Breaking: CCM Yampitisha Magufuli kwa Asilimia 100 – Video
#BREAKING: Mkutano Mkuu wa CCM Taifa leo Julai 11, 2020 umempitisha Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Dkt. John Magufuli kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania kupitia CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020 kwa kupata kura za ndiyo 1,822 (sawa na asilimia 100).
“Wajumbe wa Mkutano Mkuu mmenipa heshima kubwa na mimi nimebaki na deni kubwa, namuomba Mungu kura nilizozipata leo zisinipe kiburi, zisifanye nijione muhimu sana, bali zinipe nguvu nitumikie Watanzania wote bila kujali Vyama vyao, Dini au Makabila.
“Ndugu zangu mmenipa kura 100% lakini msitoke hapa mkiamini tutashinda Uchaguzi kwa 100%, tusifurahi kabla hatujafika mwisho, tukafanye kazi ya kutafuta kura za Rais, Wabunge na Madiwani, sisi sote tuna wajibu wa kukisaidia Chama chetu kushinda.
“Hussein Mwinyi ni mnyenyekevu sana, hajaubeba Urais wa Baba yake, na ndio maana wakati anashukuru hapa hajaanza kumshukuru Baba yake, kamshukuru Mkapa, akamshukuru Kikwete kisha kanishukuru mimi akafuata Baba yake, Mwinyi ana hekima.
“Nawaambia hii siri, Hussein Mwinyi nilimteua kuwa Mgombea Mwenza pamoja na Mama Samia, lakini kwakuwa Mama Samia ni Mwanamke akashinda kuwa Makamu wa Rais, maana huwezi kushindana na Wanawake ukashinda, Wanawake wanatuzidi kwa mambo mengi, Wanawake oyee.
“Asingekuwa Mzee Jakaya Kikwete pengine nisingekuwa Rais, alinipitisha kugombea wakati akiwa mwenyekiti wa Chama (CCM), aliwatema mpaka marafiki zake akaniteua mimi, huo ndo ukweli, saa nyingine kwenye hizi kazi za uongozi hakuna cha urafiki.
“Nilipomchagua mama Samia kuwa mgombea mwenza mwaka 2015 sikujua vizuri uchapa kazi wake wakati ule lakini mama huyu ni mchapa kazi, ana heshima, nikimtuma anenda, sura yake nzuri, Wasukuma tunapenda weupe, nimemteua tena Mhe. Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza wangu,” -Rais Magufuli