The House of Favourite Newspapers

Luis Atinga Anga za Morrison Bongo

0

DAKIKA 85 alizotumia kiungo mshambuliaji wa Simba, Luis Jose Miquissone kwenye mchezo kati ya Simba na Kagera Sugar, juzi Jumanne, zilitosha kabisa kuonyesha umwamba wake kwenye soka la Bongo.

 

Luis ambaye alisajiliwa na Simba akitokea UD do Songo ya nchini kwao Msumbiji akiwa ni mchezaji pekee mgeni aliyesajiliwa na timu hiyo kwenye dirisha dogo la usajili, alianza kwenye mchezo huo na kufanya mambo makubwa ambayo yamemfanya aache gumzo. Alitolewa dakika ya 85 na kuingia Hassan Dilunga.

 

Kiungo huyo alitumia dakika 45 za mwanzoni kuonyesha mambo makubwa kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar na Simba kushinda bao 1-0.

 

Mbali na mashuti makali ambayo alikuwa akiyapiga, lakini dakika za mwishoni kipindi cha kwanza aliacha gumzo baada ya kuwachambua viungo watatu wa Kagera huku akiondoka kwa mbwembwe nyingi jambo ambalo liliwaacha mashabiki wa timu hiyo kinywa wazi.

Awali alionekana kuwa mzuri wa kuchukua mpira na kuachia, lakini alipopata nafasi zaidi alionyesha maujuzi makubwa. Kwenye mitandao ya kijamii, jana yeye ndiye alikuwa ametawala, lakini video nyingi zilikuwa zikimfananisha na Clatous Chama na Bernand Morrison wa Yanga, ambao hapo nyuma walikuwa wameacha gumzo.

 

Morrison anakumbukwa kwa kuonyesha mbwembwe zake za kutembea juu ya mpira, lakini Chama yeye anakumbukwa kutokana na mbwembwe nyingi alizokuwa akifanya kwenye michezo ya ligi msimu uliopita. Uwezo wa Luis, ambaye alipiga mashuti matatu kwenye mchezo wa juzi, umewaibua wengi lakini msemaji wa timu hiyo, Haji Manara ametumia ukurasa wake wa Instagram kuandika: “TFF na Bodi ya Ligi ongezeni viingilio katika game (mechi) zetu.

Ni dhambi kulipa pesa ile kumwangalia Luis akicheza, sasa nilikuwa najiuliza namuangalia Messi au?

“Sasa hivi kubaki home wakati Miquissone anacheza ni kosa linaloweza kukuweka ‘lock up’ wiki.” Hii ina maana kuwa kiungo huyo raia wa Msumbiji ameshaingia kwenye anga za mastaa wakubwa wa soka la Bongo na anaaminika kuwa anaweza kufanya mambo makuwa zaidi huko mbele.

 

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, amemzungumzia kiungo huyo kwa kusema: “Miquissone ni mchezaji mzuri sana, nazidi kuvutiwa na anavyocheza kila siku japo namuona akiwa hajazoea vizuri mazingira, hivyo huko mbele akiyazoea mazingira atatusaidia sana,” alisema kocha huyo.

SPOTI HAUSI: SABABU za YANGA Kupata SARE MFULULIZO ni HIZI…

Leave A Reply