The House of Favourite Newspapers

MABADILIKO KATIKA MFUMO WA HOMONI ZA UZAZI ZA MWANAMKE

0

HOMONI kwa kitaalamu huandikwa Hormone, ni kemikali zinazochochea mifumo ya mwili ifanye kazi yake inavyotakiwa. Vichocheo hivi vipo vingi na vya aina tofauti, lakini katika makala yetu leo tunazungumzia vichocheo vinavyohusiana na mfumo wa uzazi wa mwanamke.

 

Homoni kwa jumla hufanya kazi kwa mawasiliano maalumu yanayosimamiwa na kiungo kiitwacho Hypothalamus kinachopatikana katika tezi ya Pituitary iliyo kichwani.

Sehemu hii upande wake wa mbele huzalisha vichocheo vinavyoitwa Gonodotropin Releasing Hormone ambazo huwa na kazi ya kuzisimamia homoni za Luitenizing Hormone au LH na Folicle Stimulating Hormone au FSH.

 

Kazi ya vichocheo vya LH ni kuamsha upevushaji wa mayai na kumfanya mwanamke apate Ovulation na kunasa ujauzito, pia zina kazi kubwa ya kuamsha vichocheo vya kike au homoni za kike ziitwazo Estradiol na Projesterone kutoka katika vifuko vya mayai au Ovaries na kumfanya mwanamke aonekane kijana, mwenye nguvu na mrembo, pia zinamfanya mwanamke afurahie tendo la ndoa, awe na msisimko na uwezo wa kushika mimba.

 

Vichocheo vinapotolewa huzunguka katika mfumo wa damu na huishia katika uhamasishaji wa kukuza na kuboresha viungo vya uzazi katika maziwa, kizazi na uke. Vichocheo hivi pia humsaidia mwanamke wakati wa tendo la ndoa, apate majimaji na asiwe mkavu ukeni, husaidia kupata ute wa uzazi kila anapopata Ovulesheni au upevushaji mayai.

 

KUVUNJA UNGO

Kuvunja ungo kwa msichana ni hatua ya balehe pale inapotimia ndipo hupata damu yake ya kwanza ya mwezi. Balehe ni kipindi cha mfululizo wa mabadiliko mengi mwilini ya vichocheo mbalimbali na hasa vya uzazi.

 

Mwenendo huu huanzia kwenye ubongo katika Hypothalamus na huendelea katika sehemu ya mbele ya Pituitary na kuamsha vichocheo vya LH, FSH, Estradiol na Progesterone ndipo sasa kama tulivyoona hapo awali jinsi vinavyofanya kazi na kumuona huyu binti anakuwa msichana mkubwa.

 

Wakati wa balehe au karibia ya kuvunja ungo, maumbile ya mtoto wa kike huanza kubadilika na hii hutokea katika umri wa kati ambao kitaalamu tunaita Adolescence Period, ni kati ya miaka kumi na mbili hadi kumi na tano. Hapa maziwa yanachomoza na kuwa makubwa na uotaji wa nywele sehemu za siri na kwapani huanza. Damu ya kwanza ya hedhi hutokea miaka miwili tangu maziwa yaanze kuchomoza.

 

Nyonga hutanuka na mafuta na nyama hujaa kwenye nyonga, kiunoni na katika makalio. Hadi sasa bado hakijulikani ni kitu gani hasa kina amsha balehe kwa mtoto wa kike bado hakipo wazi kisayansi katika umri inapoanza, lakini kadiri mabadiliko yanapoendelea kutokea ndipo vichocheo vingine zaidi vinapozidi kutoka na kuendelea kumbadilisha mwili.

Uotaji wa vinyweleo husababishwa na vichocheo vya Adrenal Androgens Dehydroepiandrosterone Sulphate au kwa kifupi DHEA.

 

MABADILIKO KATIKA VIFUKAO VYA MAYAI

Kwa kawaida mtoto wa kike anapozaliwa tayari anakuwa na mayai na hupungua taratibu, kwani huwa mengi sana hadi anapovunja ungo ndipo mayai hayo huanza kukomaa na kupevuka. Mayai yanapopevuka ndipo mwanamke anapoanza kupata ujauzito. Mfumo wa hedhi unapoanza huwa unaendelea kila mwezi kutokana na mabadiliko katika mfumo wa homoni unavyoendelea.

 

Hili la mfumo wa hedhi tutakuja kuliona kwa undani katika makala zijazo. Katika mfumo mzima wa hedhi tuna vipindi vikuu vitatu ambavyo ni Follicular Phase hiki ni kipindi ambacho mayai yanakuwa ambayo tayari yameshaandaliwa katika ovari kwa kushirikiana na vichocheo vya LH, FSH, Estradiolna Progesterone vyote hivi huwa kwa kiasi kidogo kipindi hiki huwa hakina muda maalumu.

 

Kipindi cha pili ni Ovulatory Phase, hiki ni kipindi cha upevushaji wa mayai ambayo tayari yamekuwa baada ya kuandaliwa, kichocheo cha Estradiol huwa juu sana na Progesterone, huongezeka kidogo na kumfanya mwanamke apate ute wa uzazi na hamu ya tendo la ndoa inaongezeka LH huongezeka sana hasa kati ya saa 36 hadi 48 na huku homoni ya FSH ikiongezeka taratibu.

 

Kiwango cha LH kinaongezeka kutokana na kupanda sana kiwango cha Estradiol hivyo inasukuma au kuamsha LH. Wakati huohuo LH ikianza kupanda na kuwa juu. Homoni ya Progesterone nayo hupanda taratibu na kusababisha vifuko vya mayai vipasuke na yai lianze kutoka likiwa tayari limekomaa. Tangu kifuko cha mayai kinapoanza kupasuka hadi yai linatoka huchukuwa masaa 16 hadi 32.

 

KIPINDI BAADA YA UPEVUSHAJI

Kipindi hiki huitwa Luteal Phase ambapo vifuko vya mayai baada ya kumaliza upevushaji hubadilika na kuwa Corpus Luteum, kipindi hiki kina wastani wa siku 14 ambazo hazibadiliki na hutoa vichocheo vya Progesterone na huongezeka zaidi baada ya kipindi cha Ovulation kupita.

 

Vichocheo hivi vya Progesterone vinakuwa juu husababisha tabaka la ndani la kizazi kubadilika na kuanza kutengeneza mazingira ya kupokea mimba, wakati huu joto la mwili la mwanamke huongezeka kwa nyuzi 0.5 ya joto la kawaida la mwili kwa sababu ya ongezeko la Homone ya Progesterone.

Kipindi ambacho homoni hizi zinakuwa juu, homoni za FSH na LH zinashuka kiwango chake. Endapo mimba itatungwa na kujikita katika mji wa mimba Corpus Luteum itaendelea kuwepo kwa muda mrefu huku ikiendelea kutoa Progesterone.

Itaendelea wiki ijayo.

 

DK. CHALE

SIMU: +255 713 350 084

Leave A Reply