The House of Favourite Newspapers

Live na Kafulila: JPM na Mawaziri Watano Walitaka Nikomalie Escrow

0
Rais Dk. John Magufuli

 

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ni kijana aliyejitoa mhanga kukomaa kuhusiana na sakata la ufisadi wa Tegeta Escrow akiwa bungeni na hata nje ya bunge. Leo anajibu maswali mbalimbali ambapo anasema Rais Dk. John Magufuli alikuwa akipinga mambo hayo ya kifisadi tangu akiwa bungeni; fuatana nami katika makala haya ili ujue mengi kwa kina:

Swali: Wewe umekuwa kinara wa kupambana na ufisadi uliofanywa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, una neno gani baada ya watuhumiwa wawili kukamatwa na kufikishwa mahakamani?
Jibu: Ninachoweza kusema ni hatimaye imekuwa! Vinara katika ufisadi wa IPTL/ESCROW Singasinga Seth na James Rugemarila wametiwa nguvuni. Huu ni uamuzi mkubwa uliosubiriwa sana. Na siku zote sikujua kwa nini rais alikuwa anahofu kuagiza hatua hii.

Swali: Kwa nini unasema hukujua kwa nini rais alikuwa na hofu kuagiza hatua hiyo?
Jibu: Sikujua kwa nini kwa sababu wakati wa mnyukano wa hoja hii, rais alikuwa bungeni (kama mbunge wa Chato) na alikuwa sehemu ya maazimio ya Bunge kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe na wahusika watiwe nguvuni.

 

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (kushoto) akifanya mahojiano na Global TV Online, kushoto ni Mhariri wa Uwazi, Elvan Stambuli.

Swali: Je Rais Magufuli wakati huo akiwa bungeni, alikuunga mkono dhidi ya vita hiyo?
Jibu: Nakumbuka nikiwa kwenye kipindi kigumu hata kutishwa kuondolewa kichwa na kuitwa majina ya wanyama ( aliitwa jina hilo na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema) , yeye rais alikuwa miongoni mwa mawaziri 5, walionidokeza kwamba ESCROW ni dili nikomae tu mpaka kieleweke!

 

Swali: Sasa Serikali ya Rais Magufuli imewafungulia kesi watuhumiwa wa Escrow ambayo ilikuwa ikikutesa, unamwambiaje rais?
Jibu: Nampongeza Mheshimiwa  Rais Magufuli  kwa uamuzi huu muhimu uliosubiriwa siku nyingi kuamua hatima ya ufisadi huu uliomshinda vibaya mtangulizi wake.

 

Swali: Kuna habari kwamba baada ya kukomalia ‘ishu’ hii ulitiwa msukosuko na huyo Singasinga, je ni kweli?
Jibu: Ni kweli; Singasinga alinifungulia kesi kunidai Shilingi 300 bilioni Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2014, Agosti 2015 nikamshinda lakini akaamua kunifungulia upya Mahakama ya Kisutu akidai Shilingi 100 milioni, zote akidai nimsafishe kuwa yeye na wenzake hawakuchota zaidi ya Shilingi 300 bilioni kifisadi.

 

Swali: Nikikupa nafasi useme chochote kuhusiana na kesi hii kifupi kwa ushauri, unashauri nini?
Jibu: Kifupi naomba PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa)  na DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka) , wasituangushe Watanzania. Nilipata kuwaza kumwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali anipe kibali niendeshe kesi na hawa majabali wa Escrow kwani nina ushahidi wakutosha.

 

Swali: Lakini, je una maoni gani kuhusu kuburuzwa kwao mahakamani?
Jibu:  Sasa nina furaha kwamba PCCB wameamua kuwaburuza kortini ili sheria ikachukue mkondo wake.

 

Swali: Nini ushauri wako kwa serikali sasa?
Jibu: Nashauri mali zote za wahusika hawa ziwekwe chini ya ulinzi, kwani ni muhimu zikakamatwa kusubiri hukumu ya kesi hii ya Tanzania pia kesi iliyopo Mahakama ya kimataifa ya International Centre For Settlement of Investment Disputes (ICSID) ambako Septemba 2016, iliamuliwa tulipe Bank ya SCB-HK kiasi zaidi ya 400 bilioni kwa kuwa ndiyo wamiliki halali wa IPTL na wenye share certificate za IPTL.

 

Mwaka huu Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) wamekata rufaa kuomba wapunguziwe hukumu ifanane na uamuzi wa ICSID wa Februari 2014.

 


Swali: Kwa nini unashauri hivyo?
Jibu: Kwa kuwa Singasinga Seth alisaini hati na Benki Kuu ya Tanzania, kwamba deni lolote litakalotokana na migogoro ya IPTL atawajibika yeye na wenzake wanaomiliki Kampuni ya PAP, ndiyo maana nasisitiza mali za watu hawa zishikiliwe.

 

Swali: Nini ushauri wako kuhusu mitambo ya IPTL?
Jibu: Nashauri mtambo wa IPTL uwekwe chini ya Tanesco kama ilivyoazimiwa na Bunge Novemba 2014, tuachane kabisa na kulipa matapeli shilingi saba bilioni kila mwezi ambazo ni malipo ya capacity charges walizokuwa wanalipwa na serikali hii bila kujali IPTL imezalisha au haijazalisha umeme.

 

Swali: Baada ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani unawaambia nini Watanzania?
Jibu: Watanzania watambue kwamba huyu Singasinga anayetambulishwa kama mmiliki wa PAP iliyochota Shilingi  300 bilioni za Tegeta Escrow kama mmiliki mpya wa IPTL, mpaka fedha hizo zinachukuliwa alikuwa anamiliki asilimia 50% tu ya kampuni lakini asilimia 50 zilikuwa zikimilikiwa na kampuni ijulikanayo kama Simba Trust, inayomilikiwa na watu wasiotajwa ni akina nani. Hawajawahi kutajwa popote kwenye ripoti zote.

 

Nilijaribu kutaka majina yao kwenye Kamati ya Viwanda wakati tukiwahoji Brela ((Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) na hata baadaye bungeni, serikali iliendelea kusisitiza kuwa majina hayo ni SIRI. Hawa wahusika naomba wajulikane.

 

Hongera Rais (Magufuli) kwa hatua hii, nazidi kuomba Mungu kesi hizi zifike mwisho kwani kwangu haya ni muhimu katika kumbukumbu zangu kuliko Aprili 28, 2015, siku niliyopewa tuzo kwa mapambano dhidi ya ufisadi kwa rejea ya sakata la Escrow, kwani tuzo haina maana kama vita haifiki mwisho.

 

Nishauri katika hili, asiwepo yeyote wa kulindwa kwa kinga yoyote kwani katiba na sheria vipo kwa ajili ya Watanzania na siyo Watanzania kwa jili ya katiba na sheria. Tusipofika huko vita ya ufisadi mkubwa itakuwa ngumu sana kufika mwisho.

Mwandishi: Nakushukuru sana.
Jibu: Asante.

Na Elvan Stambuli | UWAZI

======

Kafulila: Naunga Mkono Juu Ya Hatua Zinazochukuliwa na Rais Sakata La Escrow

Leave A Reply