The House of Favourite Newspapers

LUNGI ANUSURIKA KUCHINJWA

DAR ES SALAAM: Msanii wa filamu Bongo, Lungi Maulanga hivi karibuni alionja joto ya jiwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam na kunusurika kuchinjwa baada ya mtu aliyejulikana kwa jina moja la Khassimu kumpiga kwa bapa la panga katika maeneo ya mbalimbali ya mwili wake.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea alfajiri ya Jumamosi iliyopita ambapo mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwa Lungi akiwa na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la mama Kessy anayedaiwa ni ndugu yake na kukata bomba za mashine ya kupoza hewa (AC) ikiwa haijazimwa ili aiibe. Alizungumza na Gazeti la Amani siku ya tukio, Lungi alisema kuwa alifanyiwa unyama huo nyumbani kwake na watu ambao wanajulikana kwa matukio ya uhalifu katika mtaa huo.

Akifunguka zaidi msanii huyo alikuwa na haya ya kusema: “Nilikuwa nimelala ghafla nikaona hewa nzito baada ya kukatiwa AC na kwa kuwa ilikuwa sijaizima ile hewa ilitoka na kuingia kwenye madirisha ya nyumba ya pili na majirani hao wakahisi hewa nzito.

“Wakaanza kupiga kelele na wakatoka nje, baada ya kutoka wakawa wanatafuta ni eneo gani ile hewa inatoka, wakakuta ni kwenye ile AC yangu na wakawaona watu waliokuwa wanaikata, mmoja wa wezi hao alikuwa amejifunika tisheti usoni. “Baada ya kuona watu, wezi hao wakakimbia kuelekea nyumba nyingine ambayo ipo jirani sehemu yenyewe wanauza pombe za kienyeji. Wale majirani zangu wakaniamsha, baada ya mimi kutoka wakaniambia kuwa aliyekata AC amekimbilia kwenye nyumba ya jirani.

“Ilibidi mimi na wale majirani twende kwenye nyumba ambayo yule mwizi alikimbilia, kufika pale akatoka kaka mmoja aitwaye Saidi na dada mmoja ambaye ndiye yule aliyekuja na yule mwizi, mimi nikawauliza mbona mwizi aliyetaka kuiba AC yangu ameingia humo ndani kwao? Saidi aliamua kutoka na panga na kuanza kunitukana na kusema mimi nitafanya nini hata kama mwizi kaingia humo ndani?

“Ghafla Saidi akaanza kunipiga na ubapa wa panga na kuna moja nilikwepa, ilikuwa kidogo tu anikate shingoni. Nashukuru Mungu wale majirani zangu walingilia kati kuniokoa, nilipotoka pale nilienda moja kwa moja Kituo cha Polisi cha Magomeni na wakanifungulia jalada lenye namba MAG RB 73082018 (shambulio la mwili na kuibiwa), tukarudi kwenye ile nyumba na polisi na kukuta Saidi hayupo, akakamatwa yule dada, mama Kessy.

“Vijana hao wahuni waliposikia nimeleta polisi wamesema kwamba pale mimi sitaishi vizuri kwani wao hawaogopi polisi kwa kuwa wakipelekwa asubuhi, jioni wanarudi,” alisema Lungi. Afisa mmoja wa Kituo cha Polisi cha Magomeni ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji alithibitisha Lungi kufungua jalada kituoni hapo na akasema polisi watafanya uchunguzi.

Stori: Neema Adrian, Amani

Comments are closed.