Lebo Tishio Bongo 2022

ZAMANI wakati muziki wa Bongo Fleva unakua, miongoni mwa lebo zilizokuwa zinasimamia kazi za wasanii na kutengeneza kazi bora ni pamoja na Bongo Records, MJ Records, Mawingu Studio, Sound Crafters, Empty Souls, Akili Records, G Records na nyinginezo.

 

Hizo ni miongoni mwa lebo zilizoandaa kazi bora. Hata hivyo, pamoja na utitiri huo wa lebo, bado kuna baadhi ya lebo za kibabe ambazo kila msanii alipenda kufanyia kazi na kama asipopita huko basi aliona kuna kitu kinakosekana kwenye muziki wake. Mfano Lebo ya Bongo Records.

 

Wasanii wengi wamekuwa wakiweka wazi kwamba pamoja na kufanya kazi zilizopata umaarufu katika studio mbalimbali enzi hizo, bila kufanya kazi na Prodyuza P Funk Majani wa Bongo Records, waliona kuna deni wanalo kwenye muziki.

 

Unaweza kujiuliza ni kwa nini wanamuziki walipenda kufanya kazi kwenye lebo hii? Jibu lipo wazi kwamba ni kutokana na namna lebo hii ilivyojipatia jina kutokana na kutengeneza kazi bora na kusimamia vyema wasanii mpaka wanafika kwenye mafanikio kimuziki. Mifano ni mingi; Professor Jay, Fid Q, Mangwair, Juma Nature, Matonya na wengine wengi.

 

Sasa kama ilivyokuwa zamani, hata kwa sasa mambo ni vilevile. Kuna lebo kibao katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania amabzo zinafanya poa mno.

 

Baadhi ya lebo kubwa zinazofahamika ni pamoja na Wasafi Classic Baby (WCB) chini Diamond Platnumz ambayo ina wasanii sita ambao ni Diamond Platnumz, Ryavnny, Mbosso, Zuchu, Lava Lava na Queen Darleen.

Lebo nyingine ni Kings Music chini ya King Kiba ambayo ina wasanii wanne ambao ni King Kiba, Abdu Kiba, K2GA na Tommy Flavour.

 

Nyingine ni Konde Gang Music ambayo ipo chini ya Harmonize na ina wasanii saba ambao ni Harmonize mwenyewe, Ibraah, Country Wizzy, Cheed, Killy, Anjella na Skales wa Nigeria.

Bila kusahau kuna Lebo ya Next Level Music ambayo ipo chini ya Rayvanny ikiwa na wasanii wawili tu ambao ni Rayvanny mwenyewe na Mac Voice.

 

Ni wazi kuwa biashara ya muziki nchini Tanzania imezidi kunawiri na hii ni kutokana na uwepo wa lebo hizo mbalimbali ambazo zimezidi kustawisha kiwanda cha Bongo Fleva kwa kusimamia wasanii, kuwaandalia matamasha mbalimbali, kuwatafutia kolabo za kimataifa pamoja na kusambaza kazi za wasanii kwenye mitandao ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki duniani.

 

Kutoka nchini Tanzania zifuatazo ni lebo za muziki ambazo zinatarajiwa kutazamwa zaidi zikifanya vizuri kwa mwaka 2022;

 

WASAFI CLASSIC BABY (WCB)

Kwa mwaka 2021 lebo hii ilifanya maajabu makubwa ikiwemo kutoa albam ya Mbosso ya Definition of Love na Sounds From Africa ya Rayvanny. Pia ilitoa EP za Promise ya Lava Lava na New Chui ya Rayvanny.

Mwaka 2022 bila shaka mashabiki hawana budi kujifunga mikanda kwani Diamond anatarajiwa kuachia albam yake ambayo inatarajiwa kuwa na ngoma 12 kali huku Zuchu naye akitabiriwa kuwa huwenda akaachia albam yake ya kwanza mwaka 2022.

 

KINGS MUSIC

Mwaka jana, Lebo ya Kings Music ya King Kiba iliweka rekodi baada ya kuachia albam yake ya kwanza ya Only One King na EP ya msanii K2GA ya Safari. Kwa mwaka huu wa 2022, mambo yanatarajiwa kuwa matamu zaidi kwani Tommy Flavour ametangaza kuachia albam yake ya Heir To The Throne huku King Kiba naye siku chache zilizopita alitangaza kuachia albam yake ya nne ndani ya mwaka huu.

KONDE GANG MUSIC WORLDWIDE

Kupitia lebo hii kwa mwaka 2022 wengi wanategemea kuona albam za wasanii Ibraah, Cheed na Killy zikiingia sokoni huku kwa upande wa Anjella yeye anatarajiwa kuachia EP yake ambayo ilitakiwa kuingia sokoni mwezi Desemba, lakini iliahirishwa.

 

Bila shaka kutoka kwa bosi wa lebo hiyo, Harmonize huu ni mwaka ambao tutaona video nyingi zaidi za muziki kutoka kwenye albam yake ya High School ambayo sasa inakimbiza sokoni.

 

HIGH TABLE SOUNDS

Hii ni lebo ambayo inamilikiwa na Barnaba Boy na inasifika kwa muziki mzuri hasa ule wenye mahadhi ya Bongo Fleva. Kikubwa kwa mwaka huu ni kuwa msanii mwingine wa lebo hiyo, Ziddy Value anatarajiwa kufanya vizuri zaidi kwa 2022 kama alivyofanya mwaka jana kupitia EP yake ya From The Street EP.

NEXT LEVEL MUSIC

Kwa sasa lebo hii ina wasanii wawili pekee ambao ni Rayvanny na Mac Voice ambaye ndani ya muda mfupi amepata mafanikio makubwa ikiwemo kutajwa kuwania tuzo kubwa za AEUSA zilizofanyika huko nchini Marekani. Kwa mwaka 2022, wengi wanategemea kuona wasanii wengi zaidi wanatambulishwa kwenye lebo hiyo kubwa nchini Tanzania na ikiendelea kutamba zaidi.

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO


Toa comment