The House of Favourite Newspapers

Lwandamina akabidhi Wazambia wawili Yanga

AKIENDELEA kukiboresha kikosi chake, Kocha Mkuu wa Yanga Mzambia, George Lwandamina amekabidhi majina mawili ya kiungo na mshambuliaji mmoja wa kimataifa atakaowasajili kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo, tayari imeanza maandalizi ya usajili wa wachezaji wapya wa msimu ujao wa ligi kuu kwa kuanza kufanya mazungumzo na kiungo wa Mbeya City, Kenny Ally.

Yanga huenda ikasajili wachezaji wengi katika msimu ujao wa ligi kuu kutokana wachezaji wake 12, mikataba yao kumalizika akiwemo Donald Ngoma, Thabani Kamusoko (wote raia wa Zimbabwe), Vincent Bossou na Haji Mwinyi.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Lwandamina tayari ametoa mapendekezo ya wachezaji wawili kwa uongozi ambao anaamini kama akiwapata kazi itakuwa imemalizika kutokana na ubora wa wachezaji hao.

Mtoa taarifa huyo alisema, majina ya wachezaji amepanga kuyakabidhi mara baada ya kurejea nchini akitokea nyumbani kwao Zambia alikobaki baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa kumalizika dhidi ya Zanaco.

“Hatutaki kumuingilia kocha wetu kwenye usajili wake na kwa kifupi tulichopanga ni kumuachia kila kitu yeye kuamua mchezaji yupi amsajili na yupi amuache ili kuepuka visingizio baadaye.

“Hivyo, hivi karibuni tulifanya kikao na Lwandamina na  akatuambia kuwa tayari amewaona wachezaji wawili wa kimataifa ambao anaamini kama akiwapata, basi kikosi chake kitakuwa tishio. “Majina hayo mawili amepanga kuyakabidhi kwa viongozi mara baada ya kurejea Dar akitokea Zambia alikobaki kwa ajili ya kuiangalia familia yake, tunaamini wachezaji hao ni wazuri kwa kuwa wanatoka kwenye nchi hiyo na anawafahamu,” alisema mtoa taarifa huyo. Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa hivi karibuni aliwahi kuliambia Championi kuwa jukumu la usajili wa wachezaji wapya na wa zamani wamemuachia kocha wao Lwandamina na yeye ndiye ataamua.

Na Wilbert Moland/CHAMPIONI/GPL

Comments are closed.