MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. John Magufuli na mgombea mwenza, Samia Hassan, leo Jumanne, Agosti 25, 2020, wamerejesha fomu zao katika ofisi za makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zilizopo Njedengwa, Dodoma, na kuthibitishwa kuwa wamekidhi vigezo vyote kugombea nafasi hiyo na sasa ni wagombea halali.
Akikabidhi fomu hizo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mst. Rufaa Semistocles Kaijage, Magufuli amesema kuwa amepata wadhamini katika mikoa 10 kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi lakini pia amepata wadhamini katika mikoa mingine mitano hivyo amepata wadhamini wa kutosha katika jumla ya mikoa 15.
Akizungumza baada ya mapokezi ya fomu hizo, Mkurugenzi wa NEC, Dkt. Wilson Mahera, amesema Magufuli na Samia wametimiza vigezo vyote vya uteuzi na kuwania nafasi hiyo.
“Fomu za uteuzi zimejazwa kwa ukamilifu na kwa idadi inayotakiwa na ziada, wagombea wametoa tamko la kuwa wanazo sifa za kugombea, katibu mkuu wa chama ametoa tamko la uthibitisho wa kuwateua wagombea, wagombea wamedhaminiwa na wapiga kura katika mikoa 10 iliyokuwa inatakiwa na mingine mitano ya ziada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Wasimamizi wa uchaguzi wamethibitisha majina ya wagombea, wagombea wametoa tamko mbele ya jaji kuwa wanazo sifa za kugombea, wamewasilisha stakabadhi ya dhamana ya Tsh milioni 1, wamewasilisha nakala picha nne za passport size, wametoa tamko la kutekeleza na kuheshimu maadili ya uchaguzi,” amesema Mahera.
“Baada ya kujiridhisha kwa mujibu wa sheria ya taifa ya uchaguzi na kwa mamlaka niliyopewa na Katiba ya nchi na kanuni za uchaguzi wa mwaka huu, tume ninatamka kuwa tume imewateua Dk. John Pombe Magufuli na Samia Suluhu Hassan kuwa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Kaijage.