The House of Favourite Newspapers

Leo Ndiyo Leo.. Nyoshi, Bushoke Kusepa Na Kijiji Leo Dar Live

Mfalme wa Muziki wa Dansi, Nyoshi El Saadat (kulia).

 

BAADA ya kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa Muziki wa Dansi, hatimaye leo imewadia ambapo mashabiki watakuwa wakiishuhudia rekodi ya muziki huo kutoka kwa Mfalme wa Muziki wa Dansi, Nyoshi El Saadat kwa kupiga nyimbo 15 mfululizo za bendi yake mpya ya Bogoss Musica leo (Jumamosi) ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Itakuwaje?

Akizungumza na Mikito Nusunusu, Nyoshi alisema hii imekuwa ni nafasi kwa wakali wa Wilaya ya Temeke kupata utambulisho wa bendi hiyo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.

 

“Utajulikana kama Usiku wa Mwafrika na niwaambie mashabiki tutaupeleka Kiafrikaafrika zaidi hakuna kuremba, Bogoss Musica itapiga nyimbo zake zote kali live kwa kutumia vyombo, nikiwa na madansa wa dijitali kabisa,” alisema Nyoshi.

Nyoshi aliyewahi pia kutamba na Bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ aliongeza kuwa, miongoni mwa ngoma zitakazotawala kati ya hizo 15 ni Naliamsha Dude, Aziza, Mapenzi Basi na nyingine nyingi.

 

Naye Meneja wa Dar Live, Rajabu Mteta ‘KP Mjomba’ alisema kuwa Usiku wa Mwafrika utanogeshwa na mastaa wengine kibao akiwemo mkongwe wa Muziki wa Bongo Fleva, Maxi Bushoke ambapo atawakumbusha mashabiki nyimbo zake zote kali zilizowahi kubamba zikiwemo Barua, Usiende Mbali na nyinginezo.

 

“Burudani zote hizo utazipata kwa kiingilio kidogo tu cha shilingi 5,000 tu getini.”

Mara baada ya kumalizika kwa shoo hiyo, Jumamosi itakayofuata (Oktoba 13, mkesha wa Nyerere Day), Dar Live itafanya fainali ya sita bora ya wanaoimba kwa kufuata biti kupitia skrini kubwa (Karaoke).

 

“Usiku huo lazima mshindi wa Karaoke apatikane, hivyo niwaombe wale wote tulioanza pamoja tangu shindano hili linaanza msikose kuja kumuona mshindi,” alisema KP Mjomba.

 

Shoo hiyo itasindikizwa na mkali wa Muziki wa Rhumba, Benson ambaye pia anabamba na Ngoma ya Hauzimi pamoja na mkali wa Singeli, Vairasi ‘Mdudu’ kwa kiingilio cha 3,000 na kinywaji bure mkononi.

Comments are closed.