The House of Favourite Newspapers

LIVE: Mahakama Kuu Kenya Yafuta Matokeo ya Urais, Yaamuru Urudiwe

0

UCHAGUZI KENYA: Mahakama Kuu imefuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa nchi hiyo yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta. Imeamuru uchaguzi urudiwe ndani ya siku 60.

ILIVYOKUWA

IDARA ya Mahakama imesema majaji wa Mahakama Kuu nchini Kenya wameanza kutoa uamuzi kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyowasilishwa na Umoja wa Vyama vya Upinzani (NASA) saa 5:00, leo ambapo ndiyo siku ya mwisho kikatiba kwa mahakama hiyo kutoa uamuzi.


Matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi

Kulikuwa na wagombea wanane katika uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 8 Agosti mwaka huu. Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa Ijumaa tarehe 12 Agosti na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati.

Matokeo yalikuwa kama ifuatavyo:

Ekuru Aukot 27,311 (0.18%)
Abduba Dida 38,093 (0.25%)
Cyrus Jirongo 11,705 (0.08%)
Japheth Kaluyu 16,482 (0.11%)
Uhuru Kenyatta 8,203,290 (54.27%)
Michael Wainaina 13,257 (0.09%)
Joseph Nyagah 42,259 (0.28%)
Raila Odinga 6,762,224 (44.74%)

Waliokuwa wamejiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo ni 19,611,423 lakini waliopiga kura walikuwa 15,073,662 ambao ni sawa na asilimia 78.91.

Mahakama Kuu ya Kenya ina majaji saba ambao walianza kusikiliza kesi hiyo ya matokeo ya uchaguzi wa urais.

Mahaka Kuu ya Kenya.

Majaji hao ni:

  1. Jaji Mkuu David Maraga
  2. Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu
  3. Jaji Prof Jackton Boma Ojwang
  4. Jaji Mohammed K. Ibrahim
  5. Jaji Njoki S. Ndungu
  6. Jaji Dkt Smokin C. Wanjala
  7. Jaji Isaac Lenaola

Jaji Mohammed Ibrahim aliugua siku ya mwisho ya kusikizwa kwa kesi hiyo Jumanne wiki hii.

Kukaguliwa kwa mitambo ya tume ya uchaguzi

Wakati wa kusikizwa kwa kesi, kulikuwa na mvutano kuhusu kukaguliwa kwa mitambo ya tume ya uchaguzi. Upinzani ulikuwa umedai mitambo hiyo ilidukuliwa na kuingiliwa ili kumfaa Bw Kenyatta.

Tume hiyo baadaye jioni siku ya Jumanne iliwapa wataalamu wa upinzani Nasa fursa ya kukagua mitambo hiyo ingawa bado kulikuwa na kutoelewana kuhusu kiwango ambacho mitambo hiyo ilifunguliwa.

Ulinzi waimarishwa mahakama ya juu Nairobi

Ulinzi umeimarisha ndani na nje ya majengo ya Mahakama ya Juu jijini Nairobi ambapo majaji wanatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na IEBC.

Mpiga picha wetu Rod Mcleod ametutumia picha hizi za maafisa wakishika doria nje ya majengo hayo.

Mawakili wa Odinga wawasili mahakamani

Mawakili wa mgombea urais wa upinzani, waziri mkuu wa zamani Raila Odinga wamewasili katika majengo ya mahakama wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo.

  • Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo akiwa na kura 8,203,290 (54.27%)
  • Tume ya uchaguzi ilisema Raila Odinga alipata kura 6,762,224 (44.74%).

Odinga awasili mahakamani

Mgombea urais wa upinzani Raila Odinga, ambaye aliwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Kenyatta amewasili mahakamani.

“Uamuzi unaweza kwenda upande wowote,” ameambia wanahabari.

Viongozi wengine wa muungano huo Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula pia wamewasili mahakamani.

Maraga: Kulitokea makosa yaliyoathiri uchaguzi wa urais

Jaji Maraga akisoma uamuzi wa wengi, amesema “mshtakiwa (Tume ya Uchaguzi), alikosa au akakataa kuandaa uchaguzi kwa njia ambayo inatakiwa kwenye katiba na sheria za uchaguzi.”

Amesema IEBC ilifanya makosa katika kupeperusha na kutangaza matokeo. Jaji amesema makosa hayo yaliathiri matokeo. Majaji waliotoa msimamo tofauti ni Jaji Ojwang na Jaji Ndung’u.

Jaji Ndung’u: Uchaguzi ulikuwa wa kuaminika

Jaji Njoki Ndung’u, akisoma uamuzi wake wachache amesema uchaguzi huo ulikuwa wa kuaminika na ulisifiwa sana hata na waangalizi.

“Makosa yanaweza kutokea. Yaliyotokea hayakuwa makusudi. Natofautiana na uamuzi wa wengi, na nitatoa hukumu yangu kamili katika kipindi cha siku 21,” amesema.

Jaji Ojwang’: Hakuna ushahidi wa kutosha kuufuta uchaguzi

Jaji Ojwang, ambaye alitofautiana na wachache amesema hakujakuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba uchaguzi unafaa kufutiliwa mbali.

Amesema makosa ya lawama yamekuwa ya jumla. Jaji huyo amesema pia kwamba waangalizi waliafikiana kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa haki.

Jaji Maraga: Ushahidi haukufanyika kwa kufuata katiba

“Uchaguzi si tukio, ni mchakato, kuanzia mwanzo hadi mwisho.”

Ninaamini tutaonyesha ni kwa nini tulifikia uamuzi wetu, kwa kuangalia uchaguzi wote kwa jumla, kwamba uchaguzi haukuandaliwa kwa mujibu wa katiba.

Maraga: Uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku 60

Jaji Mkuu David Maraga ameagiza: Uuchaguzi wa urais uliofanyika 8 Agosti, 2017, haukuandaliwa kwa mujibu wa katiba na sheria, hivyo matokeo yake ni batili.

“Natangaza hapa kwamba Bw Kenyatta hakuchaguliwa na kutangazwa kwa njia inayofaa.

“Agizo linatolewa, kuagiza Tume ya Uchaguzi kuandaa na kufanyisha uchaguzi mwingine kwa kufuata katiba na sheria katika kipindi cha siku 60.”

Odinga: Ni siku ya kihistoria Kenya na kwa Afrika

Mgombea urais wa upinzani Raila Odinga amesema leo ni siku ya kihistoria kwa Kenya na kwa Afrika. Kwa mara ya kwanza, Mahakama imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais. Imetoa mfano mwema.

“Tulisema tangu awali kwamba safari yetu ya Canaan haiwezi kuzuiwa. Siku ya tarehe 8 Agosti tulivuka mto Jordan.”

Bw Odinga amesema upinzani hauna imani kwamba tume ya sasa ilivyo inaweza kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Breaking News: Bavicha Wahoji… Kwa ni Chadema Pekee Ndio Wanaokamatwa?

Leave A Reply