The House of Favourite Newspapers

CHADEMA WAMPONGEZA JPM, WATAKA TUME IUNDWE KESI ZA MAUAJI – VIDEO

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimempongeza Rais Dkt John Magufuli kwa kumuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswallo Mganga kuchunguza kesi ya mauaji kwa madai kuwa watuhumiwa walibambikiziwa kesi huku kikiiomba serikali kupitia DPP huyo kuunda tume maalum itakayochunguza kesi mbalimbali za makosa ya jinai nchini.

 

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho leo Jumatano, Machi 20, 2019, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu amesema watuhumiwa wengi waliopo mahabusu kesi zao huchukua muda mrefu kupepelezwa na wengine hubabimbikiziwa kesi jambo ambalo halikubaliki.

 

Mwalimu amesema hayo baada ya DPP Biswalo, kuawafutia shitaka la mauaji watuhumiwa Musa Sadiki na Edward Matiku kufuatia agizo la Rais Magufuli la kuchunguzwa kwa kesi hiyo baada ya kusoma katika gazeti moja ambapo Musa Sadiki aliandika barua ikionesha alivyobambikiwa kesi ya mauaji na jeshila polisi huku wakichukua fedha taslim Tsh. 788,000 na simu ya mkononi.

 

“Kama chama tumeelekeza mamlaka zinazohusika na kukamata, kuhukumu na kupeleleza kuunda tume maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kwa watuhumiwa, mahabusu na wafungwa wote kule magereza ili kujiridhisha hali ilivyo.

 

“Kule Tabora imeripotiwa kijana alibambikiziwa kesi ya mauaji, DPP na Jeshi la Polisi limekiri, tafsiri yake ni kwamba, kijana yule asingekuwa jasiri kuandika barua ile angeozea ndani hadi leo, na wangapi wapo ndani kwa kibambikiziwa kesi hizo.” amesema Mwalimu.

 

Aidha, DPP aliagiza polisi kuwachunguza waliohusika katika kupanga kesi hiyo namba 8/2018 mkoani Tabora ili wachukuliwe hatua huku akiweka sharti la kutaka kesi zote za jinai zipitie ofisi yake kabla ya kwenda mahakamani.

 

Mwalimu amesema vyombo vya usalama nchini vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha utu wa mtu haupotei na kama watamtia hatiani mwananchi basi upelelezi ufanyike kwa haraka badala ya kuendelea kusota rumande.

VIDEO: TAZAMA CHADEMA WAKIZUNGUMZA

Comments are closed.