The House of Favourite Newspapers

Lowassa: Magufuli, Tundu Lissu Asikutishe, Dunia Inajua

0

KITENDO cha mgombea urais wa Tanzania, kupitia Chadema, Tundu Lissu kuonekana kwenye televisheni na kuzunguka majimboni wakati wa kampeni zake, kimebezwa na Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho mwaka 2015. 

 

Akizungumza leo tarehe 24 Septemba, 2020 kwenye kikao cha ndani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Monduli jijini Arusha ambapo mwanae, Fred Lowassa anawania jimbo hilo. Lowassa amemsifu aliyekuwa mpinzani wake mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Dk. John Magufuli, kwamba utawala wake umefanya makubwa.

 

 

Lowassa amemtaka Dk. Magufuli ambaye ni mgombea urais wa CCM kutokuwa na wasiwasi wa kushinda kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

 

Lowassa amesema, “Huko kwa kina Lissu wameanza kujipambanua sana, maneno mengi, fujo zile, wanaonekana kwenye mamitaa, maTV (televisheni), matv pengine yanatishatisha, lakini tulimwambia rais wetu, usitishike hata kidogo, umma wa Watanzania upo nyuma yako na dunia inajua,” amesema Lowassa.

 

Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, amesema, hana mashaka na ushindi wa Dk. Magufuli na kwamba, alicho na mashaka nacho ni idadi ya kura zake za ushindi.

 

“Umma wa Watanzania uko nyuma yako na dunia inajua kwamba kuna mwanaume Tanzania. Nasema hivyo kwa sababu, Australia kama ulisikiliza BBC leo, rais anajiuzulu, kule Bolivia rais anajiuzulu, yote kwa sababu ya hii kitu, corona si mchezo.

 

“Nyinyi mtu wenu tena mtu mweusi hana nguvu za Mitume anawaambia Taifa lake jamani tumuende MUNGU tumuombe tuepukane na hili janga, watu wa ajabu wakasema anababaisha, tumepita wiki mbili tatu hamna Corona,” amesema Lowassa.

Lowassa alijiunga na Chadema Jumanne tarehe 28 Julai 2015, akiambatana na familia yake, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.

 

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Lowassa alipata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39.97 huku Dk. Magufuli akipata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46. Hata hivyo, Lowassa alirejea CCM tarehe 1 Machi 2019 na kupokewa na Dk. Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, kwenye ofisi ndogo ya CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam.

 

Wengine waliompokea Lowassa aliporejea CCM ni pamoja Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti CCM-Bara), Dk. Bashiru Ally (Katibu Mkuu), Humphery Polepole (Katibu wa Itikadi na Uenezi), Kasim Majaliwa (Waziri Mkuu) na swahiba wake wa siku nyingi Rostam Aziz.

Leave A Reply