The House of Favourite Newspapers

LUKAMBA: KUTOKA MTAANI, UIGIZAJI, HADI KUANGUKIA KWA DIAMOND

Lukamba Akiwa Kazini

Mmoja kati ya vijana waliofanya kazi ya kupiga picha za video (Videographer) kuthaminiwa na kupewa heshima kubwa zaidi ni,
Ashraf Haji maarufu kama Lukamba, ambaye jina lake limenga’ra zaidi kupitia Mkali wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz.

Lukamba akiwa ameweka pozi na kamera mkononi

Lukamba kwa sasa ni Videographer wa Diamond Platnumz, lakini kabla ya hapo alikuwa na ndoto ya kuwa muigizaji mkubwa
na tayari alishaanza kujishughulisha na masuala ya uigizaji ambapo Muandaaji wa filamu nchini, William Mtitu,
alishamuandaa kumtoa katika filamu ambayo angecheza kama Hemed Phd wa pili.

Lukamba Akiwa Kazini na Diamond

Ndoto ya kuwa muigizaji mkubwa ilififia kutokana na maslahi, kumbe wakati huo Mungu alikuwa ameshafungua milango ya baraka.

Akiwa Katika Harakati za kutafuta nafasi ya kupenya WCB, Lavalava alimfuata Lukamba ambaye alikuwa akiishi naye maeneo ya Bunju na kumuomba amshuti Kava ya wimbo wa Diamond wa ‘Utanipenda’.

Lukamba Akiwa na Lavalava

Lukamba alikubali na ilipokamilika kava hiyo Lavalava aliichukua na kuipeleka WCB, Diamond alipoiona Kava hiyo kitu cha kwanza alichouliza ni nani ameshuti kava hiyo, naye Lavalava bila hiyana akalitaja jina la Lukamba.

Siku iliyofuata Diamond alimwambia Lavalava amuite Lukamba na walipoonana akamuuliza kama ameajiriwa akajibu hapana, basi huo ndiyo ukawa mwanzo wake wa kufanya kazi WCB na kwa mara ya kwanza alianza kufanya kazi na Rayvanny kama sehemu ya majaribio na Diamond aliporidhishwa na kazi zake akamchukua rasmi kuwa Mpiga picha wake wa Video na kwa mara ya kwanza akakwea pipa kwenda Afrika Kusini akiwa na mkali huyo wa Bongo Fleva huku akiwa amejawa na kitete na hofu kubwa kwani alikuwa akimuogopa kidogo.

Kushoto ni Lukamba, Katika Mwanamuziki wa Marekani Omarion, Kulia ni Diamond

Ukimuuliza Lukamba Mafanikio aliyoyapata tangu aanze kufanya kazi na Diamond chini ya WCB atakwambia kwanza Kujulikana kwani hakuna mahali utafika wasilijue jina lake hivyo umaarufu umempa fursa nyingi za mafanikio, lakini pia kwa sasa ni baba mwenye gari anamiliki ndinga aina ya Altezza aliyopewa na Bosi wake kama zawadi na shukrani ya kutambua mchango alioutoa kwenye kusogeza muziki wake mbele.

Lukamba Akiwa juu ya Altezza Yake

Mbali tu na kuwa Mpiga Picha anayeheshimiwa zaidi na wasanii wa ndani na nje ya nchi hiyo pekee kwake haitoshi, Lukamba amedhamiria kuwachomoa wapiga picha wengine mitaani na kuwaleta kwenye ramani aliyopo yeye ambapo ameshaanza taratibu za kufungua kampuni yake inayoitwa It’s Lukamba itakayokuwa inajishughulisha na utayarishaji wa Video (Video Production) ambapo atatoa fursa za ajira kwa vijana wenye vipaji kama vyake ambao wanapambana na mitaa kwa sasa.

Lukamba Akiwa na Mwanamuziki wa Jamaica Morgan Heritage

Kuna vitu vingi sana vya kujifunza kwa Lukamba ambavyo kijana wa leo unayeishi kwa malengo na unatamani kufanikisha malengo yako basi unapaswa kuiga, kwanza  ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 26 lakini ni mpambanaji, mvumilivu, mwenye nidhamu na anayependa kazi yake, vitu vilivyomfanya Diamond kwa moyo mkunjufu kuzama mfukoni na kutoa pesa za kumnunulia gari.

Lukamba Akiwa na Diamond Siku Aliyopewa Gari

Kwa upande wa familia Lukamba ameoa na ni baba wa mtoto mmoja aitwaye Imran.

Mtoto wa lukamba Anaitwa Imran

Makala Hii imeandikwa na isri Mohamed.

Comments are closed.