Rais Magufuli Awapigia Simu Wasanii, Awapa Milioni 100 – Video
Rais Dkt. John Magufuli amempigia simu Rais wa Chama cha Muziki Tanzania, Ado Novemba na kumweleza kuwa kuwa anafuatilia shughuli ya kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Magufuli amepiga simu hiyo leo Ijumaa, Novemba 15, 2019 kupitia simu ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati kongamano hilo lilipokuwa likiendelea ukumbini hapo na kusema; “Ninawapenda sana, ninaisikia risala yako, hongereni sana, Waziri Mkuu atatoa maagizo yangu.”
Rais Magufuli pia amempigia tena simu LIVE Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akihutubia katika Kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere na kumwambia atatoa Tsh milioni 100 kwa ajili ya Mfuko wa Wasanii nchini, ambao umeanzishwa leo.
Wasanii hao wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu aliyemuwakilisha Rais JPM waliyakumbushia mambo mengi na makubwa yaliyofanywa na Hayati Baba wa Taifa katika kulijenga taifa hili ambayo kwasasa mambo hayo yanafanywa na Rais JPM.
Awali, wakati risala hiyo ikiendelea kusomwa na rais wa shirikisho la muziki nchini, Ado Novemba aliyekuwa akielelezea jinsi Rais JPM alivyofanikisha kuongeza Zahanati, Hospitali, Shule lukuki kwa kipindi cha miaka minne aliyokaa madarakani kumbe Rais JPM alikuwa akiifuatilia risala hiyo.
Akiendelea kusoma Rais JPM alimpigia simu Waziri Mkuu Majaliwa na kumwambia anaifutilia hotuba hiyo na atahakikisha anayafanyia kazi yote yaliyoorodheshwa kweli risala hiyo. Naye Waziri Mkuu akiwa kwenye tamasha hilo aliwaahidi wasanii hao kuwemo kwenye mpango wa bima ya afya ya bei nafuu.
Wasanii hao pia amewaahidi kuweka mikakati ya kulinda haki zao na kumaliza vilio vya kudhulumiwa kila kukicha. Umati wasanii waliofurika kwenye tamasha hilo ulilipuka kwa mayowe ya furaha baada ya Waziri Mkuu kuhamasisha kuundwa kwa mfuko wa kuwasaidia.
Wakati Waziri Mkuu Majaliwa akihamasisha mfuko huo alianza na kujitolea shilingi milioni tano na kufikisha mpaka milioni 48 kutoka kwa viongozi wengine waliokuwepo kwenye tamasha hilo huku viongozi mbalimbali wakiuchangia mfuko huo Rais JPM alipiga simu tena na kuongezea shilingi 100 na hivyo kufikia milioni 148.
Aidha, Waziri Mkuu amesema; “Uamuzi wenu wa kuandaa tamasha hili ni wa kizalendo na unaakisi nia yenu thabiti ya kuunga mkono jitihada zinazoendana na shughuli ambazo baba wa Taifa alizifanya wakati wa uhai wake na kuwa fundisho kwetu sote.
“Serikali ya Awamu ya Tano inawaheshimu sana, inawathamini sana na inatambua mchango mnaotoa katika taifa letu, Mhe. Rais Magufuli anatambua sana kazi zenu, yupo pamoja nanyi na tutaendelea kufanya kazi pamoja.
“Tunaendelea kusimamia bajeti ya Serikali kuwa na muelekeo wa kugusa maisha ya watanzania pamoja na ikiwa tumeondoa kodi zenye kero zipatazo 57 ambazo pia zimegusa sekta ya sanaa,” amesema Majaliwa.
Comments are closed.