KWANINI WANAUME WANATAKA TENDO TU NA SIYO KUOA ?-2

WIKI iliyopita nilileta mada hii kwenu na kwa kweli mwitikio wake umekuwa mkubwa hivyo ngoja nimalizie ujumbe wangu niliolenga kuufikisha. Ukweli ni kwamba siku hizi majukumu ya baba kama kichwa cha familia yamebadilika. Kwa asili wanaume wameumbwa na kiu ya kuongoza, kutaka kuwa wasimamizi au kila kitu kwenye maisha yao, kwenye vipaji vyao, kwenye kazi zao, kwenye uhusiano wao na hata kwenye familia zao. Pamoja na kiu hii, kwa miaka ya karibuni hali imebadilika, maendeleo ya kijamii na kiteknolojia yameondoa ule ukuu aliokuwa nao baba.

Leo kwenye familia nyingi, baba hawezi tena kumuadabisha mtoto wake maana anaweza kumshtaki na kumpeleka mahakamani. Leo katika jamii nyingi duniani, kwenye nchi zilizoendelea na hata hizi zetu zinazojikongoja, baba akisema atumie mamlaka yake kama baba haiitwi tena mamlaka inaitwa unyanyasaji.

Sasa hivi kila mwanamke anataka usawa, ukifanya hivi mke atafanya vile, ukitaka hiki na yeye atataka kile, ndoa nyingi zimeshakuwa kama chama tawala na upinzani, wanandoa wengi wameanza kuishi kama taasisi na siyo kama wapenzi. Inasemekana kwamba kama ile kiu ya baba au mwanaume kuhangaika na kuwekeza jasho na akili yake kwenye familia yake ili aiongoze, awe kichwa imeoza au haileti faida, basi hakuna anayeona umuhimu wa jitihada hizo tena.

Imekuwa kama mfanyabiashara, anaona ya nini kuwekeza ambako una uhakika patakupa hasara? Maana ya hii ni kwamba, hamasa ya wanaume kuingia kwenye ndoa imeonekana kupungua na hivyo kulitafuta hitaji lao la asili ya tendo la ndoa nje ya ndoa.

Sheria za ndoa zinawabana wanaume zaidi. Wanaume wengi wameonesha kuhofia sheria za ndoa kwa jinsi zinavyomgandamiza mwanaume na kumpa chapuo mwanamke. Wanaume wengi wanasema wana hofu ya kuingia kwenye makubaliano tena ya maandishi ya kuishi pamoja maishani wakati makubaliano hayo yanamuelemea mtu mmoja na siyo wote, husuan pale mambo yanapoonekana kuharibika baina yao.

Nyakati ndoa zinapovunjika na wanandoa wakalazimika kuchukulia mambo kisheria, mwanaume anahofia kupoteza kila anachonacho. Pamoja na kwamba upo ukweli kwamba hata kama mwanaume ndiye alitafuta, lakini kuna watoto nao wanatakiwa kufaidika au kuendelezwa pamoja na kwamba ndoa imeshindikana, lakini wengine wanasema hata kama hakuna watoto, bado mwanamke ana nafasi kubwa ya kumbana mwanaume kisheria.

Pamoja na kwamba hofu hii haionekani kwa wanaume wa nchi kama ya kwetu ila wapo baadhi wenye mtazamo huu. Kwa mtazamo huu, wengi wanaona bora waendelee kutafuta tendo la ndoa halafu hayo mambo ya kuishi pamoja yatajulikana huko mbele.

Hamasa ya kukua na kupevuka imepungua. Kuendesha familia kunahitaji kumaanisha na kujitoa, pasipo tabia hizi utabaki kuitwa baba au mume, lakini lazima kutakuwa na upungufu mwingi na malalamiko kwenye familia.

Kwa bahati mbaya inaonekana tabia hizi za kumaanisha zinapungua kwa kasi kwa wanaume wengi. Vijana wanaonesha uvivu na kukwepa majukumu wakiwa wadogo. Wanachukia kazi na kuwa walegevu. Wanapenda vitu virahisi na maisha ya anasa. Mtu anatamani aangalie televisheni siku nzima na asifanye kazi.

Familia nyingi zimepwaya kwenye suala la malezi. Mwanaume hapangiwi majukumu ya kumfanya ajitume akiwa nyumbani. Akitoka shule, basi ni kucheza na kukaa tu na baadaye wazazi haohao waliomfundisha aina hiyo ya maisha wanakuja kuanza kulalamika eti huyu mtoto ameharibuka wakati wao wenyewe ndiyo waliomharibu. Kwa bahati mbaya, tabia hizi za kivivu na kilegevu na kukwepa majukumu huendelea hadi wanapoingia kwenye ndoa. Mtu anaingia kwenye ndoa hata tabia ya kuhifadhi fedha kwa matumizi ya dharura hana, akipata pesa ni starehe tu.

Mtu anapata mke hajui hata namna ya kumhudumia, mtoto akizaliwa ndiyo kabisa vita kila siku na mkewe maana ni kama vile huyo mke wake analea watoto wawili wakati mmoja anajiita baba. Kwa hali hii vijana wengi wanaogopa majukumu ya kifamilia, wanaishia kutaka tendo la ndoa tu na hata kijana wa aina hii anapokuwa kwenye familia hafanyi kitu cha ziada, mke ndiyo jembe la nyumba, kijana yeye anasubiri kupewa unyumba tu.

Kufuatia hali hii, baadhi ya wanawake wamekata tamaa au kuchukia kuolewa, wako tayari wafurahie maisha na kufanya mapenzi na mwanaume wanayemtaka ila pasipo masharti, akihitaji mtoto, basi atampata kwa muda wake bila kujali baba ni nani au anaishi wapi. Maisha yameba-dilika!

 


Loading...

Toa comment