The House of Favourite Newspapers

Kwenye Kampeni, Tuepuke Kauli Mbaya,Uchochezi

Mgombea ubunge wa Cuf Jimbo la Kinondoni, Rajabu Salim Juma (kulia) akitambulishwa.

KWANZA kabisa naomba mimi na wewe msomaji wangu tumshukuru Mungu kwa kutufanya leo tuwe tunapumua. Mimi nina afya njema hakika namhimidi daima.

 

Baada ya kusema hayo leo nazungumzia kampeni ambazo vyama vilivyosimamisha wagombea ubunge katika majimbo ya uchaguzi ya Siha na Kinondoni zimeanza kwa kasi kubwa.

 

Miongoni mwa vyama ambavyo vimesimamisha wagombea ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ni wazi kwamba viongozi wa serikali watashiriki katika kampeni hizo na hakuna mwiko kwa waziri kushiriki katika kampeni hizo.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu (katikati) akisindikizwa na wanachama wa Chadema.

Ni tumaini la kila Mtanzania kwamba viongozi hao watashiriki kampeni bila kujichanganya, yaani kutohusisha shughuli zao za kiserikali na chama ili kuepusha kesi siku zijazo.

 

Nimesema hivyo kwa sababu nimewahi kushuhudia baada ya chaguzi wagombea kupinga matokeo kortini kwa madai kwamba kuna kiongozi wa serikali alitumia vibaya madaraka yake kwa kushawishi watu kwa kutumia cheo chake.

 

Hii husababisha baadhi ya kesi kufikishwa mahakamani baada ya kumalizika kwa uchaguzi na walalamikaji kuwataja baadhi ya viongozi wa serikali kwamba walitumia ofisi zao kujaribu kushawishi wapigakura kumchagua mgombea wao.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba (kushoto) akimtambulisha mgombea ubunge jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia (CCM).

Waziri kupanda jukwaani na kusema fulani mkimpa kura wizara yangu itafanya a, b, c au kutumia magari ya serikali kwenye kampeni za uchaguzi ni makosa kwa sababu huko nyuma tuliwahi kushuhudia chaguzi mbalimbali zikitenguliwa kutokana na kauli kama hizo.

 

Huwa wenyewe wajuzi wa sheria wanasema kauli kama hizo zinakiuka misingi ya utawala bora na kauli hizo huwa zinaichafua serikali kwa kuonekana kuwa inaweza kuwasaidia wananchi iwapo watamchagua mgombea wa chama fulani wakati inajulikana jukumu la serikali ni kushirikiana na mtu yeyote aliyechaguliwa na wananchi ili awawakilishe.

 

Kama nilivyosema awali kauli kama hizo zinaweza kuwafanya wagombea wa upande fulani kwenda mahakamani iwapo itatokea mgombea wa chama hicho ameshindwa hivyo rasilimali nyingi za walipa kodi kuishia katika kulipa wanasheria wa serikali kushughulikia kesi ambazo zingeweza kuepukika na pia kuweka uwezekano wa uchaguzi kurudiwa na hivyo fedha nyingi zaidi kutumika kuendesha uchaguzi mdogo.

 

Fursa ambayo chama kimoja kinapata kutokana na kuaminiwa na wananchi kuendesha serikali isitumiwe vibaya na waliopewa dhamana hasa kwenye siasa kwa sababu inaweza kuigharimu serikali.

 

Ni vizuri viongozi wa serikali wanaposhiriki katika shughuli za kampeni wajiepushe na matamko ambayo yanahusisha nyadhifa zao katika kuhudumia wananchi.

Kwa mfano, siyo vema kwa mkuu wa wilaya kusimama na kusema hadharani kwenye kampeni za uchaguzi kwamba wafuasi wa upande fulani ni wakorofi na watashughulikiwa, hiyo haileti picha nzuri kwa sababu yeye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya wilaya.

 

Nasema hivyo kwa sababu wapinzani wake wanaweza kuleta madai kwamba mkuu huyo wa wilaya ametumia madaraka yake kuwashughulikia kisiasa hata kama vurugu zitasababishwa na wafuasi wa chama hicho.

Nimeamua kuwatahadharisha wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na hata mawaziri kuwa makini na kauli zao wanazotoa kipindi hiki cha kampeni kwenye mikutano ya kampeni za kisiasa kwa kuwa zinaweza kuichafua serikali mahakamani.

 

Kampeni za uchaguzi wa wabunge ni siasa hivyo neno moja linaweza kuleta taswira kubwa na hasi na hivyo kuharibu taswira nzuri ya serikali kwa baadhi ya wananchi.

Nasema hivyo kwa sababu suala la kutenganisha shughuli za kisiasa na za chama tawala na serikali ni la kikatiba, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuonyesha mfano kuwa wanaweza kufanya shughuli za vyama vyao bila kutumbukiza uwezo wao wa mamlaka ya kiserikali kufanikisha mambo ya chama kimoja.

 

Viongozi wanaoshiriki kampeni za uchaguzi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa serikali haingii lawama kila mara wakati wana uwezo wa kuiepusha na lawama hizo kwa kuwa makini katika kauli zao majukwaani.

Lakini kwa upande wa wapinzani nao wana wajibu wa kueleza kile kilicho cha kweli na siyo kueneza uongo na uchochezi.

 

Penye ukweli kwamba serikali imetekeleza hiki na kile wasiwe na haya kuyasema lakini kwenye kukosoa, wakosoe kwa sababu ndiyo demokrasia yenyewe. Wajiepushe kabisa na kusema uongo au kufanya uchochezi ili wananchi waichukie serikali yao.

Ndugu zangu, mimi naamini wote tunajenga nchi moja, hivyo kampeni hizi zisitutenganishe kwenye mshikamano wetu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

NAPASUA JIPU NA ERIC SHIGONGO |DAR ES SALAAM

Comments are closed.