MA-MISS T Z WALIOTOBOA

SHINDANO la urembo nchini Tanzania (Miss Tanzania) lilipata kuwa moja ya mashindano makubwa hapa nchini. Shindano hili lilivuta hisia za wengi.

 

Lilikuwa na msisimko wa aina yake na hata warembo wake waliokuwa wakishiriki, walikuwa wana hadhi yao na mwonekano wa tofauti na ilivyo hivi sasa. Ilikuwa mrembo akishinda taji hili ni ngumu kusahaulika masikioni mwa watu.Shindano hili la urembo liliwahi kufungiwa hapa nchini mwaka 1968 kisha kufunguliwa mwaka 1994.

 

Baada ya kufunguliwa ndipo lilipoanza kuibua msisimko mkubwa na kuwafanya watu kuwa na shauku ya kutaka kujua nani atachukua taji hilo kila mwaka.Shindano la Miss Tanzania lilipata sifa ya kutoa warembo wasomi na wenye uelewa mkubwa hadi pale lilipofungiwa kwa mara nyingine mwaka 2014. Lilifungiwa kutokana na tuhuma za kupanga matokeo (washindi) na kutotoa zawadi za kueleweka.

 

Kuna warembo wengi ambao wamepita kipindi cha nyuma cha shindano hilo ambao leo hii wana mwonekano au wanatazamwa kwa jicho la tofauti kwenye jamii kwa kufanya kazi zao zinazoonekana na kujulikana. Wengine wameaminiwa na kupewa nafasi kwenye mashirika makubwa huku wengine wakiwa wameanzisha miradi, taasisi, mifuko au kampuni zao na wenyewe ni wakurugenzi.

 

Wafuatao ni warembo waliotwaa Taji la Miss Tanzania ambao sasa wamejitengenezea maisha yao kutokana na kazi zao wanazofanya, lakini kupitia nguvu ya mashindano hayo kuanzia mwaka 1994;

 

AINA MAEDA (1994)

Baada ya mashindano haya kufunguliwa upya, Aina ndiye aliyeibuka kidedea na kuwa Miss Tanzania mwaka 1994. Aina aliwavutia majaji kwa jinsi alivyokuwa akijibu maswali. Pia alibebwa na urefu aliokuwa nao na rangi yake nyeusi ya kuteleza.

 

Baada ya shindano hili, mrembo huyu ilielezwa kwamba, alikuwa akifanya kazi za kijamii na mitindo kabla ya kupata mchumba raia wa Ufaransa aitwaye Jean Guyeu na alitimkia naye nchini Afrika Kusini. Miaka kumi baadaye, Aina alirejea Bongo na kufunga ndoa na jamaa huyo. Baadaye zilivuja taarifa kuwa alikuwa ni mgonjwa na hadi sasa hali yake bado hajajulikana.

 

EMILY ADOLPH (1995)

Emily alinyakua taji hilo akitokea mkoani Dodoma mwaka 1995. Ni kipindi hicho ndipo shindano hili lilipozidi kuwa na msisimko mkubwa na kuanza kutoa wawakilishi kutoka mikoani.

 

Wakati anatwaa taji hilo, mrembo huyu alikuwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Central mkoani humo. Kulizuka tafran kubwa mpaka kufukuzwa shule, lakini hatimaye baadaye Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) lilitoa kanuni na mwisho akaendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Makongo jijini Dar. Emily anadaiwa kuwa baada ya kufanya shughuli za kijamii aliishia kuwa mfanyabiashara hadi leo.

SHOSE SINARE (1996)

Shose alitokea Mkoa wa Arusha. Naye aliibuka kidedea kwenye Miss Tanzania mwaka huo kisha alikwenda kuwakilisha nchini kwenye Miss World nchini India. Shose ndiye aliyekuwa mrembo wa kwanza kuitisha mkutano wa waandishi wa habari wa kimataifa wakati wa shindano hilo la urembo wa dunia na kuwaeleza jinsi washiriki kutoka nchi za Afrika walivyobaguliwa.

 

Aliporejea nchini, Shose alifanya kazi za kijamii kwa mwaka moja. Alipata nafasi ya kufanya kazi za mitindo nchini Italia kwa muda mrefu na hatimaye alijipatia mchumba na kufunga naye ndoa.

 

Baadaye Shose alirejea nchini ambapo aliajiriwa katika Benki ya Stanbic akiwa Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Uwekezaji. Lakini miaka takriban miwili iliyopita, mrembo huyu alipandishwa kizimbani kwa kosa la kutakatisha fedha na mpaka sasa yuko mahabusu.

SAIDA KESSY (1997)

Saida naye alitokea Mkoa wa Arusha. Kipindi hicho Arusha ilionekana kushika chati katika masuala ya urembo. Baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania, naye aliiwakilisha nchi kwenye Miss World na kuwa kama wengine waliotangulia, kwani hawakuweza kushika nafasi yoyote. Baadaye Saida alifanya kazi za kijamii mwaka mmoja. Hivi sasa anafanya kazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (International Criminal Tribunal for Rwanda, ICTR) iliyopo Arusha. Mwanamama huyu ameolewa na ana watoto wawili.

