visa

MAAJABU UPEPO WAPANDISHA WATANO JUU YA PAA MBEYA

MAAJABU ambayo sayansi yake haijulikani ni ya karne gani yametokea jijini hapa kwa watu watano kwa nyakati tofauti kukumbwa na upepo kisha kutupwa juu ya paa za nyumba kimiujiza.  Matukio hayo kwa mujibu wa mashuhuda yamekuwa yakitokea bila kujali kama kuna mvua, jua au mawingu.

 

MWENYEKITI ASIMULIA

Mwenyekiti wa Mtaa wa Maendeleo, Kata ya Iyunga jijini hapa, Elias Mwakyusa amesema, matukio hayo yamekuwa yakimsononesha. “Ni mambo ya ajabuajabu tu, mimi nawaomba wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo waache mara moja kwani havina tija kwenye jamii,” alisema Mwakyusa kwa hasira.

 

Aliongeza kuwa: “Siwezi kuvumilia, naandaa mkutano wa kijiji ili kukemea kwa nguvu zote vitendo hivi kwani vinadhoofisha maendeleo ya mtaa.” Dodoso za kihabari zimeonesha kuwa watu waliokumbwa na upepo huo wa ajabu wamekuwa wakichukuliwa katika mazingira ya kustaajabisha.

 

MMOJA AELEZA ALIVYOCHUKULIWA

Mbali na wengine wanne ambao mwenyekiti huyo hakuweka bayana matukio yao, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Sekondari ya Maziwa (jina kapuni) ambaye alikumbwa na mkasa huo wa ajabu, Mei 15, mwaka huu aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa: “Nilikuwa najiandaa kwenda shule, nikachukua mswaki na jagi kwa ajili ya kwenda kupiga mswaki.

 

“Nikiwa bombani nilishtukia upepo mkali ukaja eneo nililokuwepo, ukaanza kunivuta kama nabebwa na mtu. “Nikaanza kupiga kelele lakini sikuweza kujiokoa, upepo ukaenda kunitupa juu ya paa ambako niliendelea kupiga kelele kuomba msaada.”

 

KILICHOTOKEA BAADAYE

Mwanafunzi huyo anaeleza kuwa hakutambua alifikaje huko na hatua gani za kujiokoa lakini anakumbuka alimuona mama yake akiwa chini ambapo alianza kumuita. “Wakati namuita ndiyo ghafla nikasikia ile nguvu iliyokuwa inanishikilia huko juu imeniachia, nikaaza kuteleza kuja chini,” alisimulia mwanafunzi huyo huku akifuta machozi.

 

HUYU HAPA MAMA MZAZI

Naye mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Scolla Alex alimwambia mwandishi wetu kuwa, wakati tukio la ajabu likimkumba mwanaye, alikuwa ndani lakini alishtushwa na kishindo alichokisikia juu ya paa la nyumba yao.

 

“Nilishtushwa na kile kishindo lakini baadaye nikasikia kelele, nilipotoka nje nikamkuta mwanangu yuko juu ya paa kashikilia jagi na mswaki mkononi. “Nikashangaa kafikaje huko, nikajua hizi ni nguvu za giza, nikaaza kuomba Mungu, ndipo mtoto akadondoka na kuvunjika mguu kama hivi unavyomuona amefunga ogo ‘plasta ngumu’,” alisema mama wa mwanafunzi huyo.

 

MATUKIO YASHAGAZA WENGI

Aidha, baadhi ya wakazi wa kata hiyo ya Iyunga walieleza kustaajabishwa kwao na matukio hayo yanayoaminika kuwa ni ya imani ya kishirikina, kuendelea kushamiri katika eneo lao. “Kuna watu wanapandishwa kwenye paa mpaka unajiuliza wanawezaje kufika huko juu bila ngazi?” Bombaga Kitwika mkazi wa Iyunga alionesha hali ya kushangazwa na vitendo hivyo.

 

Naye Sophia Mwakabenga ambaye ni shangazi wa mwanafunzi aliyekumbwa na mkasa huo mzito alisema: “Inashangaza sana.” Kwa upande wake Anna Ngairo mkazi wa eneo hilo aliwaomba wakazi wenzake kuwa na imani na Mungu na kuachana na mambo ya kishirikina.

 

DIWANI AFUNGUKA

Diwani wa Kata ya Iyunga, Mchungaji Daud Kalinga, alisema vitendo kama hivyo vinapaswa kutokomezwa mapema kwani vinadumaza maendeleo ya watu. “Kwanza nawaomba wananchi waishi kwa kumtegemea Mungu, hivi vitendo vya kishirikina havina msaada katika maisha yetu kwa sasa,” alisema diwani huyo huku akionesha kushangazwa na baadhi ya watu kuishi kwa kuamini ushirikina katika zama hizi za maendeleo ya kisayansi.

 

RAI YA DAWATI

Dawati la Ijumaa Wikienda linawaomba wakazi wa Iyunga na kwingineko nchini kupuuza matukio yote ya kishirikina kwa vile hayasaidii chochote katika maisha zaidi ya kudumaza watu kiakili na kimaedeleo.

 

Aidha, uchunguzi unaonesha kuwa maeneo mengi ambayo wananchi wake wanaishi kwa kuamini imani za kishirikina ndiko kwenye matatizo makubwa ya kimaisha ukiwemo umasikini wa kutupwa, hali inayotafsiri kuwa ushirikina ni matendo ya giza yaliyopitwa na wakati.
Toa comment