyo kazi ya ‘kitoto’, kwa wale wafuatiliaji wa mchezo huo wa zamani na hata sasa wanatambua jinsi ambavyo mpiganaji huyo alivyo sugu katika kupigana.


Baada ya pambano kumalizika, mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 52, hakuamini kilichotokea, ilipogongwa kengele ya kumaliza pambano, aliendelea kulala kwa muda, akainuka taratibu na kuanza kuzunguka kwenye ulingo kwa muda kama anayetafakari kitu.

Baada ya muda akavua koti lake kubwa jeusi, akavua ‘gloves’ na kofia kisha vyote akaviweka katikati ya ulingo na kuondoka.

Hiyo ikiwa ni ishara ya kuwa amemaliza kazi na amekubali kushindwa, baada ya hapo akatoka ulingoni taratibu huku mashabiki wakimtazama kwa huruma kama vile hawaamini mwisho wa enzi umewadia.

Baada ya kufika nje ya ulingo akasogea sehemu ya mashabiki, kisha akamfuata mkewe, Michelle McCool akambusu na kumkumbatia kitu ambacho hakuwahi kukifanya kwa kuwa haikuwa kawaida yake kufanya hivyo, baada ya hapo akaondoka.

Uamuzi wa kustaafu ameuchukua kutokana na umri kumtupa mkono kwani amekuwa katika mchezo huo wa mieleka kwa miaka 27, akipambana na mastaa wengi ambao enzi zao zilipita lakini yeye akiendelea kubaki.

Baadhi ya mashabiki wa WWE walimwaga machozi wakati alipokuwa akiondoka kutokana na mchango wake kwenye mchezo huo.

Hivyo hadi anafikia hatua ya kustaafu rekodi yake katika Wrestlemania inasomeka 23-2, ikiwa na maana ameshinda mapambano 23 na kupoteza mawili.

Katika pambano lake la Jumapili ambalo lilikuwa la mwisho, alionekana kuchoka zaidi ya ilivyo kawaida yake, huku akikubali mpinzani wake huyo kumshambulia muda mrefu na hata alivyomlaza chini na kukubali mwamuzi kupiga chini mara tatu, kulionyesha wazi nguvu zimepungua.

Enzi zake ilikuwa ni nadra kuona anapoteza pambano kirahisi tofauti na ilivyokuwa Jumapili iliyopita.

Akimzungumzia mkongwe huyo, Reigns ambaye ndiye aliyemstaafisha alisema: “Kama umekuwa mmoja wa watu katika biashara hii, unatakiwa kuelewa kuwa huu ni mchezo na kila mtu anamheshimu Undertaker.

“Kwa kuwa ni kazi yangu lazima nifanye kile nilichokifanya. Mimi ni chipukizi, nina familia na ninatakiwa kubeba majukumu, hicho ndicho nilichokifanya.”

Maoni na shukrani kwa Undertaker yalikuwa mengi kutokana na jinsi alivyokuwa akimheshimika kwenye mchezo huo.

Inaeleweka wazi kuwa Undertaker ambaye jina lake halisi ni Mark William Calaway siyo mzungumzaji sana lakini matendo yake yamekuwa kivutio kwa wengi kutokana na kuwa na matendo ya kipekee alipokuwa akiingia ulingoni, ikiwemo kuingia ukumbini akiwa ndani ya jeneza.

ALIPOTOKA THE UNDERTAKER

Alianza kupigana mieleka mwaka 1984, alianza kupata umaarufu baada ya kumpiga Hulk Hogan aliyekuwa mbabe wa mchezo mwaka 1991 ndipo dunia ikaanza kumfahamu.

Undertaker ni mzaliwa wa Texas, enzi zake wakati anasoma alikuwa ni mchezaji wa kikapu na soka, akiwa ngazi ya chuo alikuwa ni mchezaji mzuri wa fani hizo na hata alipohitimu mwaka 1983 akafikiria kuwa mwanamichezo wa kulipwa wa kikapu.

Baadaye alibadili mawazo na kuamua kuongia kwenye mieleka akianza kwa kujiita jina la Texas Red, jina lililotokana na sehemu aliyozaliwa na kukulia.

Mwaka 2013, The Undertaker alipigiwa kura na mashabiki kuwa mwanamieleka bora kuwahi kutokea katika WWE.

NDOA

Alifunga ndoa yake ya kwanza na Jodi Lynn mwaka 1989, wakabahatika kupata mtoto wa kiume lakini walitalikiana mwaka 1999. Akaoa mke mwingine Sara mwaka 2000, wakapata watoto wa kike wawili lakini pia waliten-gana mwaka 2007.

Mwaka 2010 alifunga ndoa na Michelle McCool aliyekuwa ni mpiganaji mieleka pia ambapo wamebahatika kupata mtoto mmoja aliyezaliwa Agosti 29, 2012.

Calaway au Undertaker ni shabiki wa mchezo wa ndondi na amewahi kuhudhuria mapambano ya Pacquiao vs Velázquez na Lennox Lewis vs Mike Tyson

MKE WA THE UNDERTAKER

Mke wa Undertaker wa sasa, Michelle McCool aliwahi kuolewa na aliyekuwa mpenzi wake wa siku nyingi, Jeremy Louis Alexander, lakini wawili hao walitalikiana mwaka 2006.

Baada ya hapo alielekeza nguvu kwenye mchezo wa mieleka kabla ya baadaye kuangukia kwenye mikono ya mbabe huyo.

Amewahi kupata majeraha makubwa katika mchezo huo wa mieleka ikiwemo kuvunjia pua na mbavu. Aliamua kustaafu kupigana mieleka Mei 1, 2011, kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya mguu kwa miezi miwili huku kidole gumba chake kikiwa kimevunjika.

Mwaka 2016, McCool alieleza kuwa anasumbuliwa na saratani ya ngozi na hivyo alilazimika kutoa sehemu ngozi yake kwa ajili ya kukwepa kusambaa kwenye mwili wote.

The Undertaker
Kuzaliwa: Machi 24, 1965
Wake:
Jodi Lynn (1989-1999)
Sara Frank (2000-2007)
Michelle McCool (2010- sasa)
Watoto: 4
Majina ya utani
The Commando
Kane the Undertaker
Dice Morgan
The Master of Pain
The Punisher
Texas Red
Urefu: Futi 6 inchi 10
Kuanza mieleka: 1984
Kustaafu: Aprili 2, 2017

Rekodi Mpinzani Mwaka
1-0 Jimmy Snuka 1991
2-0 Jake Roberts 1992
3-0 Giant González 1993
4-0 King Kong Bundy 1995
5-0 Diesel 1996
6-0 Sycho Sid 1997
7-0 Kane 1998
8-0 The Big Bossman 1999
9-0 Triple H 2001
10-0 Ric Flair 2002

Rekodi za The Undertaker katika Wrestlemania

11-0 Big Show na A-Train 2003
12-0 Kane 2004
13-0 Randy Orton 2005
14-0 Mark Henry 2006
15-0 Batista 2007
16-0 Edge 2008
17-0 Shawn Michaels 2009
18-0 Shawn Michaels 2010
19-0 Triple H 2011
20-0 Triple H 2012
21-0 CM Punk 2013
21-1 Brock Lesnar 2014
22-1 Bray Wyatt 2015
23-1 Shane McMahon 2016
23-2 Roman Reigns 2017

Comments are closed.