Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa mwaka mmoja kwa viongozi wa mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa, Singida na Shinyanga ihakikishe iwe imekamilisha kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Juni 15, 2019) wakati akifungua Kongamano la Nne la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Kongamano hilo limeandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(NEEC) na kauli mbiu yake ni Wezesha Watanzania Kujenga Viwanda.
Amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama kilichopo Kahama ili kuharakisha nia ya Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi.
Waziri Mkuu amesema mikoa yote iliyokamilisha kuandaa mwongozo wa uwekezaji, nayo ifikapo mwakani inapaswa kuonesha hatua za utekelezaji katika kutumia fursa mbalimbali zilizoainishwa pamoja na mikakati ya kutangaza fursa hizo zilizopo katika maeneo yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema matokeo ya tafiti ziliyofanywa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuhusu biashara na uwekezaji nchini yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uandaaji wa maandiko ya miradi mikubwa inayopendekezwa na shirika hilo.
“Miradi hiyo ni pamoja na ule wa “Harmonized Innovation Solutions for Local Economic Development” ambao upo katika hatua za maandalizi.
Lengo la UNDP ni kuhakikisha kuwa miradi inayohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi inatekelezwa moja kwa moja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.”
Amesema NEEC ina uwezo mkubwa katika kusimamia miradi mbalimbali ya uwezeshaji ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Serikali pamoja na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo UNDP, ILO, UNCTAD, AfDB na UN-Women, hivyo ameyahakikishia mashirika hayo kuwa Serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yote ili kupata matokeo yaliyo tarajiwa.
Pia, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liendeleekuratibu masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2015 – 2020 kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.
“Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iboreshwe sambamba na kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia Watanzania wengi hususan wale wa vijijini. Vilevile, kamilisheni na hakikisheni mnazindua haraka mfumo wa kupima mifuko ya uwezeshaji kwa matokeo ya kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya.”
Comments are closed.