Licha Kim Kukanusha! Korea Kaskazini Yadaiwa Ina Wagonjwa wa Corona
LICHA ya viongozi wa Korea Kaskazini kukanusha kila mara kuwepo kwa wagonjwa wa homa kali ya mapafu, Corvid-19, inayosababishwa na virusi vya corona nchini humo, madai hayo yanaonekana kuwa si kweli baada ya mtu mmoja kutoka nchini humo aliyekuwa anajaribu kutoroka kwa kuvuka mpaka na kuingia nchini, kupimwa na kuonekana ana maambukizi ya virusi vya Corona.
Mtu huyo alipigwa risasi Aprili 20, mwaka huu na walinzi wa China wakati akijaribu kuvuka Mto Tumen na alipopelekwa hospitali aligundulika kuwa na maambukizi hayo na sasa yuko chini ya karantini.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily NK, tukio hilo linatoa ushahidi kamili kwamba maambukizi ya ugonjwa huo yameingia Korea ya Kaskazini licha ya viongozi wake kukataa jambo hilo.
Gazeti hilo la Daily NK ambalo lina ‘mashushushu’ nchini Korea ya Kaskazini, liliwahi kuripoti matukio kadhaa ya ugonjwa huo ambapo mwezi uliopita lilisema askari 180 walifariki kutokana na maambukizi ya virusi hivyo nchini humo.
Pia liliripoti kwamba watu wengine 23 huenda walikufa kutokana na maambukizi hayo, jambo ambalo taasisi za afya na serikali zimekuwa hazilizungumzii kabisa.
Wiki iliyopita Radio Free Asia iliripoti kwamba wahadhiri nchini humo wamekuwa wakiwaambia kwa siri raia nchini humo kwamba maambukizi ya ugonjwa huo yapo.
Waliwaambia kwamba mwishoni mwa mwezi Machi, virusi hivyo vilikuwa vinasambaa katika nchi mkuu wa nchi hiyo, Pyongyang, jimbo la Hwanghae Kusini na Hamgyong Kaskazini.
Hata hivyo, wahadhiri hao walisema nchi hiyo ina wagonjwa wachache kuliko nchi nyingine duniani kutokana na mfumo wake thabiti wa afya.


