NA MWANDISHI WETU| GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA | OVER THE WEEKEND
MALKIA wa Bendi ya Jahazi Modern Taarab, Leila Rashid amefunguka kuwa tofauti na mara zote ambazo bendi yake imekuwa ikifanya maonyesho huko nyuma,
katika onyesho ambalo italifanya Jumamosi ya mwisho ya mwezi huu, April 29, katika Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem imepania kuwasha moto na kuacha historia.
Akichonga na Over Ze Wikendi, Leila alisema katika onyesho hilo ataibuka na manjonjo tofauti stejini ambayo yatanogesha burudani usiku huo na amewataka wapenzi wa Muziki wa Taarab na wapenda burudani kuibuka siku hiyo bila kukosa.
“Hiyo siku kitawaka Dar Live, siwezi kuweka wazi kila kitu nitakachofanya lakini kiukweli itakuwa tofauti sana na ilivyozoeleka kuwa huko nyuma. Onyesho hili nimejipanga mno kuhakikisha wapenzi wa bendi yetu na wapenda burudani wote wanapata kitu roho inapenda,” alisema Leila.
Malkia huyo aliongeza kuwa mbali na yeye kuwasha moto, lakini pia atakuwa sambamba na wakali wengine wa Jahazi wakiwo Amigo, Mwasiti Kitolonto, Ally J, Fatuma Kassim na wengine wengi.
Naye Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa kiingilio katika onyesho hilo ambalo litaacha historia Dar Live kitakuwa ni shilingi 6,000 tu.
“Naimani kabisa mashabiki wa burudani wanafahamu nini Jahazi huwa inawapa, kwa hiyo niwatake kufika bila kukosa.
Hata hivyo, mbali na onyesho hilo la Jahazi, mwezi ujao tarehe 6, kutakuwa na onyesho babu kubwa la Christian Bella atakayesindikizwa na Pam D pamoja na Gigy Money,” alisema Mbizo.
Meneja huyo alimalizia kuwa ukiachana na Bella ambaye mara ya mwisho amepiga shoo Dar Live mwaka 2015, mwezi huohuo kutakuwa na tamasha la Nay wa Mitego linalokwenda kwa jina la Wapo. Ambapo Barnaba, Shilole, Dullah Makabila watamsindikiza huku Shamsa Ford akiwa ni ‘special apearence.’