Mabilionea Wasio na Huruma 41

gold-bullion-and-dollars-660x330WAPELELEZI wa Scotland Yard, CIA na Interpol wakiongozwa na Inspekta Masala, wanatua juu ya jengo la Hospitali ya Thailand Cosmetic and Plastic Surgery Center na helikopta ikaondoka zake, kishindo kikubwa kikasikika na kufanya watu wote waliokuwemo ndani kupatwa na mshtuko, kazi ya wapelelezi hao haikuwa nyingine, isipokuwa kuhakikisha wanawakamata Dk Viola na pacha wake Vanessa.

Wanaingia ndani ya chumba cha upasuaji, huko wanakutana na Dk Jeremy Ho ambaye anashangazwa na ujio huo akiwauliza ni kwa nini waliingia chumbani hapo bila kusugua mikono yao na kuvaa mavazi maalum. Baada ya maswali kadhaa na kutopata ushirikiano kutoka kwa Dk Ho, daktari huyo anawataka watoke haraka ndani ya chumba hicho na kama walihitaji msaada wake basi wasubiri mapokezi ambako angeungana nao muda mfupi ujao.

Inspekta Masala anatoa amri kwamba watoke na kuanza kukagua chumba kimoja kimoja ili kuwaangalia wahalifu waliowafuata hapo, walipitia vyumba vyote lakini hawakubahatika kuwaona, Inspekta Masala akachanganyikiwa kabisa, hakuwahi kukutana na wanawake wajanja kiasi hicho maishani mwake.

Upande wa pili wa hadithi hii nchini Tanzania wameingia wawekezaji wawili bwana Lin Chu na John Hui raia wa Thailand, wamewasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na kupokewa na Waziri wa Utalii na Biashara wa Serikali ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Jamhuri Azimio na Katibu Mkuu wake Teofil Ezekia na viongozi mbalimbali.

Baada ya salamu, wanapanda kwenye magari maalum safari kuelekea Ikulu ya Magogoni ambako wangekula chakula cha mchana na rais, inaanza.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…

MAZUNGUMZO ya hapa na pale yaliendelea, wote wakionekana kufurahia ujio wa wageni hao na hatimaye dakika kumi na tano tu baadaye, tayari walishawasili ndani ya ngome ya Ikulu na kupokewa kwa heshima kubwa.

Kama ilivyotokea uwanja wa ndege wakati wakitua, ndivyo ilivyotokea pia Ikulu, zuria la rangi nyekundu lilitandikwa pamoja na maua mazuri yalipambwa kila mahali kuonyesha furaha waliyokuwa nayo viongozi wote wa Tanzania, Bwana Lin Chu na John Hui wakashuka na kupokewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akionyesha furaha ya ajabu.

Baada tu ya kushuka na kukanyaga zuria maalum lililoandaliwa maalum kwa ajili yao, wimbo maalum ukapigwa ukiongozwa na bendi ya Brass Band ambayo ilitumbuiza na kuwafanya bwana Chu na Hui kufurahia huku wakipiga makofi kuonyesha furaha yao.

Wimbo ulipokwisha, rais akachukua jukumu la kuongoza wageni wake sehemu maalum iliyokuwa imeandaliwa na kuwakaribisha waketi wakisubiri kuongea na waandishi pamoja na wageni mbalimbali kisha kupata chakula cha mchana na kuwaruhusu kwenda kupumzika hotelini.

Dakika kumi tu baadaye, tayari mambo yote yalikuwa yakienda kama ilivyopangwa, rais akafungua mkutano kwa kuwatambulisha wageni ambao walipokelewa kwa makofi, muda wote huo wakati hayo yakiendelea, bwana Chu na Hui walikuwa kimya kabisa kwa kuwaangalia ni kama vile walikuwa wakitafakari jambo fulani ndani ya vichwa vyao.

Baada ya rais kuhutubia na kumaliza, ikafika wakati wa wageni nao kuzungumzia kilichokuwa kimewaleta Tanzania na jinsi ambavyo uwekezaji huo ungesaidia sana kupandisha uchumi wa Tanzania hasa ukiangalia kwamba nchi yetu ilikuwa ikipigana kufa na kupona kuhakikisha uchumi wake unapanda kwa kasi.

