The House of Favourite Newspapers

Maalim Seif: Hii Ndiyo Siri Yangu na Karume -02

0
Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli (kulia) akifanya mahojiano na Maalim Seif Sharif. Picha na Amani Madebe.

WIKI iliyopita aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na sasa ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi alieleza mengi kuhusu chama chake na mambo mengine ya nchi alipohojiwa na safu hii pamoja na Global TV Online, endelea kusoma mahojiano hayo:

Swali: CUF mnadai mlidhulumiwa ushindi wetu kiti cha urais na hata kwenye baraza la uwakilishi, je, kuna matumaini yoyote ya kurudishiwa haki hiyo mnayoidai?

Jibu: Tumefanya juhudi kubwa kuuambia ulimwengu jinsi CCM ilivyotudhulumu ushindi wetu. Nilikwenda Umoja wa Mataifa nikaonana na naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia siasa, nikaenda nchi za Ulaya nimewaonesha ushahidi wote ndiyo maana baadhi ya misaada wameacha kutoa kwa serikali.

Swali: Unadhani nani wa kulaumiwa kwenye mgogoro huo wa uchaguzi?

Jibu: Ni Rais Jakaya Kikwete. Yeye ndiye aliyeamuru majeshi kuja Zanzibar ili kuhakikisha wanatupokonya ushindi, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha aliamriwa tu akafanya aliyoyafanya, lakini hapa aliyetumia ubabe ni Kikwete.

Rais wa Zanzibar na sasa ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi.

Swali: Dk. Wilbroad Slaa aliondoka Chadema kwa sababu ya kutokubaliana na namna Ukawa mlivyompokea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kama kiongozi wa upinzani ndani ya Ukawa, unafi kiri Ukawa inammisi Dk. Slaa?

Jibu: Hatum-misi kwa sababu aliondoka na vyama vinaendelea bila yeye.

Swali: Unadhani nini kilimuondoa Ukawa, ni Lowassa tu?

Jibu: Kifupi, kilichomuondoa Dk. Slaa ni kwamba alitaka yeye ndiye awe mgombea urais, angechaguliwa yeye asingeondoka hata kama Lowassa angekuwepo, lakini baada ya makubaliano yetu kwamba awe Lowassa, akaondoka.

Swali: Kama ungetakiwa kutoa alama za ufanyaji kazi wa serikali ya awamu ya tano kwa manufaa ya taifa, ungetoa alama ngapi?

Jibu: Mimi nilikuwa mwalimu wa kufundisha watu darasani, kwa serikali hii ya awamu ya tano ningeipa asilimia 39 tu tena basi kutokana na kupambana na rushwa. Serikali ilianza vizuri sana lakini baadaye ikafeli mambo mengi ya msingi, yaani mambo ya uchumi kwani sasa hivi wananchi wanaishi kwa shida sana, wengi hata mlo mmoja imekuwa shida kuupata.

Kodi zimekuwa kubwa, hali hiyo imefanya biashara nyingi kufa, wafanyabiashara wamefunga, serikali inakosa mapato lakini wananchi pia wanakosa kazi. Hili serikali iliangalie.

Swali: Hali ya kisiasa kwa upande wa vyama vya siasa nchini inaridhisha? Kama hairidhishi nini kifanyike?

Jibu: Hairidhishi hata kidogo, mheshimiwa rais amepiga marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa lakini yeye anafanya. Mtindo huo ni kinyume cha katiba ya nchi, mheshimiwa anavunja katiba inayoruhusu vyama vya siasa na mikutano ya hadhara.

Swali: Kulikuwa na madai kwamba kuna baadhi ya viongozi wa siasa wanataka kuwepo serikali moja badala ya tatu kama inavyopendekezwa, unazungumziaje hilo?

Jibu: Suala la kutoka serikali mbili kwenda serikali moja hilo halitakubalika. Mimi silikubali. CUF hailikubali, na Mzanzibari mzalendo yeyote halikubali. Siamini kuwa Serikali ya Muungano itakuwa tayari kutumia vifaru, mizinga na madege ya kivita kulazimisha muundo wa serikali moja.

