MAAJABU YA KAROTI KATIKA KUTIBU MACHO

MATATIZO mengi yanayowapata wana jamii ya leo hii kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na ulaji usiokuwa mzuri na kutozingatia kanuni bora za afya.  Watu wengi wamekuwa wakila kwa mazoea kwa maana ya milo mitatu kwa siku lakini linapokuja suala la mlo gani alioupata mtu husika; ndipo penye tatizo na huzalisha matatizo mengi ya kiafya kwa binadamu.

Mtu anaweza kumaliza siku nzima bila kugusa hata kipande cha tunda au kunywa juisi ya tunda au kirutubisho cha mwili kama karoti. Kitaalamu ni kwamba matunda yana virutubisho vingi mwilini na iwapo yatazingatiwa huwa ni kinga na tiba ya maradhi mbalimbali.

Karoti watu wengi wanaifahamu kama kiungo cha mboga lakini ni lazima tutambue kuwa karoti ni mzizi wenye manufaa kwa binadamu. Karoti kuna watu wanasema ni tunda lakini ukweli ni kwamba ipo kwenye jamii ya mizizi inayoliwa kama kilivyo kiazi au muhogo ama ming’oko. Licha ya kuitumia kama kiungo katika chakula, karoti pia unaweza kuitumia kwa kuitafuna au kuisaga na kunywa juisi yake tena bila kuongeza sukari.

Karoti ina protini kidogo na haina mafuta kama yalivyo baadhi ya matunda tunayoyala. Pia ina asili ya wanga na ni chanzo kizuri cha vitamini B, C na E. Aidha karoti ina madini mengi ikiwemo madini ya chuma. Kuna kitu kinaitwa beta – rotene ambayo imo ndani ya karoti, hii ikiingia mwilini inabadilishwa na kuwa vitamini A.

Vilevile karoti ina kirutubisho kinachoitwa fiber ambacho ni muhimu kwa kukinga kuta za utumbo wakati wa mmeng’enyo wa chakula. Karoti inasaidia kupambana na magonjwa mbalimbali mwilini.

Moja ya kazi yake mwilini karoti ni kukinga na kuponya magonjwa kama macho hasa kama yana tatizo la kutoona gizani au kwenye mwanga hafifu. Ukitumia karoti kila siku tatizo hilo litakwisha. Pia karoti  huifanya ngozi kuwa nyororo, hupunguza tindikali inayodhuru tumboni na kukinga magonjwa yenye asili ya kansa tumboni.

Karoti inaweza kuliwa kwa namna mbalimbali kama vile, ikiwa mbichi kwa kutafuna, inaweza kupikwa na kuchanganywa na mbogamboga nyingine wakati wa mapishi ya mboga jikoni. Karoti pia inaweza kusagwa na kupata juisi ambayo pia inaweza kuchanganywa na juisi nyingine ili kupata ladha tofauti japokuwa hata ikiwa yenyewe tu, haina tatizo.

Aidha wengine hukatakata karoti na kuchanganywa kwenye saladi ya matunda na mbogamboga, hivyo kuwa moja ya saladi nzuri na tamu. Machicha ya karoti iliyosagwa yanaweza kutumika kama dawa kukinga ama kuponya maradhi ya nje ya mwili kama vile kidonda au vipele. Anza sasa kula karoti kwa afya ya macho yako kama tulivyoona hapo juu.


Loading...

Toa comment