BASILA MWANUKUZI (1998)

Basila alitokea wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar. Kama kawaida, naye aliiwakilisha nchini yetu kwenye Miss World, lakini bahati haikuwa upande wetu ambapo baada ya kumaliza kazi ya dunia alipata kazi kwenye Kampuni ya Multi Choice na baadaye aliajiriwa kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP). Alifanya kazi nchini Afrika Kusini kisha Ethiopia na sasa yupo nchini Tanzania akiendelea na biashara zake huku akiwa ni Mkurugenzi wa Miss Tanzania. Basila alifunga ndoa hivi karibuni.

HOYCE TEMU (1999)

Mrembo huyu alitokea Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar ambapo aliwakilisha vyema kwenye mashindano ya urembo nchini Uingereza. Aliweza kuitangaza vyema nchini yetu na mpaka kupachikwa jina la mrembo wa Millenium. Baada ya kufanya kazi nyingi za kijamii alikwenda nchini Marekani kusomea Shahada ya Sheria. Aliporejea aliajiriwa na Benki ya Standard Chartered na baadaye Umoja wa Mataifa (UN) ambapo mpaka sasa anafanya kazi. Hoyce ameolewa na ana mtoto mmoja.

JACQUELINE NTUYABALIWE (2000)

Mrembo huyu naye alitokea wilayani Ilala Mkoa wa Dar. Aliiwakilisha vyema nchi kwenye mashindano ya dunia. Aliporejea nchini aliendelea na kazi za kijamii. Kabla ya kushiriki Miss Tanzania, alikuwa akiimba katika Bendi ya Tanzanite kabla ya kuingia kwenye Bongo Fleva.

 

Akiwa staa wa Bongo Fleva, aliachia wimbo wake wa Crazy Over You akitumia a.k.a ya K-Lynn. Baada ya hapo alitoa nyimbo kama mbili na mwisho akaacha kuimba baada ya kuolewa na Mwenyekiti wa Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi. Kwa sasa mwanamama huyu ni mkurugenzi wa kampuni yake ya Amorrete ambayo inatengeneza samani za ndani.

HAPPINESS MAGESE (2001)

Mrembo huyu alitokea wilayani Temeke na kuibuka mshindi na ndiye aliyekuwa mrembo ambaye alitingisha washikiri kutoka barani Afrika kwenye Miss World ambayo ilifanyika nchini Afrika Kusini. Hata mshindi wa Miss World aliyetokea Nigeria, Agbani Darego alikiri kuwa mwanadada huyu ndiye alikuwa tishio lake.

 

Mrembo huyu baada ya kumaliza mwaka wake mmoja alipata kazi kwenye Kampuni ya Mitindo ya Elite nchini Afrika Kusini kisha kuzunguka nchi mbalimbali duniani kabla ya kuhamia Marekani. Baada ya hapo alibadilisha jina na kujiita Millen na bado anaendelea na kazi za unamitindo.

 

ANGELA DAMAS (2002)

Mrembo huyu naye alitokea Wilaya ya Ilala na kuibuka kidedea kwenye shindano la Miss Tanzania. Kama wengine, mrembo huyu aliwakilisha vyema nchi yetu kwenye Miss World iliyofanyika nchini Uingereza. Baada ya kutumikia taji hilo kwa mwaka mmoja, alipata kazi nje ya nchi katika Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP).

SLYVIA BAHAME (2003)

Mrembo huyu yeye alitokea Wilaya ya Temeke. Baada ya kunyakua taji lake la Miss Tanzania aliiwakilisha nchi kwenye mashindano ya urembo wa dunia yaliofanyika Sanya nchini China. Baada ya mwaka wake wa kulitumikia taji hilo, alirudi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea na masomo ya sheria na sasa ni mwanasheria wa kujitegemea.

FARAJA KOTA (2004)

Mrembo huyu naye aliibuka kutoka Wilaya ya Temeke. Aliibuka kidedea katika Miss Tanzania. Akiwa katika harakati ya kugombea taji hilo, alitangazwa kwenye tano bora ya wanafunzi waliofanya vizuri nchini kwenye mtihani wa kidato cha sita.

 

Baada ya kutwaa taji hili, alikwenda kuiwakilisha nchi kwenye Miss World huko Sanya nchini China. Alipomaliza muda wake, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua Shahada ya Sheria. Baadaye aliolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasilia na Utalii, Lazaro Nyalandu na kuzaa naye watoto wawili. Amejiajiri mwenyewe.

NANCY SUMARY (2005)

Kwa takriban miaka 10 Tanzania haikuwahi kufurukuta katika mashindano ya urembo ya dunia, lakini mwaka huo iliweza kupeperusha bendera yake kupitia mrembo huyu ambapo alikuwa ndiyo mrembo wa dunia kwa Bara la Afrika. Alipata mapokezi baabkubwa yaliongozwa na mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Salma Kikwete aliporejra nchini.