Swali: Inadaiwa Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe alitaka kuwepo kwa serikali tatu, wewe ulikuwa karibu naye, unazungumziaje hilo? Jibu: Kwamba mzee Aboud Jumbe alituhumiwa kutaka kuwepo kwa muundo wa Muungano wa serikali tatu na akalazimishwa kujiuzulu. Wakati huo mimi nilitetea muundo wa sasa wa serikali mbili. Ili hili lifahamike vyema na wananchi ni vyema kwanza kuelezea mazingira yaliyomfi kisha mzee Aboud Jumbe kujiuzulu.

Nitangulie kueleza kuwa binafsi na kwa dhati ya nafsi yangu nilikuwa namheshimu na kumthamini sana mzee Aboud Jumbe. Kwanza ni mwalimu wangu nilipokuwa nasoma katika skuli ambayo wakati huo ikiitwa The King George VI Secondary School (sasa Lumumba College).

Pili, ni mzee Jumbe ndiye ambaye alisababisha mimi kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara baada ya yeye kuwa Rais wa Zanzibar mwaka 1972, baada ya kukaa kwa miaka minane tangu nilipomaliza masomo ya kidatu cha sita (Form VI) hapo 1963 na kuzuiwa na Serikali ya Mapinduzi kujiunga na masomo ya chuo kikuu, pamoja na kuwa kila mwaka nilikuwa napata nafasi katika vyuo mbalimbali duniani.

Tatu ni mzee Jumbe huyo huyo alisababisha mimi kuwa kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi na kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM. Hivyo namshukuru na katu siwezi kumsahau kwa mchango wake mkubwa ulionifanya niwe nilivyo.

Sasa nirejee kuelezea mazingira ya wakati huo ambayo yalikuwa kama ifuatavyo; nianzie mwaka 1982 ambapo kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa CCM.

Katika kipindi kilichotangulia Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM wa 1982 wa kuchagua viongozi wa kitaifa, kulijitokeza makundi mawili miongoni mwa

viongozi wa CCM kutoka Zanzibar yaliyokuwa yakikinzana. Kundi la kwanza likijulikana kama Liberators, na la pili likijulikana kama Frontliners. Kundi la Liberators kimsingi lilikuwa na viongozi ambao walikuwa wanapinga mabadiliko ya aina yoyote yale katika uendeshaji wa mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Zanzibar.

Swali: Kundi hilo kwa lugha rahisi tungeweza kuwaitaje?

Jibu:  Kwa lugha ya sasa unaweza ukaliita kundi la Wahafi dhina. Kundi la Frontliners lilikuwa na vijana, damu mpya iliyoingia katika uongozi wa Chama na SMZ. Kundi hili lilitaka mabadiliko katika uendeshaji wa mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Unaweza ukaliita kundi la Reformers. Uchaguzi wa viongozi wa kitaifa (Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa- NEC) wa 1982 ulishuhudia msuguano mkali kati ya makundi hayo mawili. Nia ya Liberators ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Frontliners hawaingii katika Halmashauri Kuu ya Taifa.

Nia ya Frontliners ilikuwa ni kuhakikisha damu mpya inaingia katika kikao hicho kikuu cha maamuzi cha chama ambacho wakati huo kilikuwa ndiyo kimeshika hatamu zote za uongozi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bahati njema Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, kwa busara zake, uliwaingiza watu kutoka makundi yote mawili katika NEC na baadaye NEC ikawaingiza watu kutoka makundi yote mawili katika Kamati Kuu. Frontliners walishukuru kuona kuwa miongoni mwao walifanikiwa kuchaguliwa kuingia katika vikao vyote viwili vikuu vya maamuzi vya chama. Itaendelea wiki ijayo.

STORI: ELVAN STAMBULI | UWAZI JUNI 20 | MAKALA

Leave A Reply