Waliongea mambo mengi wakijaribu kuwashawishi wananchi wa Tanzania kukubaliana na uwekezaji katika Kisiwa cha Bongoyo na kwamba wangehakikisha uchumi unapanda kwa kasi na kisiwa hicho kingeleta sifa kubwa sana kwa wageni na watalii mbalimbali ambao wangefika nchini na kukitembelea, wananchi wote wakaonekana kuwaunga mkono, wakiwatakia kila la kheri katika uwekezaji huo, aliongea bwana Chu pembeni yake akiwa amesimama Hui ambaye alionekana kutingisha kichwa ishara ya kumuunga mwenzake mkono.

Baada ya hotuba hiyo kukamilika, ilifuatiwa na maswali mengi kutoka kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali na kujibiwa bila kipingamizi, jambo lililozidi kuwatia hamasa zaidi Watanzania wote, wakaonekana kukubaliana na uwezekezaji wa wageni hao kutoka Thailand.

Mkutano ukamalizika na watu wengine wote kusambaa kurejea katika sehemu zao, rais na wageni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na viongozi wengine wakaingia ndani kwa ajili ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na rais akiwa ndiye mwongozaji wao.

Kwa sababu ya uchovu waliokuwa nao wageni hao wawekezaji, walilazimika kupeleka mambo harakaharaka, chakula kikaliwa huku wakiongea mawili matatu na hatimaye wakamaliza na wageni wakatakiwa kwenye hotelini kupumzika, rais akaomba tena kukutana nao jioni kwa ajili ya mkutano wa Dhifa ya Kitaifa ambayo aliamini kabisa ingesaidia sana kwa wawekezaji hao ambao walikuwa wamekuja nchini Tanzania kuwekeza na kuinua uchumi ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa vijana wengi wasiokuwa na kazi. Alitaka viongozi wa serikali, dini na matajiri mbalimbali wa Tanzania wafahamu ujio huo kwa taifa, ambao aliamini kwa asilimia mia moja kwamba kwa uwekezaji huo, Tanzania ingepiga hatua kubwa kiuchumi.

Bwana Chu na Hui wakaagwa na kutolewa mpaka nje ambako walikuta gari likiwasubiri, safari kuelekea Hoteli ya Serena ikaanza, huko wangepumzika mpaka jioni ambako wangekutana tena ikulu kwa ajili ya Dhifa ambayo iliandaliwa na rais wa nchi.

***
Ulikuwa ni mchezo hatari kupindukia, hata wao wenyewe walioucheza hawakufikiria kama zoezi lingekwenda kama ilivyotakiwa, baada tu ya kufanyiwa upasuaji wa kubadilishwa sura zao kuonekana kama wazee, kwao ilikuwa ni ushindi tosha, jambo moja tu lilibaki, wangetokaje nchini Thailand na kurejea Afrika ambako wangeendelea na maisha huku wakitumbua utajiri bila kugundulika?
Kwa msemo wa siku hizi walicheza karata dume.

Dk Viola na pacha wake, Vanessa walifahamu kabisa kwamba ni lazima dunia nzima ingekuwa ikiwasaka, hivyo walitakiwa kutumia akili za kuzaliwa ili kukimbia mkono wa sheria, hivyo walipotoka Hospitali ya Thailand Cosmetic and Plastic Surgery Center, walitumia gari la wagonjwa ambalo walilipia na kuomba liwapeleke hotelini, walishuhudia helikopta ikiwa juu ya paa la hospitali, wakiwa njiani pia kupitia madirisha ya vioo yaliyokuwepo kwenye gari la wagonjwa, walishuhudia magari mawili yaliyobeba polisi waliokuwa na silaha za kutosha, yakielekea hospitali.

“Ha! Haa! Wamekwisha,” aliongea Vanessa karibu kabisa na sikio la Dk Viola ili kuficha uhalisia wao.
“Ni kweli lakini hivi mpaka lini?”
“Tukifanikiwa kuondoka hapa Thailand salama, itakuwa ndiyo basi tena.”

“Haya, ngoja tuone,” alinong’ona Dk Viola, ni kweli, kwa muonekano wa sura, wasingeweza kujulikana, lakini je, ingekuwa hivyo milele? Hakuwa na uhakika, ndani ya moyo wake aliamini kabisa kwamba ipo siku kila kitu kingewekwa wazi na wao kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Gari la wagonjwa walilokodisha, liliwapeleka moja kwa moja mpaka Hoteli ya Pattaya nje kidogo ya mji huo, huko wangepumzika huku wakiendelea na taratibu nyingine zote za kutafuta vibali na hatimaye kurejea nchini Tanzania.

