Video: Zitto Aibua Mazito ‘Wametekwa, Wamepigwa, Wamepata Ulemavu’

KIONGOZI wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amelaani vitendo vya utekaji na kuwatesa baadhi wananchi akidai kuwa ni kinyume cha haki huku akiilaumu serikali kwa madai ya kuminya uhuru na kushindwa kuvipa nafasi vyama vya upinzani kufanya siasa kama chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinavyofanya.
Zitto amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa uchumi wa wananchi umekuwa ukishuka siku hadi siku kutokana na serikali kutumia pesa nyingi kwenye miradi mikubwa ya ujenzi kwa fedha za ndani.
“Nimetembelea walioko gerezani, wavuvi waliodhulumiwa wakachomewa nyavu zao, wafanyabiashara wanaobambikiwa kesi, wanafunzi wanaonyimwa na kukosa haki ya elimu bora, wapo waliotekwa wakapotea na hawajaonana na wapendwa wao, wengine walipigwa, wakavunjwa miguu.
“Miaka minne iliyopita tumeshuhudia makundi mbalimbali yakiumizwa na maamuzi na matendo ya watawala, wakosoaji wa watawala wamekumbana na madhila makubwa, wapo waliopewa kesi, waliotekwa na wapo wanaoendelea kupandishwa kizimbani kila leo.
“Mwaka 2019 haukuwa mwaka mzuri kwangu na wanasiasa wenzangu wa upinzani, nimelala selo, nimekutana na wavuvi waliochomewa nyavu zao, wafanyakazi wasiolipwa stahiki zao, wafanyabiashara wanaobambikiziwa kodi,wanafunzi wanaonyimwa fursa za mikopo.
“Serikali ya CCM imeongeza deni la taifa kwa shilingi trilioni 16, kila Mtanzania anadaiwa milioni 1.2 tofauti na mwaka 2015 ambapo alikuwa anadaiwa shilingi laki tisa. Rais Magufuli amekataa kutekeleza mradi wa bandari ya Bagamoyo akisema una masharti makubwa, kitu ambacho ni uongo, kwa sababu hakuna makubaliano ambayo pande mbili zilikuwa zimekubaliana.
“CAG wa wananchi Prof. Assad aliondolewa ofisini kinyume na sheria kwa sababu alikataa kunyamazishwa pale alipokuwa akifichua matendo ya kifisadi yanayofanywa na serikali. Huwezi kupambana na rushwa huku ukikandamiza vyombo vya habari na hutaki uwazi katika utawala wako.
“Licha ya kuzuiwa kufanya siasa miaka minne, vyama vya upinzani vilijiandaa vilivyo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 ili wananchi waonyeshe hasira zao kwa watawala. CCM wakaamua kuweka mpira kwapani na kuchagua viongozi wanaowataka, chama ambacho kimefanya siasa kwa peke yake kwa miaka minne, kiliogopa kwenda kwa wananchi ili kuhukumiwa na hao wananchi.
“2020 ni mwaka wa uchaguzi, sisi ACT Wazalendo tumedhamiria kuijenga Tanzania inayopaa kiuchumi, tukibuni na kutekeleza sera zitakazohakikisha uchumi shirikishi unaozalisha ajira.
“Tukipewa ridhaa ya kuongoza 2020 tutajenga mfumo imara wa kutoa haki, tutahakikisha watu wote walioonewa wanaachiliwa na kuwa huru, na wale ambao wamehukumiwa kinyume na sheria tutahakikisha tunafuta vifungo vyao. Tutaongeza watalii kufikia watalii milioni sita kwa mwaka, tutahakikisha rasilimali zetu zinatumika katika kuendeleza wananchi, tutawekeza katika kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na ufugaji.
“Nikiwa kiongozi wa chama kinachojiandaa kuongoza nchi, ninajua uzito wa changamoto tulizonazo, ambazo nyingine zinatokana na maamuzi ya watawala wa sasa na watangulizi wao kutoka CCM.
“Baada ya miaka minne ya changamoto nyingi kwa Watanzania, ACT Wazalendo kimedhamiria kushirikiana nawe Mtanzania kujenga Tanzania yenye watu wenye raha na furaha, wananchi watakaofanya kazi kwa bidii na kufaidi jasho la kazi yao, Watanzania wachapa kazi na wala bata,” amesema.