 

Alipomaliza mwaka wake, alijiunga na Televisheni ya Star akiwa anatangaza kipindi cha urembo, lakini baadaye aliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi Mkurugenzi wa Mtandao wa Bongo 5, Lucas na baadaye wakaoana na wana mtoto mmoja na mpaka sasa anafanya kazi hapo.

WEMA SEPETU (2006)

Mrembo huyu alinyakua taji hili akitokea Wilaya ya Kinondoni. Baada ya kutwaa taji hili alifanya kazi za kijamii kwa mwaka mmoja kabla ya kujiingiza kwenye tasnia ya sinema za Kibongo. Baadaye alifungua ofisi yake ya Endless Fame inayojihusisha na mambo ya filamu. Hadi sasa anafanya filamu na ndiye mrembo ambaye jina lake halikuwahi kupoa tangu alipoibuka kidedea kwenye Miss Tanzania.

RICHA ADHIA (2007)

Ni mrembo ambaye alileta changamoto kubwa kutokana na rangi yake, lakini alisimamia haki yake kuwa alishinda Miss Tanzania kwa vigezo. Baada ya mwaka mmoja wa kulitumikia taji hilo, Richa alikuwa akipenda mambo ya urembo ambapo alifungua saluni yake iitwayo Beuty Clinic iliyokuwa maeneo ya Mikocheni, Dar. Kwa sasa anaishi nchini Uingereza na familia yake.

 

NASREEN KARIM (2008)

Baada ya kufululiza taji la urembo kwenda Dar, mwaka huo lilienda mkoani Mwanza ambapo Nasreen aliibuka kidedea. Baada ya ushindi aliendelea na masomo ya juu. Alipomaliza aliamua kujiajiri mwenyewe kwa kuanzisha vitu ya urembo wa asili alivyovipa jina la Enjipai ambapo anatengeza shanga, vipochi vya asili na bangili.

 

MIRIAM GERALD (2009)

Mrembo huyu ambaye naye alitokea mkoani Mwanza, baada ya kunyakua taji hilo alidaiwa kutoka kimapenzi na mshindi wa Mr Dar, aliyetambulika kwa jina la Kevin na mpaka sasa inadaiwa ameolewa na mtu mwingine, lakini maisha yake yamekuwa ya kibinafsi zaidi.

 

GENEVIEVE MPANGALA (2010)

Mrembo huyu ambaye alikuwa zao la Temeke, alijinyakuliwa taji hilo ambapo baada ya mwaka mmoja alirudi Chuo Kikuu cha Saint Augustine kilichopo Mwanza. Baada ya kumaliza masomo aliamua kujiingiza kwenye muziki wa Bongo Flava.

 

SALHA ISRAEL (2011)

Salha alinyakuwa taji hilo akitokea Wilaya ya Kinondoni ambapo baada ya kumaliza muda wake wa mwaka mmoja, hakuwa anajishugulisha na kitu, lakini baadae aliolewa na aliyekuwa mume wa video queen Jacqueline Patrick, Abdullatif Fundikira na kuzaa naye mtoto mmoja wa kiume kisha wakaachana.

 

BRIGGITE ALFRED (2012)

Mrembo huyu alinyakua taji hili wakati shindano hili likiwa limeanza kupoa. Baada ya kumaliza muda wa mwaka mmoja, alimalizia masomo yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kisha alikwenda nchini Afrika Kusini ambapo alihitimu masomo yake ya sheria. Kwa sasa ana taasisi yake ya kusaidia walemavu wa ngozi na watoto wengine wenye mazingira magumu.

 

HAPPINESS WATIMWANYA (2013)

Baada ya kunyakua taji hili mrembo huyu hakusikika sana kwani alikuwa siyo mtu wa kujichanganya kabisa hivyo mpaka sasa haijulikani anafanya nini.

 

LILIAN KAMAZIMA (2014/15)

Mrembo huyu alipewa taji hili baada ya mshindi wa shindano hilo, Sitti Mtevu kuvuliwa taji hilo na kupewa yeye ambaye alikuwa mshindi wa pili akitokea mkoani Arusha. Mpaka sasa yupo tu haijulikani kazi ambayo anafanya.

 

DIANA EDWARD (2016)

Mrembo huyu ambaye alitokea Wilaya ya Kinondoni, wakati alipokabidhiwa ushindi huu, watu waliongea mengi juu ya kupewa taji hilo, lakini mwisho wa siku alikwenda kutuwakilisha kwenye Miss World.

 

QUEEN ELIZABETH MAKUNE (2018)

Mrembo huyu ndiye amefunga dimba. Pamoja na kwamba bado yupo kwenye mwaka mmoja wa kufanya mambo ya jamii kwa taji alilolibeba, lakini bado watu hawako na muamko kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

INASIKITISHA! Hoyce Temu Apata PIGO Kubwa

Toa comment