‘Lowassa kutangazwa mapema’

Lowassa (6)
Na Neophitius Kyaruzi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuachana na dhana kuwa mgombea wa Chadema anayeungwa mkono na umoja huo hatatendewa haki na tume huku ikiahidi kwamba atatangazwa mapema iwapo atafanikiwa kushinda.

Ufafanuzi uliotolewa juzi na baadhi ya wanasheria wa tume hiyo katika mahojiano maalum na gazeti hili, unasema kuwa tume hiyo inaendeshwa kwa misingi ya sheria na maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na maadili ya mwaka huu, hivyo watarajie kuwa na uchaguzi huru na wa haki unaosimamia misingi hiyo.

“Tunajua baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakieneza maneno kuwa NEC haitatenda haki kwa baadhi ya wagombea lakini niseme tu kwamba tume hii haiendeshwi kwa misingi ya matakwa ya watu fulani bali ni chombo cha kisheria hivyo kinafanya kazi katika misingi hiyo na kamwe hakitapendelea mwanasiasa au chama chochote badala yake kitatenda haki,” alisema mwanasheria wa tume hiyo, (jina tunalihifadhi kwa kuwa si msemaji).

Wanasheria hao walisema kuwa wamekuwa wakiwashangaa baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa mihadhara ya kuchochea vurugu kwamba zipo dalili ya wagombea wao kuonewa na tume hiyo jambo ambalo si kweli kwani maadili yatakayotumika katika uchaguzi yalishirikisha viongozi wa juu wa vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi.

Walisema kuwa baada ya majadiliano ya kina kuhusu kanuni na maadili ya uchaguzi, wajumbe kutoka vyama 22 vya siasa vilikubali maadili hayo na kukubali kuyatekeleza, hivyo hoja ya kwamba NEC inaweza kuwaonea ni uzushi unaoashiria kutojiamini kisiasa.

“Julai 27, mwaka huu, wawakilishi kutoka vyama 22 vya siasa nchini baada ya kushiriki kikamilifu walisaini waraka wa maadili huku wakikubali maadili hayo na kukubali kuyatekeleza, hivyo tunashangaa kusikia baadhi ya wanasiasa kuwa na hisia za kuonewa wakati NEC haijatoka nje ya mipaka ya maadili hayo,” alisema mwanasheria huyo.

Mwanasheria mwingine ambaye pia hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa tume hiyo, aliwataja wajumbe wengine walioshiriki kusaini maadili hayo kuwa ni wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani, serikali na NEC yenyewe na kuongeza kwamba maadili hayo ndiyo kanuni zinazotumika katika uchaguzi kwa mujibu wa makubaliano ya pamoja.

Wakitolea mfano wa malalamiko ya hivi karibuni ya Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia kwamba serikali imeanza kufanya uonevu dhidi ya vyama na wafuasi wa vyama vya upinzani wanasheria hao walisema kwamba hoja hizo hazina msingi.

“Kwanza huyu Mbatia anapaswa kutambua kuwa sehemu ya tatu, kipengele Na.3.1 (b), kinasema kuwa serikali ihakikishe kwamba kuna amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi… vizingatie mahitaji na usalama wa makundi maalum kama watu wanaoishi na ulemavu, wazee, wanawake, wajawazito na wenye watoto wachanga.

Kwa kutumia kipengele hicho tume ina uwezo wa kuihoji serikali iwapo haitatekeleza hayo,” alisema mwanasheria huyo.


Loading...

Toa comment