MKONGWE na mmoja wa waanzilishi wa Kundi la Jahazi Modern, Leila Rashid anatarajiwa kuungana na mrithi wa Mzee Yusuf, Prince Amigo, Februari 25 ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live, MbagalaZakhem jijini Dar na kufunika katika shoo maalum ya kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza na Showbiz Xtra, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa, mbali na uwepo wa Leila na Amigo siku hiyo mashabiki wa Taarab watarajie pia kuliona Kundi la Jahazi likiwa na vichwa kibao kama vile Mishi, Fatuma pamoja na Ally Jay.
“Kwa mara ya kwanza tangu Jahazi izinduliwe rasmi pale Travertine, Magomeni mwaka 2007 wiki hii tena itatimiza miaka 10.
Siyo shoo ndogo bali ni shoo kubwa na ya kihistoria ambayo haijawahi kufanyika. “Wakati Jahazi inazinduliwa mgeni rasmi alikuwa Idd Azzan ambaye ni mbunge wa zamani wa Kinondoni. Safari hii tena katika kutimiza miaka kumi yeye atakuwa mgeni rasmi,” alisema Mbizo.
Shoo itakavyokuwa Mbizo aliongeza kuwa, mashabiki wajitokeze kwa wingi kufika ndani ya kiwanja hicho cha wajanja kwani wamewaandalia shoo ambayo hawajawahi kuifanya popote.
“Jahazi kama Jahazi wengi wanalitambua kama kundi la Taarab ambalo halina mpinzani tangu limeanzishwa hadi sasa. Niwaombe mashabiki wote wa Taarab waje kwa wingi kushuhudia mirindimo hii ya aina yake,” aliongeza Mbizo.
Wakali wote ndani Mbizo pia aligusia uwepo wa wakali wote waliopo na ambao hawapo kwenye kundi hilo kuwa siku hiyo watakuwa kitu kimoja jukwaani na kuwakumbusha mashabiki Jahazi halisi ilivyokuwa.
“Wapo wakali wengi waliopitia Jahazi ambao kwa sasa hawapo kundini kama vile Bi. Mwanahawa Ally, hivyo mashabiki watarajie kuwaona wakipanda na kuimba nyimbo zote za Jahazi walizokuwa wakitamba nazo,” alisema Mbizo.
Amigo kuvaa viatu vya Mzee Yusuf Mbizo alimaliza kwa kumuelezea msanii aliyechukua mikoba ya Mzee Yusuf, Prince Amigo kuwa siku hiyo ataonesha ukubwa dawa kwa kupiga nyimbo zake zote kali kuanzia Tiba ya Mapenzi na nyinginezo huku akitoa sapraizi ya nyimbo tatu alizokuwa akizipenda na kuziimba Mzee Yusuf.
“Ninaposema utakuwa usiku wa mapinduzi mengine mapya naamaanisha. Amigo atawapagawisha mashabiki wa nyimbo za Mzee Yusuf ambazo ni Tupendane, Anajua Kupenda pamoja na Kaning’ang’ania.
Kifupi jitokeze mwenyewe ufurahie shoo,” alimaliza Mbizo. Mbali na nyimbo hizo, mashabiki pia wataimbiwa albamu zote za Jahazi na nyimbo zilizowahi kubamba kama vile Mpenzi Chocolate, Nina Moyo Sio Jiwe hadi Tiba ya Mapenzi na kiingilio kitakuwa shilingi 8,000 tu, siku hiyo siyo ya kukosa mdau wa burudani.
Comments are closed.