MAANDALIZI UJIO WAKE, MSHTUKO NYUMBANI KWA LISSU DAR

NI mshtuko wa aina yake! Wakati Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu akisubiriwa arejee nchini; nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam, kumefanyiwa ukarabati mkubwa ambao umewashangaza wengi, Risasi Jumamosi limefika na kushuhudia! 

 

Kwa takriban wiki na ushee sasa, Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii baada ya Spika Job Ndugai kutangaza kumvua ubunge wake kwa kutokidhi matakwa ya sheria za bunge.

 

Mara baada ya tukio hilo, Lissu alifunguka mengi ambapo pamoja na mambo mengine, alisisitiza juu ya msimamo wake wa kurejea nchini Septemba 7, mwaka huu, tarehe ambayo mwaka juzi alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

HIKI HAPA CHANZO

Baada ya msisitizo huo kutawala, chanzo kimoja kililitonya Risasi Jumamosi kuhusu mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanyika nyumbani kwake kuashiria ujio wake unaweza kuwa kweli.

 

“Njooni wenyewe muone, nyumba ya Lissu imebadilishwa kabisa. Sikupita mtaa huu kama mwezi mmoja lakini nilipopita juzi nimeshangaa. “Yaani pamefungwa nyaya maalum za umeme kwenye ukuta, wamebadilisha geti ambapo lile la awali lilikuwa na matundu kiasi cha mtu kuweza kuona ndani lakini sasa huwezi kuona.

 

“Kule ndani nasikia wanafunga kamera za kisasa kwa ajili ya kuimarisha zaidi ulinzi. Yaani mambo ni moto, nyumba inakarabatiwa, kule ndani majani yamekatwa na kumefanyiwa usafi wa hali ya juu na kupigwa rangi mpya,” kilieleza chanzo hicho.

RISASI LATINGA NYUMBANI WA LISSU

Risasi Jumamosi baada ya kushibishwa taarifa hiyo, lilifunga safari hadi nyumbani kwa mbunge huyo na kushuhudia ukarabati wa nyumba yake ukiwa ni wa hali ya juu sawa na mambo yaliyoelezwa awali na chanzo chetu.

MAJIRANI WANENA

Baada ya kugonga geti na kutofunguliwa katika nyumba hiyo ya Lissu, wanahabari wetu waliweza kuzungumza na majirani ambao walielezea mabadiliko hayo huku pia wakionesha hisia za furaha kwani wanaamini jirani yao (Lissu) anarejea.

 

“Mimi ni jirani yake hapa nyumbani, kiukweli tulifurahi sana baada ya kuona mafundi wanakuja kurekebisha hapa na kwa vile yeye mwenyewe (Lissu) alishatangaza kuwa anarudi, tunaamini kabisa haya marekebisho ya nyumba yake yanaashiria ujio wake huo,” alisema jirani aliyejitambulisha kwa jina la mzee Petro.

MWINGINE AMUOMBEA

Jirani mwingine ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini naye alisema anaamini ukarabati huo mkubwa unafanyika kwa sababu Lissu anarejea na anamuombea kwa Mungu afike salama. “Kwa kuwa tunaona makazi yake yanarekebishwa basi anakuja kweli maana wengi tulikuwa hatuamini kama anaweza kurejea.”

 

KAKA WA LISSU ANASEMAJE?

Jitihada za kumpata kaka wa Lissu, Alute Mughwai ili kuzungumzia mabadiliko hayo na maandalizi ya kumpokea Lissu kwa ujumla hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutopatikana hewani hadi tunakwenda mitamboni, lakini mmoja kati ya watu wa karibu na familia ya Lissu alisema: “Ataachaje kuja nyumbani kwake, Lissu ni Mtanzania ana haki ya kuishi hapa kama raia wengine.”

TUJIKUMBUSHE

Lissu amekaa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana eneo Area D jijini Dodoma yalipo pia makazi yake, muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha bunge.

 

Kwa kipindi chote hicho, alikuwa akipatiwa matibabu ambapo awali alilazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kabla ya kuhamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi. Juni 29, mwaka huu Spika Ndugai alitangaza kumvua ubunge wake kwa kutaja sababu mbili ambazo ni kutoonekana bungeni bila spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya maadili.


Loading...

Toa comment