Mabilionea wasio na huruma 43

US+dollar+dollars+USAIBU inakaribia kuibuka, baada ya wawekezaji wakubwa wawili walioalikwa kwa ajili ya dhifa iliyoandaliwa na rais kushindwa kutokea huku muda nao ukizidi kusonga mbele. Hakuna anayejua kilichotokea ni nini hadi wageni hao, bwana Chu na Hui, wawekezaji kutoka Thailand, washindwe kufika kwenye dhifa hadi wakati huo, wasiwasi unaanza kumkumba waziri mwenye dhamana, hasa ukizingatia tayari wageni waalikwa wameshajazana kwa wingi kwenye viwanja vya ikulu.

Upande wa pili, bwana Chu na Hui, wakiwa chumbani hotelini, wanapata wasiwasi mkubwa baada ya kusikia mlango wa chumbani kwao ukigongwa kwa nguvu. Hawapo tayari kufungua mlango, kwani wanajua pengine wanaweza kukamatwa na kujikuta wakiwa kwenye aibu kubwa. Wanafikiria kujirusha dirishani, wafe kabla ya kukamatwa.

Je, wawekezaji hao watajiua kweli? Je, kule viwanjani mambo yatakuwaje kama wageni wao hawatafika huku watu wengi mashuhuri wakiwa wameshafika?SONGA NAYO…

WOTE walikuwa wamechanganyikiwa, maisha yao sasa ni kama yalikuwa yamefika mwisho baada ya kukimbia mkono wa sheria kwa muda mrefu. Hawakuwa tayari kuingia mikononi mwa polisi, kwao ilikuwa ni heri kutangulia kuzimu kuliko kupitia mateso na fedheha ambazo wangezipata baada ya kujulikana kwamba ni wauaji walioua watu wengi kwa kuwaibia figo zao na mwisho wakaangusha ndege na kulipwa fidia zote za yatima 62 waliokuwa wakisafiri kutoka Tanzania kwenda nchini Uingereza.
“Ni bora kufa!”

“Kabisa.”
“Hebu chungulia kwenye tundu la mlangoni uone kuna akina nani kabla hatujajirusha na kufa,” bwana Chu alisema.

Haraka bwana Hui akajiondoa mikononi mwa Chu na kwenda moja kwa moja hadi mlangoni na kuchungulia kupitia kwenye tundu dogo la kuonea nje lililokuwa kwenye mlango, alichokiona huko kilimfanya atetemeke na hofu kuongezeka.
“Vipi?”

“Kuna watu wawili wamevaa suti na miwani ya rangi nyeusi.”
“Hakika hao ni polisi.”
“Sasa tufanye nini?”
“Uamuzi ni ule ule wa mwanzo, turuke.”
“Sawa!”

Bwana Hui akaanza kulifungua dirisha tayari kwa kuruka, ghafla simu iliyokuwa kando ya kitanda ikalia, kwa kasi bwana Chu akaifuata na kuinyanyua kisha kuanza kusikiliza upande wa pili kabla ya kuongea chochote.
“Hallo, nani mwenzangu, Waziri wa Biashara na Utalii anaongea.”
“Aaah! Mheshimiwa Waziri, naitwa Chu!”
“Chu?”

“Ndiyo!”
“Umeelewa Kiswahili mara hii?”
“Niliwahi kujifunza miaka ya nyuma.”
“Mbona Kiswahili chako kizuri kuliko changu?”
“Mimi mwepesi sana wa kuelewa lugha.”
“Mh!”

“Mbona umeguna?”
“Nashangaa, tutaongea vizuri tukikutana, kuna vijana wangu nimewatuma hapo kuwafuata, wapo nje ya mlango wenu wanagonga lakini hamfungui na huku tayari watu wamejaa ukumbini, mnasubiriwa ninyi tu kabla Mheshimiwa Rais hajaingia.”
“Pyuuu!” Bwana Chu alishusha pumzi, mara moja sura yake ikajawa na tabasamu.
“Upo bwana Chu?”

“Ndiyo nipo!”
“Mbona umeshusha pumzi?”
“Basi tu, tunakuja.”
Bwana Chu akakata simu na kumkimbilia bwana Hui, akamsimulia kila kitu alichoongea na Mheshimiwa Jamhuri Azimio, wakakumbatiana kwa furaha huku wakielekea mlangoni baada ya kugundua kwamba kumbe waliokuwa nje hawakuwa askari, bali maafisa wa ikulu.

