JPM Azikumbuka Bakora 24 Nyerere – Video

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli amehudhuria maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana Kitaifa katika Uwanja wa Ilulu Mkoani Lindi.

Akihutubia wananchi Rais Magufuli, amesema moja ya vitu ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa akivikemea ni suala rushwa na kueleza alihakikisha watuhumiwa wa rushwa, walikuwa wakichalazwa bakora 12 wakati wa kuingia jela, na kupigwa bakora 12 wakati wa kutoka jela.

“Miaka 20 iliyopita Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere alikuwa hai, lakini sasa hayupo, miaka 20 ijayo sidhani kama kuna watu tutakuwa hai, tufanye mambo ambayo kila mmoja wetu atakumbukwa kama tunavyomkumbuka Baba wa Taifa leo.
“Serikali ya awamu ya tano imemuenzi Mwl. Julius Nyerere kwa kuanzisha Balozi mbalimbali ikiwemo, Korea na Cuba, kuhamishia Makao Makuu Dodoma, na mimi nimetangaza juzi kuhamia rasmi huko rasmi.
“Tunamuenzi Mwl. Nyerere kwa kujenga uchumi wa viwanda ili kupunguza umaskini na kuongeza ajira kwa vijana, hadi sasa tumeshajenga viwanda 4000 nchi nzima na kufufua viwanda vilivyokuwa vimekufa.
“Nchi hii ilikuwa inajipanga vizuri kwenye ukuaji wa viwanda chini ya Jemedari Mwl. Julius Nyerere. Yeyote ambaye alijihusisha na vitendo vya rushwa alipigwa bakora kabla na baada ya kutoka jela, kupitia hotuba zake nadhani mnajua hili.
“Niwapongeze vijana sita walioongoza mbio za Mwenge. Katika risala yao wamenieleza kuwa walipokea vitisho kutoka kwa mikoa iliyofanya vibaya.
“Ipo miradi yenye viashiria vya uhujumu uchumi na rushwa. Naikabidhi ripoti hii kwa TAKUKURU, ukaikague, uiangalie wale wanaotakiwa kupelekwa mahakamani wapelekwe, wale wakubwa unaoona huwawezi niletee ripoti zao nitafanya maamuzi, nataka Tanzania inyooke.
“Namshukuru Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa kushughulikia matibabu na mazishi ya muasisi wa Taifa letu, Mwl. Julius Nyerere na kuweka siku hii maalumu ya kumuenzi Baba wa Taifa.
“Pia Rais Mstaafu Jakaya Kikwete aliyeendeleza maadhimisho haya, bila hawa pengine leo tusingekuwa kwenye maadhimisho haya,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, akifunga hafla hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema mbio za Mwenge kwa mwaka 2020 zitazinduliwa katika Mkoa wa Kusini Unguja na kuhitimishwa Makao Makuu ya Nchi mkoa wa Dodoma.

 


Loading...

Toa comment