LULU AVUNJA REKODI YA ZARI

DAR ES SALAAM: Kamwene Lulu! Ndivyo unavyoweza kumsalimia mwanadada mrembo kutoka kiwanda cha Bongo Muvi, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ukikutana naye baada ya kuvunja rekodi iliyowahi kuwekwa na mwanamama mjasiriamali kutoka Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Bosslady’ ambaye ni mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

KAMWENE NI NINI?

Kamwene ni salamu inayotokana na kabila la Wahehe kutoka mkoani Iringa inayomaanisha hujambo? Salamu hii imejichukulia umaarufu mkubwa hivi karibuni baada ya kutumika katika sherehe za utoaji Tuzo za Sinema Zetu za Kimataifa za Sziff zilizofanyika wikiendi iliyopita kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar ambapo watoto wawili, Flora Kihombo (11) na Rashid Msigalla (10) waliotwaa tuzo hizo walisikika wakisalimia mashabiki “KAMWENE”!

TURUDI KWA LULU

Katika usiku huo wa tuzo, Lulu alikuwa mshereheshaji mkuu ‘MC’ sambamba na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Azam, Baruani Muhuza. Katika tukio hilo, Lulu aliweka rekodi ya ulinzi mkali kwa kulindwa na msafara ambao hakuna staa yeyote Bongo aliyewahi kufanyiwa hivyo kwani hata ule wa Zari haukufikia kiwango hicho.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia msafara wa Lulu ambao ulianzia maeno ya Kijitonyama katika Jengo la Millenium Tower jijini Dar, staa huyo alivalia gauni jekundu ambapo muda mwingi hakutaka mtu wa pembeni alishike zaidi yake huku nje ya jengo hilo magari ya kifahari yakimsubiri likiwemo Range Rover Sport ambalo alilitumia kumbeba.

“Tulijua huenda anatengeneza filamu mwanzoni wakati anapodolewa, kumbe alikuwa akifanya kweli. Mabodigadi walioshiba wawili walikuwa wakimlinda kila kona, kuanzia anapambwa hadi anatoka katika jengo hilo. Kifupi walikuwa hawachezi mbali mpaka anaingia kwenye gari huku wakipeana zamu ya kufungua milango na kufunga,” kilisema chanzo.

ULINZI WAKE WASHTUA WENGI

Baada ya kutoka katika jengo hilo ambalo ilikuwa hatua yake ya kwanza kujiremba, Lulu aliongozana na magari hayo ya kifahari yasiyopungua matano pamoja na king’ora cha pikipiki ya Polisi, zote zikiwasha taa mithili ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au kiongozi mkubwa anapita.

“Barabara nzima kutoka Kijitonyama kwa kutumia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kisha kukata Mwenge na kuingia Barabara ya Sam Nujoma, magari yalikuwa yakipisha hivyo kushtua watu walioshuhudia msafara huo uliojaa mbwembwe kama zote. Hadi wanaingia Mlimani City, bado kuna wengine walikuwa hawaamini anayeongozwa na msafara huo kama ni Lulu au ni kiongozi mkubwa wa nchi.

MASTAA WAPIGWA NA BUTWAA

Baadhi ya mastaa ambao walikuwa wameshatangulia ukumbini hapo kushuhudia utoaji tuzo hizo walipigwa na butwaa baada ya kumuona Lulu akifunguliwa mlango na mabaunsa kisha kumsindikiza hadi ndani kwa ajili ya kuvaa nguo nyingine. “Si vizuri kuwataja, lakini ni hawa mastaa wenzake wakubwa tu wanaofanya naye filamu. Hawakuamini kwa jinsi alivyoshuka kwa ulinzi mkali,” kilimaliza kudokeza chanzo ambacho ni mmoja wa watu waliokuwa wakifuatilia kwa karibu tukio hilo la Lulu.

ANAVUNJAJE REKODI YA ZARI?

Oktoba, 2017, Zari akiwa katika uhusiano na Diamond alipata mualiko wa kwenda kufungua duka jipya la Danube lililopo ndani ya Mlimani City jijini Dar.

Katika siku hiyo inayoaminika ilikuwa rekodi mpya Bongo, mbwembwe zilikuwa za kutosha kutokana na watu wengi kujazana katika jengo hilo huku wengine wakimzingira Zari na kulitaja jina la wifi. Hata hivyo, Lulu anatajwa kuvunja rekodi hiyo baada ya kumzidi Zari kwa idadi ya magari ya kifahari na ulinzi mkali wa Polisi na mabaunsa.

STORI: Andrew Carlos, Risasi Mchanganyiko

Toa comment