“Hili jambo litatupasua mishipa ya ubongo, kama mtu angenipima presha hakika ingekuwa hata elfu moja chini ya mia tano!”

“Mimi mkojo ulishanipenya,” walinong’onezana kabla hawajafungua mlango na walipofanya hivyo maafisa wawili waliovalia suti nyeusi, waliingia na kujitambulisha.
“Subirini kidogo tujiandae!”
“Hakuna shida, ila tumechelewa maana tumegonga kwa muda mrefu sana.”
“Tulikuwa tunasali!”

Maafisa walitoka nje ambako walisubiri kwa dakika kumi na tano kabla bwana Chu na Hui hawajatokeza wakiwa wamevalia suti zao nyeusi na tai nyekundu, kama mapacha! Wote wakaingia kwenye lifti na kushuka hadi chini ambako waliingia ndani ya gari aina ya benzi iliyokuwa ikiwasubiri karibu kabisa na lango kuu la kuingilia Hoteli ya Serena, mmoja wa maafisa wa ikulu akawafungulia mlango wa nyuma, wakaingia na kuketi.

Safari kuelekea ikulu ikaanza wakiwa kimya, hapakuwa mbali sana, kama mita mia mbili hivi kutoka katika Hoteli ya Serena, gari likaegeshwa ndani ya ikulu, nao wakashuka na kuanza kutembea kuelekea ukumbini baada ya kupokewa na Waziri wa Biashara na Utalii na Maofisa wengine wa ikulu.
“Umenishangaza sana bwana Chu!”
“Kwa nini?”

“Kiswahili chako.”
“Miaka mingi nilipanga kuja kuwekeza Afrika, hivyo nikaamua kabisa kujifunza Kiswahili Chuo Kikuu cha London!”

“Oh! Hata bwana Hui anaongea Kiswahili pia?”
“Huyo ndiye mpemba kabisa.”
“Safii, hiyo itafanya kuishi kwenu hapa Tanzania kuwe rahisi maana ukiongea sana Kiingereza hapa lazima watu wakupunje kila kitu unachotaka kununua.”
“Hawawezi, sisi ni Wajapan wa mtaani!”

Tayari walishaingia ukumbini ambako watu wote walisimama na kuwapigia makofi wawekezaji, wakaketi kwenye meza maalum ambako muda mfupi baadaye, rais aliingia na kuungana nao, dhifa ikaanza kwa wimbo wa taifa na baadaye hotuba mbalimbali kutoka kwa rais na serikali, kisha bwana Chu na Hui, halafu yakafuata mambo ya maakuli, vinywaji na utambulisho, viongozi wa Serikali ya Tanzania wakiwafurahia wawekezaji bila kufahamu walikuwa ni watu hatari ambao dunia ilikuwa ikiwasaka.

Dhifa iliendelea mpaka saa tano usiku ndipo bwana Chu na Hui wakarejea hotelini ambako walianza kutafakari tena juu ya mahali mambo yalipokuwa yamefika, hapakuwa na namna yoyote ya kurudi nyuma, ilikuwa ni lazima kusonga mbele kama wawekezaji na kwa jinsi mapokezi na heshima waliyopewa, wakawa na uhakika kabisa hakuna mwanadamu yeyote angehisi kwamba wao ndiyo Dk Viola na nduguye Vanessa ambao dunia ilikuwa ikiwasaka kwa gharama yoyote.

“Kinachofuata sasa hivi ni ujenzi wa Dar es Salaam New City, uwekezaji tutakaoweka pale, misaada tutakayotoa kwa serikali na kodi tutakayokuwa tukilipa, itawafanya Watanzania watuone ni kama miungu, hakuna atakayetugusa!”
“Kweli kabisa.”

“Tutafute kampuni ya uchoraji wa ramani kutoka Dubai, ya ujenzi kutoka China ambao tutawakabidhi kazi ya kuujenga huo mji mpya, ndani ya miaka mitano lazima uwe umekamilika ili tuanze kuingiza fedha!”

“Tutatumia kiasi gani?” bwana Hui aliuliza.
“Dola milioni mia sita zinatosha kwa kuanzia.”
“Ni sawa.”
“Lakini ni lazima tuhakikishe watu wote wanaofanya upelelezi wa kutusaka, popote walipo duniani wanakufa, huo ndiyo utakuwa usalama wetu, vinginevyo uwekezaji wote tunaoufanya utakuwa hauna maana!”

JE, nini kitafuata? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.


Loading...

Toa comment