The House of Favourite Newspapers

Luis Aikumbushe Simba Mapema Kuna Hatari Mbele

0

LAZIMA ukubali kwamba kama ukiamua kufanya kazi na wakubwa wakubwa, basi lazima ukubali kuwa na mawazo ya kikubwa na uishi maisha ya aina yao.

 

 

Klabu ya Simba imeamua kuwa klabu kubwa si Tanzania pekee, badala yake sasa wanaangalia zaidi barani Afrika ambako tayari kuna vigogo wake.

 

 

Safari ya Simba kutaka kuwa bora na wakubwa barani Afrika si nyepesi na haiwezi kuwa nyepesi. Wao wanalijua hili ndiyo maana wamekuwa na mikakati kadha wa kadha kuhakikisha wanakuwa katika kiwango hicho wanachokitaka.

 

 

Wanajua yanahitajika mambo mengi sana ya kufanyika ili wafikie katika kiwango hicho. Vizuri wamejipanga na unaona hatua wanazoanza kuchukua kwenda wanapotaka zinakuwa na mashiko au mwonekano mzuri.

 

 

Simba wanajua juu watazikuta klabu nyingi kubwa kama Al Ahly, Esperance, Mamelodi, TP Mazembe na nyingine. Wameonyesha kutolihofia hilo na nia yao ni kujifunza na kuendelea kukua zaidi.

 

 

Tunawaona Simba wamekuwa na mwendo mzuri sana, unaona mfano msimu huu baada ya mechi nne za hatua ya makundi wameshinda mechi tatu na sare moja. Unaona wameshinda ugenini mara tatu na kutoa sare moja.

 

 

Simba ni moja ya timu ambayo haijaruhusu hata bao moja katika mechi zake nne wakati walipocheza hatua hiyo msimu uliopita, ndani ya mechi tatu za ugenini, walifungwa mabao 13.

 

 

Simba sasa wanakua na wanajifunza kupitia makosa. Inaonekana watafikia mbali kwa kuwa ni wale waliokubali kujifunza kulingana na makosa ambayo waliyafanya. Kwa kifupi, wameamua kuishi na wakubwa na wao ni wakubwa.

 

 

Ili kuendelea kuwa wakubwa lazima Simba wajifunze mambo mengi ya wakubwa nami nilikuwa ninawakumbusha hili suala la kiungo wao nyota Luis Miquissone raia wa Msumbiji, kwamba kwa hapa alipofikia anaiamsha Simba kwamba lazima waanze kujiandaa mapema wa kuziba nafasi yake.

 

 

Bila ya ubishi, baada ya msimu huu ofa za Miquissone zitaanza kumiminika kutoka katika klabu mbalimbali kubwa ambao ndiyo hao wakubwa kwa kuwa wana uwezo mkubwa wa kifedha. Hiyo itawafanya wao kuamua suala la ununuzi.

 

 

Simba wanaweza kukataa lakini ofa ikawa kubwa na yenye ushawishi au Simba wanaweza kukataa na mchezaji akalazimisha. Maana yake ni hivi, sasa Miquissone ni tegemeo la Simba lakini kuna kipindi ataondoka kutokana na wakubwa wanavyotaka.

 

 

Tabia za wakubwa ni kupata vitu bora na kama Miquissone ameonyesha uwezo, basi lazima klabu moja mbili watamuwinda, hii maana yake Simba wanapaswa kujiandaa mapema, kwamba ikitokea wamemuuza Miquissone ameondoka, nani atashika nafasi yake?

 

 

Kwamba wanajua wao bila Miquissone basi watakuwa wamepungukiwa kitu, basi sasa ulikuwa ni wakati wa wao pia kuanza “kuchungulia” katika klabu mkbalimbali kwa wake watachukua nafasi yake.

 

 

Hii ndiyo kuishi kikubwa, maana yake unakuwa tayari wakati wowote, unapomuuza fulani basi unajua kuna fulani anakuwa tayari kuingia na kuchukua nafasi yake.

 

 

Kujiandaa mapema ni vizuri zaidi lakini lazima ujue suala la kufanyabiashara unapokuwa mkubwa ni zaidi ya lazima, hauwezi kukwepa. Na vizuri kwa Simba wamekuwa wepesi kuwaachia wachezaji wao kwenda kucheza nje au kwingine, hivyo hili haliwezi kuwasumbua.

 

 

Namtolea mfano Miquissone kwa kuwa katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, hakika amejitahidi sana, amefanya vizuri.

 

 

Tayari anaonekana na tayari wakubwa wengine wameshakaa vikao na kuangalia uwezo wake. Hivyo wakati wowote wanaweza kutua Simba na kuweka dau mezani.

 

 

Wakati wa kujiandaa kwa Simba ni sasa, kwamba kama wakifanyabiashara na wao watafanya vipi kuhakikisha wanapata mtu na kikosi chao kinaendelea kuwa imara.

 

 

Hatari iliyopo mbele ni hivi; kama mtakuwa mnauza tu na hakuna kusajili, au mnasajili lakini si usajil bora, basi baada ya muda mfupi, kikosi kitashuka hadhi na uwezo na baadaye kuanza kuboronga.

Leave A Reply