The House of Favourite Newspapers

Kwenye hili la mabadiliko, kuna hatari gani tukitofautiana?

0

2. Umati wa watu waliohudhuria mkutano wa CCM, Usa River janaSIKU za kuelekea uchaguzi mkuu zinazidi kusogea huku joto lake likipanda, maana hali ya siasa ilivyokuwa jana, sivyo ilivyo leo, kila kambi zinajitabiria ushindi.

Kuna jambo moja linaloendelea hivi sasa miongoni mwa wafuasi wa vyama hivyo, hususan Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo kwa vyovyote ndivyo vitakavyoibuka kinara baada ya wapiga kura kufanya maamuzi yao Jumapili ya Oktoba 25, mwaka huu.

Jambo hili ni dalili za kuwepo kwa uadui kati yao badala ya upinzani wa kidemokrasia. Watu wanawaona wenzao wanaotofautiana nao mtizamo kama maadui, kiasi cha kufikia sehemu na kuamua kuwatisha, kuwatukana na hata kuwakebehi, kwa sababu tu hawamuungi mkono mgombea wanaomuunga mkono wao.

Lakini bahati mbaya, wote wanaimba wimbo wa mabadiliko. Ajabu, kila mmoja anaamini mabadiliko anayotaka yeye ndiyo bora kuliko ya mwenzake. Hii inaongeza mkanganyiko mitaani na kama tusipowekana sawa katika hili, ipo hatari ya ushindani wetu wa kisiasa kugeuka kuwa uadui kabisa, wa chui na paka.

Kila Mtanzania anataka mabadiliko, bila kujali kama yatatokea ndani au nje ya CCM. Wanaotaka yatokee nje, wanaamini hayawezi kupatikana ndani kwa sababu tuna miaka zaidi ya 50 sasa hatujapata ahueni, wakati walio ndani wanadai kuwa huu ndiyo wakati wa kukisafisha chama chao, ili kiendeshe serikali inayowajali wananchi.

Na mabadiliko yenyewe ambayo kila Mtanzania anayasubiri ni upatikanaji wa huduma bora za jamii bila kulazimika kutoa michango isiyo na tija au rushwa, uwajibikaji wa viongozi katika idara zote za serikali na udhibiti wa mianya yote inayowawezesha watumishi wa umma kujilimbikizia mali.

Watu hawataki badiliko la sura ya mtu, wanataka vijana wao wapate elimu bora, huduma za uhakika za afya, upatikanaji wa maji safi na salama kwa muda wote, umeme wa bei nafuu, fursa za ajira na kujiajiri.

Na zaidi, wanataka kuona rasilimali zao nyingi zilizopo zinawanufaisha badala ya kushuhudia viongozi wakipata utajiri wa kutisha huku wao wakiogelea katika umaskini. Maana inashangaza kuona tuna madini ya kila aina, gesi, mafuta, bahari, mito na maziwa, misitu mikubwa ya mbao, mbuga za wanyama na vivutio vingi vya utalii lakini eti bado ni maskini wa kutupwa.

Haya ndiyo mabadiliko wanayotaka, yenye kubadilisha aina ya maisha wanayoishi sasa, siyo kila siku wanabambikiwa kesi na polisi, halafu wanaenda kukamuliwa fedha ili warudishiwe uhuru wao.

Katika kutafuta mabadiliko haya, lazima watu watofautiane, kwa sababu kila mmoja ana jinsi yake anavyoona mabadiliko yakija. Watu wote hatuwezi kumpigia kura mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli au wa Ukawa, Edward Ngoyai Lowassa.

Sasa mtu anapoamua kumshabikia Lowassa aachwe amshabikie kwa sababu ana masilahi naye na yule anayefanya hivyo kwa Magufuli naye aachwe. Siyo kama baadhi yetu wanavyofanya kutaka kulazimisha watu wote tumuunge mkono mgombea wanayemtaka wao.

Sisi wote ni Watanzania, sasa asiwepo mtu anayejifanya yeye ni Mtanzania zaidi kuliko mwenzake, eti atulazimishe tumchague fulani, kama wewe una haki ya kumchagua unayemtaka, hata na yeye pia anayo haki hiyo. Tukijua hili, hatutaweza kugombana kwa sababu mwisho wa siku, kila mmoja atakuwa ametumia vyema haki yake ya kidemokrasia.

Uchaguzi huu utapita na maisha yataendelea. Kitu kimoja ambacho hatujui ni kuwa hawa wanasiasa wanaotaka kutugawa, wenyewe hawana mpango wa kugawana. Hukutana na kukaa meza moja wakijadili dili zao, bila kujali kama ni Ukawa au CCM, sasa ajabu wewe unataka uadui na mtu kwa sababu tu hamuungi mkono mgombea wako!

Leave A Reply