Kartra

Lamine Afunguka Kila Kitu, Yanga Wagoma

LICHA ya uongozi wa Yanga kufunguka kuwa sakata la nidhamu la nahodha wa timu hiyo, Lamine Moro limemalizwa, nahodha huyo ameibuka na kufungukia kila kitu kuhusu ishu hiyo akikana kuhusika na utovu huo wa nidhamu.

 

Hivi karibuni, Lamine aliondolewa kikosini kwenye kambi ya Yanga iliyokuwa ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC, kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Lamine alisema: “Si kweli kuwa mimi ni mtovu wa nidhamu kama ambavyo imekuwa ikiongelewa na baadhi ya watu ikiwemo viongozi wa Yanga, kabla hatujasafiri kwenda Mtwara nilipata majeraha ambayo benchi la ufundi walilifahamu, tulipofika Mtwara sikufanya mazoezi, lakini nilikuwepo pamoja na timu.

 

“Kocha aliuliza madaktari kwa nini sifanyi mazoezi, akaambiwa kuhusu majeraha yangu, lakini alisisitiza kwamba nilitakiwa kufanya mazoezi, nikamweleza kuhusu hali yangu lakini alionyesha kutoniamini, kiasi cha kupimwa kwa mara nyingine na ikathibitika kuwa nina majeraha.

 

Siku ya mwisho ya mfungo wa Ramadhani, sikuamka vizuri, hivyo sikwenda mazoezini, na kutokana na hilo meneja wa timu akanieleza kuwa kocha anahitaji kikao cha pamoja, nikakubali na kwenda kuswali kabla ya kikao.“Niliporudi sikukuta mtu yeyote sehemu ya kikao, nikarudi chumbani kwangu.

 

Saa mbili baadaye, meneja akanipigia kunijulisha kuwa uongozi umesema natakiwa nirudi Dar es Salaam, sikusema chochote nikaondoka Mtwara lakini nilikutana na Engineer (Hersi Said) uwanja wa ndege.

 

Baadaye nikaona Ofisa Habari, Hassan Bumbuli amechapisha taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram kwamba sina nidhamu, nilipigana na kocha hivyo ameniamuru niondolewe kikosini. Nikampigia simu Engineer na Dr. Msolla mara kadhaa lakini wote hawakupokea simu zangu.

 

“Hata nilipomtumia ujumbe Dr. Msolla aliusoma, lakini hakunijibu chochote, nikakaa kimya. Hakuna aliyenitafuta mpaka alipofanya hivyo, Kaimu Katibu Mkuu aliponipigia Mei 27, kwamba wananihitaji ofisini.”Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuzungumzia suala hilo alisema: “Kwa sasa sitaki kuzungumza chochote.”


Toa comment