Rais Samia Ashiriki Mkutano Wa Pamoja Na Wakuu Wa Nchi Na Serikali Wa EAC NA SADC -(Picha + Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameutaka Umoja wa Afrika kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhakikisha kuwa mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unapatiwa suluhisho la kudumu.
Akizungumza katika Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC unaofanyika jijini Dar es Salaam kujadili hali ya usalama mashariki mwa DRC, Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania inaheshimu dhamira ya kulinda amani na usalama, si tu ndani ya kanda bali barani Afrika kwa ujumla.
Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kwamba mgogoro wa DRC, taifa ambalo ni mwanachama wa EAC na SADC, umeendelea kwa muda mrefu na athari zake zimevuka mipaka na kuathiri mataifa jirani kwa namna mbalimbali, ikiwemo ongezeko la wakimbizi, kuporomoka kwa shughuli za kiuchumi, na kutishia usalama wa raia wasiokuwa na hatia.
“Kwa wiki chache zilizopita, tumeshuhudia wimbi la ghasia ambalo limeleta madhara makubwa kwa maisha ya watu, kuwasababisha kuhama makazi yao, na kuathiri shughuli za kiuchumi pamoja na biashara za mpakani,” amesema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa historia haitawasamehe viongozi wa kanda iwapo wataendelea kushuhudia hali hii bila kuchukua hatua madhubuti za kurejesha amani.
“Kama viongozi wa kanda, historia itatuhukumu vikali tukibaki kimya huku hali ikiendelea kuzorota kila siku,” amesema.
Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa mgogoro wa DRC unapata suluhisho la kudumu. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kusimamia utatuzi wa changamoto zao kwa misingi ya “suluhisho za Kiafrika kwa matatizo ya Afrika.”
“Kwa mujibu wa dhana ya kutatua changamoto za Afrika kwa njia za Kiafrika, nchi zetu zina jukumu la pamoja kuhakikisha tunashughulikia changamoto za kiusalama zinazoathiri raia wasio na hatia,” ameongeza.
Rais Samia pia ameitaka EAC, SADC, Umoja wa Mataifa (UN), na wadau wengine wa kimataifa kuongeza juhudi katika kusaka suluhisho la kudumu kwa mgogoro huu.