The House of Favourite Newspapers

KWANINI UKUNALI KUTESEKA KISA ETI UNAMPENDA?

NI WIKI NYINGINE tulivu kabisa tunakutana kupitia ukurasa huu nikiamini kwamba Mungu amekupa nafasi nyingine ya kuendelea kuishi. Hili ni jambo la kushukuru sana kwani wapo ambao leo hii wapo kaburini na wengine wanateseka mahospitalini.

 

Mpenzi msomaji wangu, tunapozungumzia maisha, hakika mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana. Ndiyo maana ukijaribu kufuatilia utabaini kwamba watu wengi wanafanya kazi kwa juhudi ili wapate pesa na mali lakini wakishapata kisha wakakosa ladha tamu ya mapenzi, maisha yao huyumba na wengine hujikuta hata wakipoteza maisha.

 

Wapo ambao wana pesa nyingi tu lakini kwa sababu mapenzi ya dhati yamekosekana kwao, wanaona hata umuhimu wa kuendelea kuishi haupo. Hivyo basi, mimi na wewe tunahitaji kuwa na wapenzi tena wenye mapenzi ya dhati ili maisha yawe ni yenye furaha na amani.Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, wapo wanaochukulia mapenzi kama kitu rahisirahisi. Hapa namaanisha hivi, mtaani kuna watu wa aina mbili.

Kuna ambao wanajua kweli kupenda. Akisema anampenda fulani, anamaanisha na kuna wale ambao wanaweza kusema wamependa kumbe hamna lolote.Unamkuta mwanaume anadanganya kuwa ametokea kumpenda msichana fulani na ana dhamira ya kufunga naye ndoa lakini kumbe hana lolote, nia yake amuonje kisha aingie mitini.

 

Achilia mbali hao, kuna wanaume ambao wanatumia pesa na utaalam wao wa kuongea kuwarubuni wasichana ili watembee nao kwa kipindi fulani kisha wakisharidhika, wanawaacha. Wavulana hao wapo na wamekuwa ni tatizo kubwa huko mtaani. Lakini pia wapo wasichana ambao wenyewe wanajiita wa mjini. Yaani wao hawajui kupenda, wanachoangalia ni mwanaume ‘mwenye nazo’. Wakishampata, watajifanyisha kuwa na mapenzi ya dhati kupita maelezo kumbe hamna kitu, usanii mtupu!

 

Katika mazingira hayo sasa utaona ni kwa jinsi gani mapenzi yamekuwa janga. Ndiyo maana leo hii kuna wanaotamani kutojihusisha na mambo ya mapenzi kwa sababu hizihizi za usanii na ujanjaujanja mwingi. Wakati mambo yakiwa hivyo, kuna baadhi ya watu ambao wamekithiri kwa tabia ya kuwatesa wapenzi wao kisa wameoneshwa kuwa wanapendwa sana.

 

Wapo watu ambao wakipenda wamependa kweli na hawawezi kujizuia kuonesha hisia zao kwamba ‘wamekufa’. Hatua hiyo sasa hivi badala ya kuwa changamoto kwa aliyependwa ili naye aongeze mapenzi, inakuwa tatizo.

 

Uchunguzi umebaini kuwa, mwanaume akioneshwa kupendwa sana na mwanamke, atavimba kichwa na kumfanyia mwenzake kila aina ya visa eti kwa kuwa amebaini amezimikiwa. Hili halipo kwa wanaume tu. Wapo wanawake ambao nao kwa kujua kuwa waume  zao ‘wamekufa’ kwao, dharau inaongezeka, heshima inapungua na kufanya hata yale ambayo wanajua yanawakera wenzao.

 

Hivi kwa nini tufikie hatua ya kuwaliza na kuwanyanyasa watu ambao wameshindwa kujizuia kuonesha mapenzi yao kwetu? Kama ulikuwa hujui basi leo tambua kuwa, anayekupenda kwa dhati kisha wewe ukamfanya kila siku ni wa kulia, chozi lake haliendi bure.

 

Inaweza kuwa ni tatizo kwako na hata pale atakapoamua kunyoosha mikono juu, unaweza kushangaa unakutana na majanga kibao na kujutia uliyokuwa unayafanya. Mimi nadhani kama humpendi mtu ni vyema ukamwambia mapema ili ajue kwamba, kama atatumia nguvu na muda wake mwingi kwako, ni kazi bure.

Unapokubali kuwa na wewe unampenda kisha baadaye unaanza kumfanyia vioja, ni dhambi hata kwa Mungu.

Iko hivi, kama kweli unampenda, mdhihirishie kwa matendo ili asiwe na shaka kwamba huenda ameingia kwenye penzi la kisanii. Kama yeye amekutamkia kuwa anakupenda lakini wewe ukahisi huna mapenzi naye, kuwa muwazi kwake ili ajue wazi amempenda mtu ambaye hampendi!

 

Lakini pia katika hili naomba niseme kwamba, wewe ambaye umetokea kupenda sana, ukibaini huyo uliyempenda hana mapenzi ya dhati kwako, muache. Usilazimishe penzi maana ukilazimisha sana, huenda akakukubalia lakini baada ya hapo utakuwa ni mtu wa kulia kila siku. Utasalitiwa sana na unaweza kujikuta unageuzwa tairi ya spea.

 

Kuwa makini sana na maisha yako, pasipo na penzi usilazimishe na kama anayekuambia anakupenda humpendi, mwambie wazi kwamba hana nafasi kwenye moyo wako.

Comments are closed.