The House of Favourite Newspapers

Maambukizi katika njia ya mkojo (UTI)-3

0

symptoms-of-utiWiki iliyopita niliahidi kuelezea dalili za UTI  na tiba yake, ungana nami sasa:

DALILI ZA UTI

Baadhi ya dalili za mtu kuambukizwa bakteria katika njia ya mkojo, kubwa ni maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na kuwa na harufu kali, japokuwa siyo kila mwenye dalili hizo ana maambukizi katika njia ya mkojo.

Dalili nyingine za UTI ni maumivu, kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa ukiambatana na maumivu na kuhisi moto wakati mkojo ukitoka. Baadhi ya wanaume wakati mwingine, hutokwa na majimaji katika njia ya mkojo wakati wa kujisaidia haja kubwa. Wengine wenye maambukizi hujikuta wakipata vichomi katika njia ya mkojo au kuhisi kuwashwa sehemu hiyo, kuumwa kiuno au tumbo na kadhalika.

Mgonjwa anaweza pia kukumbwa na homa kali mara kwa mara na mwili kuwa mchovu. Kwa watoto hupoteza hamu ya kula na mwili huonesha kuchoka.

Wagonjwa wengine hupata maumivu kwenye kibofu cha mkojo ambapo husikia maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu na huwa hayaishi.

Matatizo haya ya mfumo wa mkojo kama tulivyoona kabla, huwapata watu wote, wanawake na wanaume. Watu wenye matatizo haya kila wakipima huambiwa wana UTI.

 Kwa wanaume huhisi hata nguvu za kiume kupungua na wanawake hupoteza hamu ya tendo la ndoa.

Kwa wajawazito, ugonjwa huu unaweza kuhatarisha maisha yao na mtoto aliye tumboni.

Bakteria wanaweza kuingilia mfumo wa damu na kusababisha madhara mengine kama vile shinikizo la damu kuwa kubwa kwenye figo na hata kusababisha ufanyaji kazi mbovu wa figo.

TIBA YAKE

Maambukizi katika njia ya mkojo hutibika kwa dawa mbalimbali za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitika kuwa mgonjwa ana maambukizi hayo. Dawa ambazo anaweza kupewa ni kama vile Ciprofloxacin, Monurol, Furadantin, Sulfam Ethoxazole, Co-trimax, Ampicillin, Gentamicin na kadhalika. Mgonjwa anayesumbuliwa na UTI hapaswi kutumia dawa yoyote bila kwanza kupata ushauri wa daktari.

USHAURI

Wanawake wanashauriwa kuepuka kujisafisha sehemu za siri na maji machafu na yasiyo salama. Pia kuepeuka kupaka marashi sehemu hizo au kutumia pamba zenye kemikali ya kukata harufu kwani hizo huua bakteria wa asili wa ukeni hali ambayo hukaribisha bakteria wa maradhi kuzaliana kwa wingi.

Pia wanashauriwa wanapojisafisha baada ya kujisaidia kuanzia mbele kwenda nyuma, ili kuepusha kuhamisha bakteria walio eneo la haja kubwa. 

MWISHO.

Leave A Reply