The House of Favourite Newspapers

Kwani Yanga Wenyewe Wanasemaje

0

ZIMEBAKI siku nne kabla ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, kupigwa Jumamosi Mei 8 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Simba wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa wanajiamini zaidi kutokana na ubora ambao wamekuwa wakiuonyesha kwenye michuano ya Caf pamoja na kwenye ligi kuu na Kombe la Azam Sports Federation’s Cup.

 

Mashabiki wa Simba wamekuwa na furaha na kikosi chao, na first eleven yao ndiyo inayowapa jeuri, huku wengi wakiamini kuwa kama watawapangia Yanga full mkoko basi hawawezi kuchomoka siku hiyo.

 

Kuwa na kikosi kipana pia imekuwa sababu kubwa kwa mashabiki wa Simba kuvimba hasa katika safu yao ya ushambuliaji ambapo mara nyingi kocha Didier Gomes hufanya mabadiliko ya mara kwa mara.

 

Kuna muda kocha huyo humtumia Meddie Kagere ambaye ndiye kinara wa mabao kwa timu hiyo akifunga mabao 11 na mara nyingine humtumia Chris Mugalu aliyefunga mabao 8 mpaka sasa.

 

Licha ya hao pia mshambuliaji mzawa John Bocco amefanikiwa kufunga mabao 10 ambayo yanamfanya kocha Didier kuanza na mshambuliaji yeyote jambo ambalo linazidi kuwapa jeuri mashabiki wa Simba.

 

Kikosi cha maangamizi cha Didier Gomes ambacho kinaweza kutumika kuwaangamiza Yanga siku ya Jumamosi huenda kikaundwa na wachezaji wafuatao:

 

Aish Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Sergie Wawa, Thadeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Bernard Morrison, Clatous Chama, Luis Miquissone na Meddie Kagere.

 

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, alisema kuwa kama inavyokuwa siku zote malengo yao ni kuibuka na ushindi katika kila mchezo basi watahakikisha wanatimiza wajibu huo kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Yanga, japo anaamini haitakuwa rahisi kwake.

 

“Malengo ya timu kiujumla ni kuibuka na ushindi katika kila mchezo, tunahitaji kupata ushindi ingawa siyo rahisi, hivyo tutapambana na wala halikwepeki hili.”

 

Naye nahodha John Bocco alisema: “Mechi haitakuwa nyepesi kutokana na ubora wa Yanga, wanacheza vizuri na wanafanya vizuri kwa sasa, hivyo ili tupate matokeo tunahitaji kupambana.”

 

Kwani Yanga wenyewe wanasemaje? Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Saido Ntibazonkiza, alisema: “Mchezo wetu na Simba wala sina wasiwasi kuelekea mchezo huo, sisi tunajiandaa kwenda kupata ushindi.

 

“Niseme watu wasikariri matokeo. Mimi binafsi sina presha, huwa siangalii mechi zao, nachoangalia ni namna gani timu yetu itafikia malengo.”

 

Kumbukumbu ya mchezo wa kwanza ambao ulikuwa ni wa mzunguko wa kwanza, Yanga akiwa mwenyeji wa mchezo, matokeo yalimalizika kwa sare ya bao 1-1, bao la Yanga likifungwa na Michael Sarpong kwa penalti huku la Simba likifungwa na Joash Onyango kwa kichwa.

MARCO MZUMBE,

Dar es Salaam

Leave A Reply