Lowassa: Tume Ya Uchaguzi Inampendelea Dk. Magufuli 

LOWASSA_0.jpgEdward Ngoyai Lowassa.

MGOMBEA wa nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Ngoyai Lowassa, amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeonesha dalili za kumpendelea mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli katika matokeo ya nafasi ya urais.

Lowassa aliyasema hayo mkoani Arusha jana, alipolazimika kuita vyombo vya habari na kuonesha wasiwasi wake dhidi ya tume, muda mfupi baada ya kutangazwa matokeo ya awali, asubuhi.

Katika malalamiko hayo, Lowassa aliishutumu tume kwa kutangaza matokeo hayo, kwa kile alichokiita ‘kutowaandaa wananchi kisaikolojia’.

Lowassa alililaumu jeshi la polisi kwa kitendo cha kuwakamata baadhi ya vijana katika maeneo ya Kinondoni na Mwananyamala jijini Dar na kuwaweka selo.

“Tume wanatangaza matokeo kwa kuonesha dalili ya kuipendelea CCM na mgombea wake, Magufuli kwani bila kuwaandaa wananchi kisaikoloji, hatashinda.

“Pili, nimesikitishwa sana na kitendo cha polisi kuwakamata vijana kiholela, pale Kinondoni na Mwananyamala,” alisema Lowassa.

magufuli
Dk. Magufuli

MAGUFULI ALIVYOKIMBIZA

Katika majimbo ambayo Nec ilitangaza na kuonesha wazi ushindi wa Dk. Magufuli dhidi ya Lowassa ni kama ifuatavyo;

Jimbo la Nsimbo mkoani Katavi, Dk. Magufuli alishinda kwa kura 4,229 sawa na asilimia 83.14 huku Lowassa akipata jumla ya kura 6,042, sawa na asilimia 9.9.

Katika Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara, Dk. Magufuli aliibuka kidedea kwa kujinyakulia jumla ya kura 33,699,  sawa na asilimia 62.34 huku Lowassa akiambulia kura 19,017, sawa na asilimia 35.18.

Huko Kaskazini Unguja kwenye Jimbo la Donge, Dk. Magufuli alipata kura 5,592 ikiwa ni asilimia 83.39 na Lowassa akajikusanyia 1,019 sawa na asilimia 15.2.

Katika Jimbo la Kiwengwa, Nec ilitangaza kuwa Dk. Magufuli alipata jumla ya kura 3,317 ikiwa ni sawa na asilimia 73.30 huku Lowassa akiambulia kura 1,104, sawa na asilimia 24.40.

Katika Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, Dk. Magufuli aliibuka kidedea kwa kura 35,310, sawa na asilimia 80.25 ambapo Lowassa alipata kura 7,928, sawa na silimia 18.01.

Kwenye Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani, Dk. Magufuli alipata jumla ya kura 34,604, sawa na asilimia 57.15, huku Lowassa akipata kura 25,448, sawa na asilimia 42.05.

Katika majimbo yote matatu  yaliyotangazwa na Nec awali, asubuhi katika Jimbo la Makunduchi, Dk. Magufuli alipata kura 8,606 na Lowassa akapata 1769.

Kwenye Jimbo la Lulindi, Dk. Magufuli alipata kura 31,602 huku Lowassa akiambulia 11,545 na katika Jimbo la Paje visiwani Zanzibar, Dk. Magufuli alipata kura 6,035 dhidi ya Lowassa aliyeapata kura 1,899.

Loading...

Toa comment