The House of Favourite Newspapers

Kimenuka! CHADEMA, CCM Wachapana Ngumi Dar

JANA Jumatano, Oktoba 3, 2018 kulitokea tukio la aina yake kwenye Ukumbi wa Anatoglo uliopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ambako kulikuwa na uchaguzi wa Naibu Meya baada ya ukumbi huo kugeuka kuwa uwanja wa mapambano na ngumi kupigwa.

 

Tukio la makonde hayo lilimhusisha Diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Assenga aliyechapana makonde na baadhi ya madiwani wa CCM baada kuwepo kwa sintofahamu wakati wa kutangazwa matokeo hayo ya uchaguzi huo ambapo Omar Kumbilamoto (CCM) alitangazwa kuwa msindi kwa kura 27 dhidi ya kura 25 za Adam Rajabu (CUF) huku Mgombea huyo, Assenga (CHADEMA) akikosa kura hata moja.

 

Uchaguzi huo ulifanyika kufutia Kumbilamoto aliyekuwa Naibu Meya wa Ilala (CUF) kujiuzulu na kuhamia CCM, akieleza ameshindwa kuwatumikia wananchi kutokana na chama chake kuwa na mgogoro wa uongozi.

 

Assenga alisema chanzo cha vurugu hizo ni baadhi ya kura kuharibika lakini Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Jumanne Shauri alipinga na kusema hakuna kura iliyoharibika.

 

“Mzozo ulianzia katika chumba cha majumuisho ya kura, nikiwa kama mwangalizi wa kura niliona baadhi ya kura zimeharibika na hazifai kwa mujibu wa uchaguzi, lakini Shauri na watu wengine walikataa. Nilizishikilia zile kura nne zilizoharibika baada kuona hivyo Shauri alitoka nje ya chumba na kuwaita polisi ambao walikuja kuninyang’anya kura hizo na kunitoa nje ya chumba.” alisema Assenga.

 

Amedai baada ya kutolewa katika chumba hicho alikwenda kuzungumza na madiwani wenzake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ndipo wajumbe wa CCM walipomfuata na kuanza kurushiana maneno, kisha kuanza kuchapana makonde.

 

Aidha, Mkurugenzi Shauri amesema uchaguzi huo ulikuwa wa haki na ulifuata taratibu zote na wajumbe walikuwa 52. CCM 26 na Ukawa kwa maana ya CUF na Chadema 26. Baada ya mchakato wa kuhesabu kura kukamilika, Kumbilamoto alipata kura 27 wakati Rajab Penza wa CUF akipata 25.

 

Hata hivyo, Shauri amekiri vurugu kutokea akidai zilisababishwa na Assenga lakini polisi walifanikiwa kumdhibiti.

BREAKING: Moto mkubwa wateketeza Jengo la Benjamin Mkapa Leo!

Comments are closed.