The House of Favourite Newspapers

MAAJABU MAZITO FUNDI ALALA, AAMKA MLEMAVU

MSEMO wa hujafa hujaumbika una maana kubwa kwenye maisha ya binadamu kutokana na ukweli kwamba hali ya afya aliyonayo mtu inaweza kubadilika wakati wowote, Risasi Mchanganyiko lina kisa chenye maajabu mazito.  

 

Ungejisikiaje pale unapolala usiku ukiwa mzima halafu asubuhi unajaribu kuinuka unajikuta huwezi kutokana na miguu kupooza? Fundi ujenzi Abdul Habib (22), mkazi wa Tegeta Konoike jijini Dar, amefikwa na hali hiyo.

 

Akizungumza na mwanahabari wetu Abdul amesema, Mei 15 mwaka jana, ndiyo alijikuta katika mkasa huo mzito uliozima kabisa ndoto za maisha yake. “Nililala mapema tu, sikuwa na homa wala maumivu yoyote mwilini, alfajili niliamka ili niwahi kazini. “Yaani nilijishangaa kwa nini siwezi kuinuka, nikajitahidi nikawa siwezi, ikabidi nipaze sauti kumuita jirani yangu aje anisaidie kuinuka.

 

“Aliponiinua nikawa siwezi kusimama hapo ndipo nilipogundua kuwa miguu yangu haikuwa na nguvu na kwamba nilikuwa nimepooza kuanzia kiunoni hadi miguuni,” alisema. Aliongeza kuwa, baada ya kuona hivyo ndugu na jamaa walimkimbiza Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Pwani ambako alipimwa vipimo mbalimbali kuangalia presha, malaria, sukari, lakini madaktari hawakugundua tatizo lolote.

 

“Wakatushauri twende Hospitali ya Taifa Muhimbili, nako hawakuona kitu, hapo ndipo nilipozidi kuchanganyiwa,” alisema Abdul. Huku akiwa mwenye huzuni juu ya mkasa wake kijana huyo alisema baada ya vipimo vya kawaida kutoonesha tatizo madaktari walimwambia afanye vipimo vingine vikubwa kama MRI ili kubaini tatizo.

 

Hata hivyo, kutokana na uwezo wa familia kuwa duni Abdul walishindwa kumudu gharama za vipimo na hivyo kuamua kurudi nyumbani ambako anaendelea kuteseka bila kujua hatima ya afya yake. “Kwa kuwa siwezi kufa nimetulia bado nahangaikia afya yangu kwa kutumia dawa za asili ambazo wakati mwingine naona kama zinazidisha tatizo langu.

“Hapa unavyoniona sijiwezi kwa chochote nipo tu, kila kitu nasaidiwa hadi kwenda chooni jambo ambalo sikuwahi kuliwaza katika maisha yangu,” alisema Abdul huku akifuta machozi.

Aliongeza kwa kuwaomba Watanzania wenzake wamsaidie fedha za kugharamia vipimo ili kugundua tatizo na kulitibu kwa imani kuwa huwenda akarejea katika hali yake ya zamani.

 

“Kuna watu wananiambia nifanye mazoezi lakini siwezi, inatakiwa angalau niwe na kibaiskeli lakini sina, zote hizi ni changamoto zinazoninyima raha katika maisha yangu. “Naamini Watanzania wenzangu wakisikia kilio changu watanisaidia kuokoa maisha yangu.

 

“Kwa msamaria atayeguswa na tatizo langu na akapenda kutoa chochote awasiliane na mama yangu mdogo ambaye ndiyo ananiuguza. “Mawasiliano yake ya simu ni 0655 512 222 au 0719 461 896, jina lake anaitwa Mwanaidi Ally. Natanguliza shukrani zangu,” alisema Abdul kwa sauti yenye kuhuzunisha.

STORI: Richard Bukos, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.