The House of Favourite Newspapers

Maafisa wa Jeshi Wafanya Mapinduzi ya Kuung’oa Utawala wa Kijeshi Nchini Burkina Faso

0
Kapteni wa Jeshi la Burkina Faso Ibrahim Traore akiitangazia nchi kupinduliwa kwa Rais wa Kijeshi wa nchi hiyo Luteni Kanali Paul-Henri Damiba

MAAFISA wa Jeshi wa Burkina Faso wamefanya mapinduzi ya kumtoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Luteni Kanali Paul-Henry Damiba baada ya kushindwa kumaliza mauaji yanayosababishwa na makundi ya kigaidi nchini humo.

 

Aliyefanya mapinduzi hayo ni Afisa wa Jeshi la nchi hiyo Kapteni Ibrahim Traore akiwa na Maafisa wenzake 19, ambaye amesema kuwa Jeshi limefikia maamuzi ya kumtoa madarakani Luteni Kanali Paul-Henri Damiba kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wake wa kumaliza mauaji yanayosababishwa na vikundi vya kigaidi nchini humo.

 

Kumekuwa na taarifa za utekelezwaji wa mauaji nchini humo hasa mengi yakiwalenga Askari wa Jeshi huku ikibainishwa kuwa siku ya Jumatatu jumla ya wanajeshi 11 waliripotiwa kuuawa na wapiganaji wa makundi ya kigaidi wakati wakisindikiza msafara wa magari ya raia.

Rais aliyetolewa madarakani Paul-Henri Damiba

Mara baada tu ya kutangaza kuondolewa madarakani kwa Luteni Kanali Damiba, Kapteni Traore alitumia wasaa huo kutangaza kupitia Televisheni ya Taifa kufunga mipaka yote ya nchi hiyo na kusitisha shughuli zote za kisiasa ndani ya nchi hiyo hadi pale taarifa nyingine itakapotolewa.

 

Mnamo mwezi Januari Luten Kanali Damiba alimtoa madarakani Rais aliyechaguliwa Kidemokrasia Roch Kabore kwa sababu ya kushindwa kutatua mauaji yaliyokuwa yakisababishwa na wapiganaji wa makundi ya kigaidi.

Wanajeshi wamefunga mipaka na maeneo nyeti nchini humo

Nayo Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS imekemea vikali tukio hilo ikidai kuwa ni mwendelezo wa matukio yanayoonesha hali ya kutokuwepo kwa amani na utawala wa kidemokrasia katika taifa hilo.

 

Hadi sasa haifahamiki alipo Luteni Kanali Damiba, wakati huohuo vyombo vya Habari nchini ikiwemo televisheni ya Taifa imepigwa marufuku kutoa Habari yoyote sanjari na hilo usiku wa kuamkia leo imesikika milio ya risasi maeneo ya ikulu huku hali ilyosababisha kutokuwepo kwa amani katika mji mkuu wa nchi hiyo Ougadougou.

 

Taarifa zinadai kuwa asubuhi ya leo mji mzima umetapakaa wanajeshi ambao kwa asilimia kubwa wamekuwa wakifunga baadhi ya barabara na maeneo mengine nyeti.

 

 

Leave A Reply