
RAIS John Magufuli leo Februari 27, amemwapisha Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu jijini Dar.
Akizungumza baada ya uapisho huo, Bashiru ambaye anajaza nafasi ya Balozi Mhandisi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021, amesema:

“Mheshimiwa rais leo siwezi kusema mengi, sababu ya mazingira ya uteuzi huu. Ulinipa kazi ambayo ingechukua mwezi mzima wa tatu na tukaagana, jana nikiwa nasoma mafaili yangu nikaona habari mtandaoni kwamba umeniteua, kwa mshituko huo siwezi kusema mengi, bado ninatafakari.
“Mila, maadili na miiko ya kazi hii, Ubalozi na Ukatibu Mkuu Kiongozi, hii si kazi ya kuzungumza sana, ni kazi ya kusikiliza, kuchambua na kutenda. Waliotegemea nitazungumza sitazungumza sana, ninakuahidi Mheshimiwa Rais sitakuangusha.

“Tangu ulipoteuliwa na kuapishwa, ulianza ziara, nimekuwa nikisikiliza maelekezo yako na hayohayo niliyokuwa nayapeleka kwa katibu Mkuu Kiongozi ndiyo naenda kuyasimamia leo. Nitasimamia uzalendo na kusimamia haki na wajibu wa kila mmoja wetu ili tupige hatua.
“Ninamuombea dua Balozi Kijazi, rafiki na kaka yangu ambaye tumefanya kazi pamoja, ningetamani awepo wakati wa uapisho huu. Amekuwa mchapakazi na muungwana, siwezi kusema nitakuwa kama Balozi Kijazi lakini Mwenyezi Mungu anibariki nifanye aliyokuwa akiyatekeleza.”

