The House of Favourite Newspapers

Leo ni mapinduzi zanzibar; mgogoro utatuliwe

0

640719364Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Shariff

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuiona siku ya leo.Baada ya kusema hayo nikumbushe tu kwamba leo ni siku ya kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Lakini tofauti na miaka mingine mwaka huu siku hiyo inaadhimishwa kukiwa na mgogoro mzito wa kisiasa kati ya vyama vikuu vya kisiasa Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF) mara tu baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka jana.

Mgogoro huo uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa kwa uchaguzi huo Novembar 28 mwaka jana kwa madai kuwa kuna taratibu na sheria zilivurugwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, Mgombea Urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi akasema kwamba alikuwa ameshinda na ndiyo maana uchaguzi huo umefutwa. Kilichofuata ni mgogoro unaotishia amani visiwani humo.

Nichukue nafasi hii kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kushughulikia mgogoro huo wa uchaguzi Zanzibar kwa haraka ili usiweze kuleta mpasuko utakaosababisha machafuko ya kisiasa nchini humo.
Hali ya kisiasa Zanzibar kwa sasa si nzuri hivyo ni vyema Rais Magufuli angelipa uzito wa kipekee na kulishughulikia suala hilo kwa kasi ya haraka.

Wito wangu huu unaungwa mkono na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa ambao wameshauzungumzia mzozo wa kisiasa huo unaoendelea visiwani Zanzibar baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar-ZEC kufuta uchaguzi mkuu visiwani humo.

Najua kuna taarifa kadhaa juu ya juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa kisiasa Zanzibar ikiwemo mazungumzo baina ya viongozi wa juu na wakuu wa vyombo vya usalama, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kisiasa nchini walikuwa na maoni tofauti juu ya suluhisho la mzozo huo kwa sasa ambapo Chama Cha Wananchi CUF kupitia mgombea wake visiwani humo Maalim Seif Shariff Hamad, kikidai kuwepo mizengwe ya makusudi kuwanyima ushindi.

Niliwahi kumsikia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Benson Bana, katika mahojiano maalum na chombo kimoja cha habari akitaka kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa kama ilivyokuwa wakati wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo uliomaliza mgogoro wa kisiasa wa muda mrefu.

Kwa upande wangu naamini kwamba viongozi wa ndani ya Tanzania wana uwezo wa kusuluhisha mgogoro huo wa kisiasa na kuumaliza bila kuleta madhara yoyote.
Niiombe Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na vyama vya CUF na CCM kutafuta muafaka kwa njia ya mazungumzo kuhusiana na suala la kufutwa kwa uchaguzi huo kama njia ambayo itaepusha Zanzibar kutumbukia katika machafuko.

Yapo maswali mengi watu wanajiuliza, kama vile Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha alipotangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar kwa madai ya kuwepo kasoro nyingi katika zoezi hilo, kwa nini hakusema tarehe ya kurudia uchaguzi?
Hakika niseme wazi kwamba mgogoro huu wa Zanzibar unatia doa taifa letu na wanaoushabikia bila shaka wana maslahi nao, lakini tuwaambie bila aibu kuwa waweke maslahi ya taifa mbele na waachane na ubinafsi kwani unaweza kutuletea matatizo mazito ambayo yanaweza kuzuilika.

Nimeambiwa CUF leo wanasusia sherehe za Mapinduzi na kuna watu wanafurahia hilo, wakumbuke umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, huu ni mpasuka mpya, tusiruhusu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply