The House of Favourite Newspapers

Ma-Miss Hawa: Historia Itawakumbuka!

0

HISTORIA ina kanuni moja. Huwa haidanganyi. Utafanya jambo leo, lakini miaka kadhaa baadaye likaibuka na kubaki kielelezo muhimu kwa vizazi vingine, ndiyo maana msisitizo ni mpana juu ya utendaji wa mambo yenye tija katika jamii na maisha kwa jumla.

Leo, nataka niwagusie warembo wanne. Ambao umaarufu na kujulikana kwao kumetokana na ushiriki na ushindi wao kwenye shindano la U-miss hapa nyumbani. Kiini cha mada yangu, ni mambo ambayo wamekuwa wakiyafanya kwa jamii, tangu dunia iwatambue kupitia shindano hilo.

 

HOYCE TEMU

Huyu ni Miss Tanzania mwaka 1999, ambaye tangu hapo amekuwa akijihusisha sana na masuala ya kijamii ikiwemo kusaidia wenye uhitaji, hususan watoto. Hivi karibuni amekuwa akiratibu na kutangaza Kipindi cha Mimi na Tanzania, ambacho kiliibua watu wengi wenye matatizo yaliyohitaji msaada wa haraka na kwa kufanya hivyo, wengi wamepata unafuu wa maisha na kila kitu kubadilika.

 

JACQUELINE MENGI

Anajulikana zaidi kwa jina la Jacqueline Ntuya-baliwe au K-Lyn. Alinyakua taji la Miss Tanzania mwaka uliofuata, yaani 2000. Kwa sasa anaitwa Jacqueline Mengi, hii ni baada ya kuolewa na mfanya-biashara maarufu nchini, Dk. Reginald Mengi.

 

Jacqueline Mengi, amegeuka kioo cha jamii kufuatia kujitoa zaidi kwenye kusaidia masuala ya elimu, ikiwemo ukarabati wa vyumba vya madarasa, utoaji wa vitabu vya maktaba mashuleni pamoja na shughuli zingine muhimu za kijamii, kupitia taasisi yake ya Dk. Ntuyabaliwe Foundation, ikiwa ni njia ya kumuenzi marehemu baba yake, Dk. Ntuyabaliwe.

 

HAPPINESS MAGESE

Ni Miss Tanzania mwaka 2001. Tangu hapo amekuwa akipambana na maisha kwa kushirikiana na jamii, kwa kutoa misaada mbalimbali. Mrembo huyu ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Millen Magese (MMF), ikijihusisha zaidi na utoaji wa elimu juu ya ugonjwa wa wanawake wa kupata maumivu makali zaidi wakati wa hedhi (Endometriosis), ugonjwa ambao yeye mwenyewe ni mhanga huku ikikadiriwa zaidi ya wanawake milioni 176 duniani kote wanasumbuliwa na tatizo hilo.

 

Katika kuonesha kuwa anakabiliana na tatizo hilo, Millen amekuwa akiandaa semina mbalimbali shuleni, akitoa elimu juu ya tatizo hilo na namna ya kujikinga nalo, pia amewahi kuomba eneo la kujenga hospitali kubwa ya kisasa ya kutibu ugonjwa huo hatari zaidi duniani.

Katika kutambua mchango wake kimataifa, Millen aliwahi kupewa Tuzo ya BET, Music Meets Runway Global Awards, pia kuwahi kutajwa na BBC Unsung Hero.

 

FLAVIANA MATATA

Huyu ni mwasisi wa Taasisi ya Flaviana Matata, ambayo pia inajihusisha na kutoa misaada mbalimbali ya kielimu kwa watoto wa kike wenye uwezo mdogo, akiamini ukimpa elimu mtoto wa kike, ndiyo chanzo cha kutengeneza jamii imara yenye mafanikio lukuki.

 

Flaviana ambaye ni mshindi wa kwanza wa Shindano la Miss Universe nchini, mara nyingi amekuwa akijitoa kwenye jamii, jambo ambalo anasema alilitoa kwa baba yake, ambaye amekuwa akimshuhudia akifanya mambo mbalimbali kwa jamii inayomzunguka.

 

Orodha ni ndefu, lakini makala haya yatoshe tu kuwatambulisha warembo hawa kama nembo halisi ya kukumbukwa na jamii, wakitokea kwenye mashindano ya U-miss na sasa jamii inafaidika kwa jitihada na nguvu zao. Niwapongeze kwa ufanisi wao wa mambo hayo, Mungu azidi kuwatia nguvu na kuwabariki zaidi kwa kile ambacho wanakitoa kwa ajili ya wengine.

 

Na BRIGHTON MASALU

Leave A Reply