“Ili tufanikiwe ni lazima tupate mtu.”
“Kama yupi?”
“Tutaongea na Dk Jeremy Ho, tutalazimika kumweleza kila kitu huku tukimuahidi kiasi kikubwa cha fedha ili kufanikisha mpango uliopo mbele yetu.”
“Safi kabisa.”

Waliongea yote hayo gari likikatisha barabara kwa mwendo wa kasi na hatimaye saa moja na nusu tu tayari walishafika kwenye hoteli hiyo, hapo wakashuka na kuingia mapokezi ambako walikaribishwa kisha kuomba kupata chumba ambacho wangepumzika wakisubiri kuanza kwa mchakato mzima ambao ungewawezesha kuondoka Thailand salama.

“Tutamshikisha Dk Ho ambaye tunaamini kabisa kwa fedha ambayo tutampa, itatosha kutusaidia kupata tunachohitaji.”

Kama akili zao zilivyofikiri, ndivyo ilivyokuwa, baada tu ya kuingia chumbani, walichukua simu na kuongea na Dk Ho wakimweleza kila kitu bila kuficha na msaada waliouhitaji kutoka kwake wakimtaka ataje kiasi chochote cha fedha ambacho angekihitaji ili mradi tu awasaidie na kuondoka Thailand salama.

“Niko tayari kuwasaidia wateja wangu.”
“Ahsante na malipo yatagharimu kiasi gani?”
“Aah! Dola elfu kumi na tano.”
“Oh! Ni sawa na shilingi milioni thelathini na mbili za Kitanzania,” aliongea Vanessa.
“Itakuwa hivyo.”

“Fedha kwetu si tatizo, tunataka uhakikishe mpango huu unakamilika haraka sana na sisi kuondoka kwenda Afrika.”
“Kazi inaanza mara moja na kwa sababu hivi sasa mnatafutwa ni vyema mkahama hiyo hoteli na kwenda hoteli nyingine, nitakuwa nawasiliana nanyi kwa kutumia mtu ambaye atafanya kazi hiyo kwa niaba yangu mimi.”

“Tunasubiri maelekezo yako daktari.”
Wakiwa hotelini waliendelea kujifungia huku wakifanya mawasiliano na Dk Ho ambaye alifanya kazi akihakikisha wateja wake hao wanapata hati bandia za kusafiria na kuondoka kuelekea walikotaka kwenda.

Kwa muda wa siku mbili nzima mchakato ulikuwa ukifanywa, kwanza walihamishwa kwenda kwenye hoteli nyingine ya hadhi za chini wakiamini huko wasingejulikana lakini pia hati bandia zikatafutwa na hatimaye zikapatikana na kukabidhiwa kisha kumshukuru Dk Ho na kumpatia kiasi chote cha fedha walichokubaliana kisha wao kupanda ndege ya Shirika la Thai Air kurejea Afrika.

***
Mambo yote hayo yaliendelea ndani ya vichwa vyao wakiwa juu ya vitanda vyao ndani ya Hoteli ya Serena walijiona washindi na kuamini kwamba fedha ziliweza kufanya kila kitu na hatimaye waliweza tena kurejea nyumbani kwa njia na sura tofauti katika mwavuli wa uwekezaji bila Watanzania kufahamu kwamba watu waliokuwa mbele yao ni wahalifu waliosakwa na Polisi wa Interpol, Scotland Yard na CIA.

“Huu ni ushindi mkubwa kwetu, wajinga ndiyo waliwao, hakuna anayejua jambo hili, kwa sababu ya fedha zetu, ha! Ha! Haa sisi ni noma kweli,” Vanessa aliongea akimalizia na kicheko.

“Yaani wakati unaongea pale ikulu kicheko kilinibana, maskini wa Mungu, watu wametupokea vizuri, wametukubali wakituona wakombozi wao kumbe wangejua…” Dk Viola aliongea lakini kabla hajamalizia mlango wa chumba chao uligongwa kwa sauti.

JE, nini kitaendelea? Nani amegonga mlango wa chumba chao? Nini kitawapata? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.


Loading...

Toa comment