‘Lampard Anaweza Kuipa Ibingwa Chelsea’
FRANK Lampard anaweza kuirejesha Chelsea katika vita ya kuwania ubingwa wa Premier, lakini kama tu atapewa muda na uhuru kama anaopewa Jurgen Klopp pale Liverpool.
Hayo ni maoni ya kocha wa zamani wa Chelsea, Glenn Hoddle, ambaye anaamini Lampard lazima apewe sapoti katika soko la usajili na mmiliki Roman Abramovich.
Lampard ameiongoza Chelsea hadi nafasi ya nne kwenye msimamo na ikiwa mbioni kupata mwaka mwingine wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu klabuni hapo.
Hoddle anaamini Lampard hadi sasa anakwenda vizuri, lakini anahitaji sapoti ili aende kwenye hatua inayofuata.
“Unapoangalia kikosi chake, unashangaa kitu gani kinaendelea juu yake kuhusu usajili. Kwangu mimi, Frank anahitaji sera wazi ya usajili ili kuipeleka mbele timu yake.
“Anaipeleka vizuri mazoezini, kwenye soka mambo ni sawa, lakini hatua nyingine kubwa kwake itakuwa ni jinsi klabu inavyofanya usajili.
“Kama Frank akipata wachezaji anaowataka, siyo wachezaji wa kuletewa, atakuwa na nafasi nzuri sana, ndani ya miaka miwili au mitatu, ya kuwa na kikosi sahihi na timu sahihi ya kuwania ubingwa wa Premier. Chelsea wamfanyie Frank kama vile Liverpool inavyomfanyia Klopp, impe muda wa kujenga kikosi, impe wachezaji anaowataka,” alisema Hoddle.
LONDON, England


